NAFIKA kijiweni nakutana na mazungumzo makali kuhusu watu kujichukulia sheria mkononi. Jamaa wanabishana, upande mmoja ukiunga mkono na mwingine ukipinga.
Wanaounga mkono wanasema wizi umekithiri na wanaokamatwa wakifika Polisi wanaachwa, ama kwa kukosa ushahidi au kwa rushwa, hivyo kurejea mitaani kusumbua watu.
Wanaopinga wanasema si ubinadamu kumpiga mtu na kumwua kwa kumchoma moto, kwa sababu wengine husingiziwa na kujikuta ama wakipoteza maisha au kupata kilema cha maisha.
Mara mmoja anaibuka na ushuhuda wa kujichukulia sheria mkononi, akihusisha na mafuta ya transfoma, akisema kuna kiongozi kadai kuwa kutokana na kukithiri wizi wa mafuta hayo, watuhumiwa wamekuwa wakinyweshwa na sasa wizi umekoma.
Sikuamini, nikamtaka arudie ushuhuda huo na kunithibitishia kuwa ni kweli kiongozi huyo kakiri kufanyika hilo, tena akionesha kufurahia hatua hiyo dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa mafuta.
Kwa kweli bado niliendelea kutoamini kitendo hicho, huku nikifikiria pengine ni utani au maskhara ya kiongozi huyo, kama ambavyo mmoja alipata kutoa amri, kuwa shabiki wa soka asiingie uwanjani amevaa jezi ya timu pinzani ya kigeni.
Baada ya wanachi kulalamikia hatua hiyo iliyokuwa inalenga kulazimisha watu waipende na kuishangilia timu yao yaTaifa, ikimtaka kila Mtanzania anayeingia uwanjani ashabikie Taifa Stars, wananchi walitaka ufafanuzi.
Walishangaa kusikia eti atakayekwenda amevalia jezi ya timu pinzani basi lazima awe na pasipoti ikimwonesha anatoka nchi itokayo timu hiyo.
Hata hivyo hakufafanua, mpaka alipoibuka kiongozi mwingine na kudai kumbe mwenziwe alikuwa akitania!
Kwa hicho kilichokuwa utani nami nikaamini pengine hata aliyesema walinyweshwa mafuta ya transfoma alikuwa akitania, sawa na yule aliyeambia wananchi mkoani mwake, kuwa katika ziara ya Rais waibuke kwenye mikutano yake wakiwa na mabango ya kero mikononi.
Sikumbuki vizuri alikuwa nani, lakini nadhani aling’olewa uongozi wake na kurejea nyumbani.
Na kama ikitokea amerejea, nitaamini kuwa alikuwa naye anatania siku hiyo kwa wananchi wake.
Bado, wakati natafakari hayo, hili la mafuta ya transfoma liliendelea kunikereketa hasa nikihisi jinsi gani jamaa walikuwa wakifakamizwa, hasa nikikumbuka ladha ya mafuta ya taa niliyopata kuionja nikiwa mdogo.
Nikajihoji, hivi mathalan umekithiri wizi wa tindikali katika maabara zetu, je, kwa msimamo wa kiongozi wetu huyo, watuhumiwa wakipatikana watanyweshwa tindikali au itakuwaje?
Je, wezi wa nyama buchani watalishwa nyama mbichi? Wezi wa damu kwenye benki ya damu hospitalini je? Wezi wa saruji watabugizwa mifuko ya saruji ili wakome kuiba au itakuwaje?
Pengine hizo ndizo adhabu zisizozingatia utu na ubinadamu kabisa. Wakati adhabu kama hizi zikiendelea kutolewa na wenye dhamana ya kusimamia usalama wa raia na mali zao, bila shaka tunasubiri kusikia kuwa huo ulikuwa ni utani tu na hakuna kitu kama hicho, na kama itakuwa hivyo, tutaomba kuambiwa usio utani ni upi!
Lakini kama ni kweli kuwa kuna watu walinyweshwa mafuta ya transfoma baada ya kuyaiba na si kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili haki iweze kutendeka, basi kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hivi sasa.
Kwa maana hiyo, bila kupepesa macho, kama hakika kuna kiongozi alishiriki kadhia hii, anapaswa kupisha na kukaa pembeni, ili sheria ifuate mkondo kwa tuhuma za mataumizi mabaya ya madaraka na ukatili dhidi ya binadamu.
Lakini endapo itashikiliwa kuwa hawakunywa bali waliigiza au kutania, basi tuamini kuwa mambo mengi yanayoahidiwa na viongozi nchini, ni utani na hayatakuja kutekelezwa kwa maslahi mapana ya nchi na watu wake.
Ndiyo kusema wananchi wenye matatizo ya msingi na waliokwisha kutoa malalamiko yao, basi wajue ahadi zinazotolewa kwao ni utani na hawatakaa wasaidiwe, bali kumwachia Mungu awaamulie mustakabali wao.
Ndugu zangu wa Kipunguni mpo? Nakusalimuni kwa jina la Kipunguni na utani uendelee!
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED