Wanawake Tanzania wavutwa ajenda ya mwanamke, hatua ya mabadiliko katika siasa

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 03:47 PM Nov 28 2024
Wanavituo vya Taarifa na Maarifa Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam
Picha: Grace Mwakalinga
Wanavituo vya Taarifa na Maarifa Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam

AJENDA ya Mwanamke, Turufu ya Ushindi ilianzishwa mwaka 2015 kama juhudi ya kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na kutoa msukumo wa kutatua changamoto zinazowakabili wanawake kwenye uchaguzi na uongozi.

 Ajenda hiyo imeleta mabadiliko makubwa na ya kihistoria kwa wanawake wengi, ikiwasaidia kugombea nafasi za uongozi na  baadhi yao kufanikiwa kushinda.

Imeongeza uwakilishi wa wanawake katika siasa, na hivyo kupunguza pengo la kijinsia katika majukwaa ya uongozi.

Lilian Liundi, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), anasema kuwa malengo ya ajenda hiyo ni kuchochea mabadiliko ya kijinsia na kupunguza vikwazo na mitazamo hasi kuhusu uwezo wa wanawake kuwa viongozi.

 “Ajenda hii inapunguza changamoto za rushwa ya ngono, ukosefu wa fedha za kampeni, na ukosefu wa elimu na kuwapatia msaada wa kisheria wanawake wanaoshiriki katika uchaguzi wanapohitaji,” anasema Liundi.

MATUNDA YA AJENDA HII

Wanaharakati kutoka Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, wamefanikiwa kuhamasisha wanawake kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

 Agness Benedicto, mwanaharakati wa kituo hicho, ni mfano wa mafanikio ya juhudi hizo, anasema kuwa kupitia hamasa na elimu aliyopewa na TGNP, amegombea na kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya ujumbe mchanganyiko kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ushindi wangu ni ushahidi wa umuhimu wa kuwa na mifumo inayowawezesha wanawake kushiriki siasa. Wanawake wengi wana uwezo mkubwa, lakini wanakumbana na changamoto zinazokatisha tamaa,” anasema Agness.

Kwa mujibu wa Agness, Kata ya Mabwepande, wanawake 10 walijitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, huku saba kati yao wakigombea nafasi ya uenyekiti kupitia CCM.

Hata hivyo, amedai imekuwa ni maamuzi ya vyama vya siasa kuwateua wagombea wasio chaguo la wananchi, jambo linalowakatisha tamaa  wanawake wengi  ambao wameenguliwa.

CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WANAWAKE

Wanaharakati wanabainisha changamoto kubwa zinazowakabili wanawake katika siasa, hasa rushwa ya ngono na ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kampeni.

 “Wanawake wameshindwa kumudu gharama za kampeni, hali inayopunguza ushiriki wao kwenye uchaguzi,” anasema Asha Daudi, mjumbe wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Mabwepande.

Sarah Mwakanyamale, Katibu Msaidizi wa kituo hicho, anasema ingawa idadi ya wanawake wanaogombea imeongezeka, changamoto za kifedha na kijamii bado ni vikwazo kikubwa.

Anna Sangai, Ofisa Mafunzo wa TGNP, anatoa wito kwa vyama vya siasa kuweka ruzuku kwa wanawake wanaogombea uongozi katika uchaguzi ujao.

 “Wanawake wengi wana ndoto za kuongoza, lakini  ukosefu wa rasilimali fedha umekwamisha kufikia malengo yao,”Sangai.

UCHAMBUZI WA USHIRIKI WA WANAWAKE

Ripoti ya TGNP inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanawake wanaotamani kushiriki siasa wanakabiliwa na changamoto za kifedha, huku asilimia 40 wakikumbana na vikwazo vya kijamii kama vile mila potofu.

Licha ya changamoto hizi, TGNP inaendelea kutoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake na kuhamasisha jamii kupinga vitendo vya rushwa ya ngono.

Ushiriki wa wanawake kama Agness Benedicto ni hatua muhimu kuelekea usawa wa kijinsia katika siasa.

 Hatua hii inahitaji kuungwa mkono na wadau wote wa jamii, serikali, na vyama vya siasa ili kuhakikisha kuwa wanawake wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uongozi na uchaguzi.

 

Wanavituo vya Taarifa na Maarifa Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.