Azizi Ki apiga 'hat trick' Yanga ikirejea kileleni

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:16 AM Feb 16 2025
Stephane Aziz Ki
Picha: Mtandao
Stephane Aziz Ki

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, jana walirejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuisambaratisha KMC mabao 6-1 kwenye uwanja wa KMC Complex, huku kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki, akifunga mabao matatu, 'hat-trick.'

Hiyo  'hat-trick' ya pili kwenye Ligi Kuu msimu huu, baada ya ile iliyowekwa na straika wa timu hiyo, Prince Dube, Desemba 19 mwaka jana akifunga mabao yote matatu wakati Yanga ilipoishindilia Mashujaa FC mabao 3-2 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Dube, jana alihusika na mabao manne kati ya sita yaliyopatikana, akitoa pasi tatu za mwisho za mabao yeye mwenyewe akipachika bao moja.

Beki wa kulia wa Yanga, Israel Mwenda, jana alifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na timu hiyo kipindi cha dirisha dogo la usajili, akitokea Singida Black Stars.

Ushindi huo wa jana unaifanya Yanga kurejea kileleni ikifikisha pointi 49, ikiiacha Simba na pointi zake 47 ambayo wiki hii haikuwa na mchezo wowote baada ya Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji ambayo wachezaji na viongozi wake walipata ajali ya gari mwanzoni mwa wiki iliyopita walitokea mkoani Lindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo.

Simba inanafasi yakuishusha tena Yanga kileleni kama itafanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Namungo utakaochezwa Jumatano ijayo mkoani Lindi.

Katika mchezo wa jana, dakika ya kwanza tu, Yanga ilikuwa imeshahamia langoni kwa KMC, ikifanya shambulizi la kwanza hatari, ambapo mpira uliopigwa na Khalid Aucho ulimkuta Mudathir Yahaya ambaye aliubetua mpira juu kumpiga kanzu kipa Ismail Bombona lakini mahesabu hayakwenda vizuri na mpira ukapaa juu ya lango.

Clement Mzize, dakika mbili baadaye alikuwa wingi ya kulia, kabla ya kupiga krosi iliyoelekea kwa Dube, lakini alichelewa na mabeki wa KMC wakafanikiwa kumbana kabla ya kipa Bombona kuuwahi.

Dakika ya tano ya mchezo, Aziz Ki, akiwa hatua sita tu kutoka kwenye lango la KMC, lakini kwa mshangao wa wengi akapiga mpia nje akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga bao la mapema.

Kipa Bombona, alifanya kazi nyingine ya ziada dakika ya nane baada ya kuokoa shuti kali la Mzize ambaye alibaki naye ana kwa ana baada ya mabeki wake kulambwa chenga.

Lilikuwa ni suala la muda tu, kwani dakika ya 10, Yanga iliandika bao la kwanza lililowekwa ndani ya nyavu na Dube.

Dube alipachika bao hilo kwa kichwa baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Maxi Nzengeli aliyeambaa na mpira kwenye wingi ya kushoto na kupiga krosi iliyounganishwa vyema na straika huyo ambaye amefikisha bao la nane kwenye orodha ya wafungaji akiwa sawa na Jean Ahoua na Leonel Ateba wote wa Simba, pamoja na Elvis Rupia wa Singida Black Stars.

Dube, aliangushwa ndani ya eneo la hatari, alipowalamba chenga mabeki wawili, Juma Shemvuni na Cosmas Okoyo, akiwa ameingia kwenye boksi, mwamuzi akaamuru mkwaju wa penalti.

Alikuwa ni Stephane Aziz Ki, aliyepachika mpira wavuni na kuhesabu bao la pili dakika ya 17.

Kuingia kwa mabao hayo kuliwafanya wachezaji wa Yanga kupunguza kasi ya kushambulia, lakini hiyo haikuwapa nafasi KMC kupandisha mbele mashambulizi kwani mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika, si tu hawakupiga shuti hata moja pia hawakufanikiwa hata kufika langoni mwa Yanga.

Kipindi cha pili, kilipoanza tu, Yanga ilipata bao la tatu lililofungwa tena na Aziz Ki akipokea  pasi kutoka kwa Dube, kabla ya Redemtus Mussa kuipatia KMC bao la kufutia machozi dakika ya 51 kwa shuti kali la mguu wa kushoto.

Dube aliangushwa tena kwenye boksi na Yanga kupata penalti, Aziz Ki akaukwamisha tena ndani ya wavu dakika ya 56 na kukamilisha 'hat-trick', ikiwa ni penalti ya tatu kufunga msimu huu, huku wakiwa amekosa mbili.

Maxi Nzengeli aliipatia Yanga bao la tano dakika ya 90 akipokea  kutoka kwa Dube huku Mwenda akipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la KMC kwa bao la sita, dakika za majeruhi baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Dube.

Kwa matokeo hayo KMC inabakiwa na pointi zake 22 kwenye nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu.