Gamondi, Taoussi mechi ya marafiki

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:53 PM Nov 02 2024
Gamondi, Taoussi  mechi ya marafiki.
Picha:Mtandao
Gamondi, Taoussi mechi ya marafiki.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema watapambana na Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, kwa namna 'watakavyokuja'.

Gamondi amesema watawaangalia kwanza Azam jinsi watakavyocheza ili nao wajue namba ya kukabiliana nao na hatimaye kupata ushindi katika mchezo huo.

Kocha huyo alisema kwa sasa timu nyingi zinapokutana na Yanga zinacheza mtindo  tofauti, nyingine zikicheza kwa kukamia  zaidi, mpira mirefu, ubabe, hivyo yeye atapanga mbinu baada ya kubaini mfumo wao.

"Azam ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri mno, wana kocha mzuri kwa hiyo haitakuwa mechi ya kitoto, lakini tunafanya kila kitu kwa ajili ya ushindi, katika soka chochote kinaweza kutokea, kila timu ikija inataka kupambana na sisi kwa njia tofauti, wakati mwingine kuonyesha ubabe, lakini tunapambana kadri ya uwezo wetu, kwa jinsi timu inavyokuja ndiyo tunajua tupambane vipi," alisema Gamondi.

Aliongeza itakuwa furaha kwake kucheza na timu inayofundishwa na 'rafiki' (Rachid Taoussi), ambaye amewahi kufanya naye kazi, hivyo wanafahamiana.

"Nadhani tutakuwa na mchezo mzuri dhidi ya Azam, itakuwa mechi nzuri sana kwangu kwa sababu kocha wa timu hiyo ni rafiki yangu sana, tuliwahi kufanya kazi pamoja, tunafahamiana kwa miaka 25 iliyopita," Gamondi alisema.

Aliisifia Azam ni timu nzuri kutokana na kuundwa na wachezaji wenye viwango vizuri.

Naye Taoussi amesema anapenda sana kucheza michezo migumu kama hiyo.

"Tunakwenda kucheza mechi kubwa, huwa napenda michezo ya aina hii kwa sababu hata sisi Azam ni timu kubwa hapa Tanzania, tuna wachezaji wakubwa, nadhani kama sita hivi wanacheza kwenye kikosi cha timu ya taifa.

Nataka kwenda kushinda mchezo dhidi ya rafiki yangu Gamondi, namfahamu sana na yeye ananifahamu kitambo tu, kifupi tunafahamiana sana," alisema Taoussi.