Uhaba mbegu za alizeti chanzo utegemezi mafuta kutoka nje

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 10:23 AM Apr 30 2024
 Mafuta ya Alizeti.
Picha: Maktaba
Mafuta ya Alizeti.

CHAMA cha Wasindikaji wa Mafuta ya Alizeti Tanzania (TASUPA), kimesema kuwa nchi imekuwa tegemezi wa mafuta ya kula kutoka nje, hali inayosababisha serikali kutumia fedha nyingi kuingiza bidhaa hiyo nchini.

Aidha, kimetaja sababu nyingine inayosababisha utegemezi huo ni upatikanaji duni wa mbegu za alizeti zenye mafuta mengi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Ringo Iringo alibainisha hayo juzi jijini hapa wakati wa kongamano la wasindikaji wa mafuta ya kula ya alizeti nchini, wakulima, wadau wa sekta hiyo pamoja na wawakilishi toka serikalini.

Ringo alisema sababu nyingine ni kubanwa kwenye soko la mafuta ya kula kwa viwanda vya ndani kutokana na kuondolewa kwa ushuru wa forodha wa mafuta ya kula toka nje ya nchi.

“Hali hii inafanya mafuta hayo kutoka nje kuwa bei rahisi kuliko ya kwetu na kufifisha ufanisi kwenye soko la mafuta yetu. Ikumbukwe kuwa mafuta yetu bado yanazalishwa kwa gharama kubwa kuliko mafuta yazalishwayo sehemu nyingi duniani,” alisema.

Aliongeza:  “Kwa mfano mafuta ya alizeti yaliyosafishwa hapa Dodoma ni Sh.120,000 kwa dumu la lita 20 wakati mafuta yaliyosafishwa ya mawese toka nje ni Sh. 81,000 kwa dumu la lita 20 hapa Dodoma.

Aidha, alisema wazalishaji wa mafuta ya alizeti wanashindwa kuuza nje ya nchi kutokana na bei zao kuwa juu kupitia masoko mengi Afrika na duniani kutokana na gharama kubwa za uzalishaji nchini.

“Tunaishauri serikali irudishe ushuru wa forodha wa asilimia 25 kwa mafuta ghafi ya kula na asilimia 35 kwa mafuta yaliyosafishwa yatokayo nje ya nchi,” alisema Ringo.

Alisema madhara makubwa yaliyoletwa na uondoaji wa ushuru huo ni pamoja na wasindikaji wa mafuta ya kula watumiao mali ghafi za ndani kutokufanya vizuri kibiashara kwenye soko na kushindwa kununua alizeti zilizopo kwa wakulima.

“Baadhi ya wasindikaji wamefunga viwanda au kuviuza kabisa hii imesababisha wakulima kukosa soko la zao la alizeti na kuamua mwaka huu kuacha kulima zao hilo na kuhamia kwenye mbaazi na mahindi,” alisema Ringo.

Alisema kutokana na hali hiyo mwaka huu kunauwezekano wa kuwa na upungufu mkubwa wa alizeti kwani wakulima wengi bado wana alizeti ya mwaka jana na wasindikaji wanashindwa kuisindika na kuingiza mafuta sokoni kutokana na uwepo wa mafuta ya bei rahisi kutoka nje.