STRAIKA wa Simba raia wa Cameroon, Leonel Ateba, anaongoza kwa kufunga mabao ya penalti kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea, huku kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, akiongoza kwa kukosa.
Penalti aliyofunga juzi kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora dhidi ya Tabora United, akiiongoza Simba kushinda mabao 3-0, imemfanya straika huyo aliyesajiliwa mwanzo mwa msimu huu akitokea USMA Alger ya Algeria, afikishe mabao manne aliyoyafunga kwa njia hiyo.
Kwa mujibu wa Kitengo cha Takwimu cha Dawati la Michezo, Nipashe (KTDMN), straika huyo, amewapiku viungo washambuliaji wa Simba, Jean Ahoua na Feisal Salum wa Azam, ambao wote wamefunga penalti tatu kila mmoja. Ateba akiwa amefunga penalti zote alizopewa kupiga na timu yake.
Alianza kukwamisha penalti zake wavuni, Oktoba 4, mwaka jana, wakati Simba ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union, mechi ikichezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, baadaye aliweka nyingine, Novemba 22, mwaka jana, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Simba ikishinda bao 1-0, Desemba 18, mwaka jana, alifunga ya tatu, katika mchezo kati ya timu yake na KenGold, Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam, kabla ya kufanya hivyo tena juzi.
Kwa mujibu wa KTDMN, inaonesha kuwa mchezaji anayeongoza kwa kukosa penalti nyingi mpaka sasa ni Aziz Ki, ambaye ameikosesha timu yake ya Yanga mabao mara mbili kwenye mechi tofauti.
Aliingia kwenye rekodi hiyo, Jumamosi iliyopita, alipokosa mkwaju huo dhidi ya Kagera Sugar, licha ya timu yake kupata ushindi wa mabao 4-0, mechi ikichezwa KMC Complex.
Raia huyo wa Burkina Faso, alikosa penalti nyingine, Novemba 7, mwaka jana, katika mchezo kati ya Yanga na Tabora United, uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, akichangia timu yake kupoteza mchezo huo kwa mabao 3-1.
Hata hivyo, Aziz Ki katika penalti tatu alizopiga, amepata moja, ambayo aliifunga, Oktoba 3, mwaka jana, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, wakati timu hiyo ilipochezwa dhidi ya Pamba Jiji na kushinda mabao 4-0.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED