Aziz Ki atembea na mkataba wa Yanga

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 05:09 AM May 24 2024
news
Picha: Mtandaoni
Stephanie Aziz Ki

UONGOZI wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umesema unapambana kumshawishi mshambuliaji wake nyota, Stephanie Aziz Ki, ili asaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo, imefahamika.

Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema Yanga imefanya mazungumzo na nyota huyo lakini ameshindwa kukubali kusaini mkataba mpya kutokana na ofa mbalimbali alizonazo.

Chanzo hicho kimesema mchezaji huyo raia wa Burkina Faso anasubiri kufanya uamuzi mwingine baada ya kumalizika kwa msimu huu.

"Aziz Ki akiwa na wakala wake (mama yake), wamefanya mazungumzo vizuri na Yanga, lakini akawaambia wasubiri, atasaini siku nyingine, aliondoka na mkataba huo na kuahidi atausaini," kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza licha ya Rais wa Yanga, Hersi Said, kuongoza kikao cha mazungumzo, Aziz Ki, alionekana kushikilia uamuzi wake wa kuhitaji muda ili kukamilisha mchakato huo.

"Uongozi tayari umempa mkataba mpya, lakini bado hajausaini, Aziz Ki anaonekana kuvutiwa zaidi na ofa kutoka Afrika Kusini kwa sababu kuna timu inamtaka, kuna uwezekano akaondoka," kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza pia taarifa za nyota huyo kutakiwa na timu moja ya hapa nchini si kweli na hizo ni propaganda za usajili.

"Ofa ambayo Yanga wamempa si rahisi kwa Aziz Ki aiache, halafu asaini klabu ya hapa nchini, anachelewa kusaini kwa sababu ya ofa za nje ya nchi alizonazo, hakuna klabu ya ndani ambayo anaweza kwenda huko na kuacha ofa ya Yanga," kiliongeza.

Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, alikiri  mchezaji huyo hajasaini mkataba mpya kwa sababu bado wapo katika mazungumzo.

"Niwatoe hofu mashabiki na wanachama wa Yanga, wachezaji wote ambao Yanga bado inawahitaji tutabaki nao msimu ujao, na hata kama kuna mchezaji ambaye tunamhitaji na akataka kuondoka hakuna timu ya hapa ndani inaweza kumchukua, labda ataenda nje ya nchi," alisema Kamwe.

Alitamba mwakani wanahitaji pia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Tunataka msimu ujao kuandaa tena gwaride la ubingwa, ili tufanye hivyo lazima tuendelee kuwa na kikosi bora, Yanga itabaki na kikosi imara na bora zaidi msimu ujao," Kamwe aliongeza.