JKU yatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 05:53 AM Jun 23 2024
TIMU ya JKU SC.
Picha: Mtandao
TIMU ya JKU SC.

TIMU ya JKU SC imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa mwaka 2023/2024 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kipanga katika mechi ya kufunga pazia la ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan juzi.

Kwa matokeo hayo, JKU ilifikisha pointi 66 na kukaa kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ambayo ilishirikisha timu 16 kutoka Pemba na Unguja.

nafasi ya pili katika ligi hiyo ilichukuliwa na Zimamoto yenye pointi 62 huku KMKM yenye pointi 57 ilimaliza ya tatu na KVZ ilikamilisha 'Top Four' ikiwa na pointi 56.

Wakati JKU wakifurahia, Kundemba iliungana na timu za Ngome, Maendeleo na Jamhuri kushuka daraja. 

Mechi tano zilichezwa juzi katika viwanja vya Finya na Gombani vilivyoko Pemba wakati upande wa Unguja, michezo ya mwisho ilifanyika kwenye Uwanja wa Mau na Amaan.

Kundemba yenyewe ilicheza mchezo wake wa mwisho kwenye Uwanja wa Mao Zedong ambapo ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Malindi SC, matokeo ambayo hayakuwasaidia kujinusuru na janga la kushuka daraja wakati New City walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Zimamoto.

KVZ ilimaliza ligi hiyo kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Jamhuri, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Funya huku Hard Rock ikiwaadhibu Maendeleo United kwa mabao 4-1, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Gombani.

Kundemba iliyojikusanyia pointi 35 ilimaliza kwenye nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi hiyo ikifuatiwa na Ngome yenye alama  27 wakati Jamhuri wamemaliza msimu wakiwa na pointi 20 na Maendeleo waliburuza mkia kutokana na kujikusanyia alama 15 tu kwa msimu mzima.

JKU rasmi sasa itaiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao huku Chipukizi ya Pemba, ambao ni mabingwa wa Kombe la ZFF (Shirikisho la Soka Zanzibar), wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.