KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwenda kwa wingi leo, Uwanja wa Benjamin Mkapa, kushuhudia soka safi litakalochezwa na vijana wake dhidi ya Red Arrows kutoka Zambia katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi.
Gamondi amesema mchezo wa leo sio wa kusaka pointi wala ushindi kwa ajili ya kombe lolote, hivyo anataka wachezaji wake wafurahie soka, na ushindi utakuja kama wakitandaza soka safi ambalo anataka wacheze.
"Ni Siku ya Mwananchi, najua kutakuwa na watu wengi uwanjani, kutafurika mashabiki, najua hili kwa sababu msimu uliopita nilishuhudia pale, lilikuwa ni moja kati ya tukio langu bora sana kuliona, naamini safari hii itakuwa hivyo hivyo, ingawa pia nadhani inawezekana kuna vitu vikaongezeka zaidi kwa sababu tumefanya vyema msimu uliopita," alisema Gamondi.
Alisema katika mechi ya leo atajitahidi kuchezesha wachezaji wengi, kila mchezaji apate dakika kadhaa ya kucheza.
"Siyo kama naidharau Red Arrows, ni timu nzuri, najua na wao wamekuja kupambana, lakini ukweli unabaki pale pale leo ni burudani zaidi kuliko ushindani, ingawa hii haiwezi kutufanya tusitafute ushindi kwa ajili ya furaha ya mashabiki wetu," alisema.
Yanga inakwenda kucheza dhidi ya Red Arrows, ambayo hivi karibuni ilitwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama 'Kagame Cup', michuano ilifanyika nchini Tanzania kwenye viwanja vya KMC, Mwenge na Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Tamasha la leo litakuwa la sita kufanywa na klabu hiyo, ambapo kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2019 ikicheza dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya na kutoka sare ya bao 1-1.
Lilifanyika kwa mara ya kwanza miaka 10 baada ya klabu ya Simba kuasisi tamasha la 'Simba Day' mwaka 2009.
Kama lilivyokuwa kwa watani wao jana, tamasha hilo litaanza asubuhi, ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii na bendi za muziki wa dansi, kabla ya michezo kadhaa ya mpira wa miguu kuanza na baadaye kuanza kutambulisha wachezaji wa zamani na wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano na litahitimishwa kwa mchezo huo wa kirafiki.
Wanachama na mashabiki wa Yanga kwa mara ya kwanza watawashuhudia wachezaji wao wapya waliosajiliwa, wakicheza katika ardhi ya Tanzania baada ya kuwashuhudia kwenye runinga nchini Afrika Kusini.
Baadhi ya wachezaji hao ni Clatous Chama aliyetoka Simba, Prince Dube aliyesajiliwa kutoka Azam FC, Duke Abuya kutoka Singida Black Stars, Aziz Andambwile, akitokea Singida Fountain Gate.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED