Benchikha achambua washambuliaji Ligi Kuu

By Saada Akida , Nipashe
Published at 06:22 AM Apr 17 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.
Picha: Maktaba
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.

HUKU akikirejesha kikosi chake kambini visiwani Zanzibar kujiandaa na mechi ya 'Derby' ya Kariakoo dhidi ya Yanga, Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, amesema amegundua tatizo la kumalizia (ushambuliaji) ni janga la nchini kulingana na alivyoona timu nyingi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba imerejea Zanzibar kuweka kambi kwa mechi hiyo ya Jumamosi itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam saa 11:00 jioni, hiyo ikiwa ni mara ya pili msimu huu baada ya awali kujichimbia visiwani humo wakati wakijiandaa na mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Akizungumza na Nipashe jana, Benchikha alisema kazi kubwa ni kuhakikisha anaendelea kuwapa mbinu wachezaji wake kuelekea mechi zilizosalia ikiwamo hiyo ya Kariakoo Derby dhidi ya Yanga.

Benchikha alisema shida kubwa ya timu yake ni eneo la umaliziaji na kwamba hilo halipo kwenye timu yake pekee bali ni sehemu kubwa ya timu za Ligi ya Tanzania, lakini anahitaji kuendelea kujipanga kuhakikisha washambuliaji wake wanakuwa makini kwenye nafasi wanazotengeneza.

Alisema anaimani kubwa kutakuwa na mabadiliko katika eneo hilo kutokana na mbinu anazowapa katika mazoezi ikiwamo suala la kuwa makini kutumia nafasi hizo na kuweza kufunga.

“Hii tatizo si kwetu bali ni asilimia kubwa ya timu za ligi, lakini naangalia zaidi timu yangu, kuna nafasi nyingi tunazotengeneza tunashindwa kufunga, tunakuwa makini na hili kwa sasa ni kukaa na wachezaji kuwaeleza kuwa watulivu katika eneo hilo,” alisema Benchikha.

Aliongeza kuwa anaimani baada ya msimu huu kufikia tamati, atafanyia kazi jambo hilo kwa kuhakikisha wanafanikiwa kuimarisha safu ya ushambuliaji na kuweza kutumia nafasi zinazopatikana.

Kocha huyo alisema mechi zijazo watafanya vizuri kwa kutafuta ushindi kwa kila mchezo ikiwamo dhidi ya Yanga ili kuendelea kujiweka pazuri kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Wakati Benchikha akieleza hayo, imeelezwa kuwa kikao cha uongozi wa juu wa klabu hiyo kilichofanyika wiki iliyopita kikiongozwa na Mwekezaji na rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed 'Mo' Dewji, kimetoa mtihani kwa viongozi waliopo madarakani, kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri katika mechi zijazo hususan Jumamosi dhidi ya Yanga.

“Ni kweli kikao kilikuwa kina mambo mengi, huku baadhi ya viongozi wakipewa mtihani kuhakikisha tunashinda mechi zilizosalia tukianza na Yanga na ili kufikia malengo ikiwamo kutwaa ubingwa au kushika nafasi ya pili,” alisema mtoa habari huyo.

Kuhusu maboresho ya kikosi, alisema Benchikha amehakikishiwa kufanyiwa kazi mapendekezo yake ya msimu ujao ikiwamo suala la usajili kwa kuleta wachezaji wenye uwezo mkubwa hasa safu ya ushambuliaji.