Mo atoa neno Simba, hesabu kwa Tabora Utd

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:13 AM Jan 22 2025
Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji
Picha: Mtandao
Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji

WAKATI Klabu ya Simba ikitangaza kuwa baada ya kumaliza mchezo wake dhidi ya CS Constantine, hesabu zote sasa zipo kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United, Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji, amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kujituma uwanjani kiasi cha kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho.

Akitoa salamu za pongeza jana, Dewji, ambaye ni Rais wa Heshima wa klabu hiyo, alisema kikosi cha timu hiyo kinaundwa na wachezaji wengi vijana wadogo, ambao ni wapya kwenye timu, wasio na uzoefu kwenye michezo mingi ya kimataifa, lakini wamekuwa wakijituma kweli kweli uwanjani na kuipatia ushindi, wakati mwingine ukiwa ni wa kushangaza kwenye dakika za majeruhi.

"Niwapongeze wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba kwa mshikamano na mafanikio makubwa yaliyopatikana tunayoshuhudia. Mafanikio haya si kazi ya mtu mmoja ni juhudi za familia mzima ya Wanasimba wote, pamoja na serikali yetu.

"Kufuzu kwetu robo fainali ya Kombe la Shirikisho ni hatua muhimu kuelekea ndoto yetu ya kuleta taji la Afrika kwenye michezo ya kimataifa nyumbani. Tuna ndoto kubwa na tunapambana kwa bidii kuzitimiza. Lakini namalizika kwa pongezi za pekee kwa wachezaji wetu, wamekuwa wakijituma sana hadi kutufikisha hapa tulipo," alisema Mo.

Wakati huo huo, kikosi cha Simba kimepewa mapumziko ya siku nne, baada ya hapo kinatakiwa kurejea kwa ajili ya mchezo wa Kombe la FA, pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United unaotarajiwa kupigwa Februari Mosi, mwaka huu, katika Uwanja Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema macho na hesabu zao wanazielekeza zaidi kwenye mchezo huo wa Februari Mosi dhidi ya Tabora United.

Alisema wanauchukuliwa kwa uzito mkubwa mchezo huo na watakwenda kwa tahadhari zote.

"Tunakwenda kukabiliana na Tabora United, haitokuwa mechi nyepesi hata kidogo, lakini tutakwenda kwa ajili ya kupata matokeo mazuri. Sijajua ubora wa Tabora United uko wapi, ila ninachojua wanaweza kushinda michezo migumu, na kama ni hivyo hata sisi tunawajibika kwenda kwa tahadhari kubwa ili wasije kupata pia ushindi mbele yetu," alisema.

Tabora United ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, Novemba 7, na kisha kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Singida Black Stars Novemba 25, kabla ya kuichapa Azam FC 2-1, Desemba 13, mwaka jana.

Alisema kwa hali ambayo ligi imefika hawapaswi kudondosha hata pointi moja, hivyo hawako tayari kupoteza mchezo huo.

"Katika ligi hii ilipofika ukiruhusu hata kupoteza pointi moja umesharuhusu mpinzani wako akufikie na kukupita kwa hiyo tunawajibika kuifunga Tabora na ni moja ya michezo migumu tuliyonayo mwezi Februari," alisema Ahmed.