Fadlu: Simba imeimarika asilimia 58 tu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:20 AM Feb 04 2025
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

PAMOJA na ushindi wa mabao 3-0, ilioupata kutoka kwa Tabora United juzi, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kikosi chake sasa kimeimarika kwa asilimia 58, akifafanua kuwa bado anaendelea kukijenga ili kifike pale anapohitaji, huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri walioifanya kwenye mchezo huo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa raundi ya 16 ya Ligi Kuu dhidi ya Tabora United, uliochezwa, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Fadlu alisema wachezaji wake walifanya kile ambacho aliwaelekeza kwa asilimia nyingi sana.

"Tulitaka kucheza kama hivi tulivyocheza, tulipata bao la mapema, tukaongeza mengine, tumeondoka na 'clean sheets' nyingine pia.

"Tunachokifanyia kazi kwa sasa ni jinsi gani ya kuzifungua timu ambazo zina tabia ya kukaa nyuma ya mpira na tumeanza kufanikiwa tangu kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, dhidi ya CS Constantine, nadhani kipindi cha pili ndiyo Tabora United walianza kufunguka.

"Nawapongeza wachezaji wangu kwa kile walichokifanya mbele ya Tabora United, sasa tunajiandaa na mchezo dhidi ya Fountain Gate ambao ni miongoni mwa mechi ngumu za ugenini," alisema.

Fadlu aliingia ndani kiufundi, akisema waliweza kuidhibiti Tabora United sehemu zote za ubora wao.

"Hatukuruhusu mashambulizi yao ya kushtukiza, tukaziba mianya yote pembezoni mwa uwanja, tukaubana uwanja tukiwa kwenye eneo letu kuhakikisha washambuliaji wao wanakosa uhuru.

"Pia hatukuruhusu mipira ya pili, inayoanguka kwenye eneo letu, tukapunguza makosa yetu ya kiulinzi na kuboresha zaidi katika eneo la ushambuliaji," alisema.

Alisema kwa sasa kikosi chake kimeimarika kwa asilimia 58, na bado anaendelea kukijenga ili kiwe imara zaidi.

"Bado kikosi hakijakamilika kwa asilimia zote, tunaendelea kukijenga taratibu na nina imani kitafikia kule ambapo tunahitaji," alisema.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, yeye alisema wametimiza azma yao ya kuzilipia kisasi timu zote za Dar es Salaam zilizofungwa na Tabora United.

"Haiwezekani timu ya Dar es Salaam ikafanywa mnyonge, kwa hiyo tumemlipia kila Mwana-Dar , ambaye alidhuriwa kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kwa hiyo jukumu hilo tumelimaliza, inafaa sasa tupongezwe kwa hilo," alisema Ahmed.

Tabora United iliifunga Yanga mabao 3-1, mechi iliyochezwa, Novemba 7, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ikapata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC, Novemba 29, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Desemba 13, mwaka jana, iliichapa Azam FC mabao 2-1, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora. Timu zote hizo maskani yake ni Dar es Salaam.

Kocha wa Tabora United, Anicet Makiadi, yeye alimpongeza Kocha Fadlu pamoja na timu yake kwa ushindi walioupata, akisema kupoteza mchezo huo ni sehemu ya soka, akijipanga upya kwa michezo mingine.

Ushindi huo umeifanya Simba kurejea kileleni ikiwa na pointi 43, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 42.

Simba inashuka tena uwanjani keshokutwa, Alhamisi katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, mkoani Manyara kucheza dhidi ya Fountain Gate.