Azik Ki, Mzize rasmi sokoni

By Somoe Ng'itu ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:00 AM Jan 30 2025
Clement Mzize
Picha: Mtandao
Clement Mzize

HATIMA ya wachezaji wawili wa Yanga, Stephanie Aziz Ki na Clement Mzize, ambao wanatakiwa na Wydad AC ya Morocco itajulikana ifikapo Julai Mosi, mwaka huu, imefahamika.

Taarifa za ndani kutoka Yanga, zinasema mabingwa hao watetezi wameiambia Wydad itakuwa tayari kufanya mazungumzo ya kuwauza wachezaji hao muda huo ukifika na si wakati huu.

Chanzo chetu kilisema uamuzi huo umetokana na Yanga kuwaeleza Waarabu hao inahitaji zaidi mchango wa nyota hao wawili kwa ajili ya vita ya kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA, ambalo wanayashikilia.

"Wachezaji wote wawili ni muhimu katika kufikia mafanikio ya klabu yetu, hatuwezi kukubali kuwauza kwa sasa, tutakuwa tayari kufanya mazungumzo ya kuwauza kuanzia Julai Mosi, 2025, kama Wydad mtakuwa bado mnahitaji huduma yao," ilisema sehemu ya barua ya Yanga kwenda kwa Waarabu hao.

Mbali na Wydad, pia klabu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini pia zimeonyesha nia ya kuwahitaji nyota hao ili kuimarisha vikosi vyao.

Wakati huo huo, Yanga inaendelea na maandalizi kwa ajili ya kujiandaa kuwakaribisha Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, aliliambia gazeti hili wameshafunga 'mafaili' kuhusiana na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa hawataki kupoteza mchezo wao wa keshokutwa.

Kamwe alisema Yanga inataka kurejea kwa 'kishindo' katika Ligi Kuu, mahali ambapo hawana mpinzani ingawa baadhi ya mechi  huwa ngumu na yenye ushindani.

"Tunakwenda kucheza mechi muhimu, mechi yetu ya kwanza baada ya kutoka katika michezo ya kimataifa, tumekuwa tukiwaambia wanachama na mashabiki wetu tumetoka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, tumeumia sana, lakini tutaumia zaidi kama tutakosa kutwaa ubingwa wa Ligi KuuTanzania Bara.

Tunataka tuendeleze rekodi yetu ya kushinda mechi zetu za Ligi Kuu kwa asilimia 100, tangu ujio wa Ramovic (Sead), tumeshinda kwa idadi kubwa ya mabao, hicho ndicho kitakwenda kuwakuta Kagera Sugar," alisema Kamwe.

Yanga ilitolewa katika michuano inayosimamiwa na Shirikisko la Soka Afrika (CAF), baada ya kukubali kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya MC Alger na kumaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi A lililoongozwa na Al Hilal ya Sudan.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amewaonya wachezaji wake kutofikiria chochote juu ya kutinga robo fainali ya Kombe la FA baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Kilimanjaro Wonders, na kuimarisha mipango yao kwa lengo la kusaka pointi tatu ikiwafuata Tabora United.

Fadlu amewaambia pia wachezaji wake 'wasivimbe vifua' na kujiamini baada ya kuifunga CS Constantine ya Algeria mabao 2-0 na kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuamini wanaweza kuifunga Tabora United kirahisi.

"Nimezungumza na vijana wangu  tunakwenda kuianza duru ya pili ya Ligi Kuu, ili kuwa mabingwa tunawajibika kushinda kila mchezo ambao upo mbele yetu, tunapaswa kushinda mchezo dhidi ya Tabora pamoja na ugumu wake, kwa maana Tabora hii siyo ile tuliyoifunga katika mzunguko wa kwanza," alisema kocha huyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi chao kinaendelea vyema na maandalizi, huku kukiwa na habari njema ya kuhusiana na mchezaji wao, Awesu Awesu.

Aliongeza kikosi chao kitaondoka jijini kuelekea mkoani Tabora keshokutwa na wanafahamu mchezo huo wa Jumapili utakuwa mgumu kutokana na ubora wa sasa wa Tabora United, lakini wana imani wataibuka na ushindi.

"Kwanza lazima tukiri Tabora United ni timu nzuri na imeimarika sana ingawa  ilianza msimu vibaya, timu hii imepata kujiamini baada ya kuzifunga timu kubwa ikiwamo Yanga (mabao 3-1), na baadaye Azam (mabao 2-1) ambazo ni timu kubwa, ndiyo maana inaamini pia inaweza kufanikiwa kutufunga na sisi.

Tunawaambia kitu kimoja, ni kweli imezishinda timu ambazo zinakaribiana na sisi, lakini sisi siyo wao," alitamba Ahmed.