Hii hapa sababu kifo cha King Kikii, Samia amlilia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:43 AM Nov 15 2024
Boniface Kikumbi maarufu 'King Kikii',
Picha:Mtandao
Boniface Kikumbi maarufu 'King Kikii',

Mtoto wa marehemu msanii mkongwe wa muziki wa dansi Tanzania, Boniface Kikumbi maarufu 'King Kikii', Joseph Silumbe amesema baba yake amefariki kwa maradhi ya saratani ya ini.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 15, 2024 wakati akizungumza na Wasafi Radio.

"Ana miaka kama mitano, sita alikuwa anaugua, mara ya kwanza alifanyiwa upasuaji wa pingili za mgongo hapa shingoni baada ya hapo tukampeleka India na nilikuwa nae mimi mwenyewe, tulikaa mwezi mmoja. Wakamuwekea pampu moja ya kujisaidia kwa sababu alikuwa kama amepooza miguu na mikono.

"Baada ya kurudi hapa (nchini) akawa amedhohofika kidogo hivi karibuni tukamrudisha hospitali walivyofanya vipimo wakagundua tezi dume imerudi tena ikawa imeongezea na saratani ya ini,"amesema Joseph

King Kiki amefariki akiwa na umri wa miaka 77, enzi za uhai wake alitamba na vibao mbalimbali kikiwemo maarufu cha ‘Kitambaa Cheupe’.

Taarifa za kifo cha King Kikii zimethibitishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa asubuhi ya leo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Ameandikwa “Lala salama mzee wetu Boniface Kikumbi Mwanza Mpango (King Kikii), mwanamuziki mkongwe, jabali la rhumba na mtu mwenye utumishi uliotukuka katika tasnia ya muziki Tanzania.

“Tutauenzi mchango wako mkubwa katika muziki wa dansi Tanzania. Kwa miaka mingi umeburudisha, umefundisha, umeelimisha na uliipenda sana Tanzania,” ameandika Msigwa.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

RAIS SAMIA ATUMA SALAMU ZA POLE 

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kutokana na kifo cha nguli wa muziki wa dansi Tanzania, Boniface Kikumbi maarufu King Kikii.

Salamu hizo amezitoa kupitia mitandao yake ya kijamii leo Ijumaa Novemba 15, 2024.

“Ninatoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, wasanii na wapenzi wote wa muziki nchini kufuatia kifo cha mwanamuziki nguli Boniface Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’.

“Kwa zaidi ya miaka 50 King Kikii ametoa burudani kwa mamilioni ya Watanzania na amekuwa mlezi na mwalimu wa wengi katika tasnia ya muziki. Tutamkumbuka na kumuenzi kwa kazi zake nyingi na nzuri ikiwemo wimbo wake maarufu wa ‘Kitambaa Cheupe’ ambao umeendelea kuwa sehemu ya burudani kwenye maeneo na shughuli mbalimbali za burudani nchini,” ameandika Rais Samia