Majaliwa mgeni Betika Tulia Mbeya Marathon

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 10:38 AM May 03 2024
Meya wa Manispaa ya Newala, Hamisi Namata (watatu kushoto), akiwakabidhi bendera ya Betika washindi watano ambao wataiwakilisha Mtwara katika mbio za mwaka huu za Betika Mbeya Tulia Marathon.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meya wa Manispaa ya Newala, Hamisi Namata (watatu kushoto), akiwakabidhi bendera ya Betika washindi watano ambao wataiwakilisha Mtwara katika mbio za mwaka huu za Betika Mbeya Tulia Marathon.

WAKATI hamasa ya kushiriki ikiwa imeongezeka, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mbio ya Betika Mbeya Tulia Marathon zitakazofanyika Mei 10 na 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya.

Ofisa habari wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Edward, alisema jijini Dar es Salaam jana, maandalizi ya mbio hizo yamekamilika na Waziri Mkuu Majaliwa atakuwa na mwenyeji wake, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Joshua alisema wanatarajia wanariadha zaidi ya 5,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini watashiriki mbio za mwaka huu na baadhi ya mikoa imeanza 'amsha amsha' ikiwamo Mtwara ambao jana wadau wameshiriki mbio iliyoratibiwa na radio ya Newala FM zikiongozwa na Meya wa Manispaa ya Newala, Hamis Namata.

Meya huyo aliwakabidhi washiriki watano bendera ya Tulia Marathoni na Betika tayari kuipeperusha watakapokwenda Mbeya.

Ofisa Habari wa Betika, Rugambwa Juvelinaus, alisema wanariadha hao watalipiwa gharama zao zote na kampuni yao.

"Watu watano waliokimbia leo (jana) watagharamiwa na Betika watakapokuwa katika mbio za Betika Mbeya Tulia Marathoni," alisema Rugambwa.

Aliitaja mikoa mingine ambayo itafanya mbio 'ndogo' ili kuwaweka tayari washiriki wake ni pamoja na Dodoma, Iringa, Rukwa na Morogoro.

Alisema mbali na hao wa Mtwara, Betika pia itawagharamia wanariadha wengine  420 kutoka mkoa mwenyeji wa Mbeya na washiriki wengine 10 kutoka Dodoma, Iringa, Morogoro na Rukwa.