Metacha, Chalamanda watisha uokoaji penalti

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:49 AM Jan 20 2025
Metcha Mnata.
Picha: Mtandao
Metcha Mnata.

JUMLA ya magolikipa watano wa Ligi Kuu Bara, wameokoa mikwaju ya penalti hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na Bodi ya Ligi, makipa hao kila mmoja ameokoa penalti moja. Hakuna kipa yeyote aliyeokoa zaidi ya penalti moja, huku wengine wakifungwa na baadhi timu zao hazijaruhusu adhabu hiyo kubwa kwenye lango lao.

Makipa waliocheza penalti mpaka sasa ni Metcha Mnata wa Singida Black Stars na Hussein Masalanga, ambaye amerejea Klabu ya Singida Black Stars, baada ya kucheza kwa mkopo Tabora United. Hata hivyo penalti aliyookoa ilikuwa kwenye kikosi cha Tabora United.

Wengine ni Jonathan Nahimana wa Namungo FC, Ley Matampi wa Coastal Union ambaye kwa sasa amevunja mkataba na klabu hiyo, baada ya dirisha dogo la uhamisho lilipofunguliwa Desemba 15, mwaka jana na Ramadhani Chalamanda wa Kagera Sugar.

Takwimu hizo za Bodi ya Ligi, zimeitaja Simba kuwa ndiyo timu iliyopata penalti nyingi kwenye Ligi Kuu mpaka sasa.

Timu hiyo imepata penalti sita mpaka kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Takwimu cha Dawati la Michezo la Nipashe ni kwamba, Simba imefunga penalti zake zote, kupitia kwa Jean Ahoua na Leonel Ateba, kila mmoja akifunga tatu.

Timu za Coastal Union, Namungo na Tabora United kila moja imebahatika kupata penalti tano, huku Azam FC, Fountain Gate na Yanga zikipata penalti tatu kila moja.