ILI kuhakikisha Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), inafanya vizuri katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), maandalizi yake yawe ni 'jambo' la kitaifa na si kuacha jukumu hilo kwa Serikali na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeelezwa.
Katika fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Desemba 21, mwaka huu hadi Januari 18, mwakani nchini Morocco, Taifa Stars imepangwa Kundi C pamoja na Uganda (Cranes),Tunisia na Nigeria.
Stars itatupa karata yake ya kwanza Desemba 23, mwaka huu kwa kuivaa Nigeria halafu Desemba 27 itakutana na 'majirani' zake Uganda na itamaliza mechi za hatua ya makundi Desemba 30 kwa kupambana na Tunisia kwenye Uwanja wa Prince Moulay ulioko jijini, Rabat.
Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' amesema ili kuweka rekodi ya kufanya vyema katika fainali hizo, maandalizi ya timu hiyo yanapaswa kuwa ni jukumu la kitaifa.
Morocco kipindi cha miezi 11 iliyobakia kabla ya kufanyika kwa fainali hizo, matokeo chanya yanaweza kupatikana kama tutaongeza ushirikiano kuanzia hatua ya kwanza.
"Hili jambo si la mwalimu au benchi la ufundi, ni suala la kitaifa hasa pale katika uwezeshwaji wa kutekeleza mipango ya mwalimu, sisi kama benchi la ufundi tutakuja na programu yetu na naamini ikifuatwa vyema tutafanya vizuri kwenye fainali hizi," alisema Morocco.
Kocha huyo alisema TFF inahitaji msaada ili kukamilisha programu za kiufundi za timu hiyo ambayo haijawahi kuvuka hatua ya makundi.
Aliongeza kuwafahamu mapema wapinzani wao ni jambo zuri kwa sababu watapata muda mzuri wa kuwafuatilia na kujiandaa kuwakabili.
"Mimi naamini tumepiga hatua kwenye makundi katika kutafuta nafasi ya kushiriki, tumefanya vizuri lakini haitoshi, tunahitaji kupambana zaidi na kuendeleza pale tulipofikia," alisema kocha huyo mwenye asili ya Zanzibar.
Aliongeza katika fainali hizo hakuna timu nyepesi, kila timu iliyofuzu inaweza ikawa tishio, lakini hakuna nchi wanayoihofia.
"'Of course' timu zote ambazo zimefuzu ni tishio, kufika hatua ya fainali za AFCON si jambo la rahisi, la msingi ni kuhakikisha tunajipanga vizuri ili tuwe bora zaidi," Morocco aliongeza.
Kabla ya kushiriki fainali hizo za AFCON, Taifa Stars imekata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zitakazofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30, mwaka huu.
Tanzania, Kenya na Uganda ndio wenyeji wa fainali hizo za CHAN, ambazo awali zilitarajiwa kufanyika kuanzia mapema Februari, mwaka huu.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), imezipa nchi hizo tatu wenyeji wa michuano ya CHAN ili kuwapa uzoefu kuelekea Fainali za AFCON za mwaka 2027 ambazo zitaandaliwa na mataifa hayo matatu ya Afrika Mashariki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED