Wadau wapongeza hatua za serikali kupambana na ulaghai bei ya sukari

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 04:13 PM Jun 15 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Picha: Nipashe Digital/ Mtandao
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

KATIKA kipindi cha hivi karibuni, sekta ya sukari nchini imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi, hususan suala la bei za sukari kupanda kiholela.

Baadhi ya viwanda vya sukari viliongeza bei ya sukari na kukataa kushusha licha ya kupata msaada wote kutoka kwa serikali ili kuongeza uzalishaji.

Hali hii ilifikia kilele wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo bei ya sukari ilipanda kutoka TZS 2,500 kwa kilo moja hadi TZS 4,000 na hadi 6000 maeneo mengine kwa kilo moja na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
 
Serikali iliamua kuchukua hatua kali ili kudhibiti hali hiyo kwa kutoa vibali vya uagizaji wa sukari kwa wafanyabiashara wengine sokoni.

Hatua hii ilileta matokeo chanya kwani bei za sukari zilianza kushuka kutoka TZS 4,000 kwa kilo moja hadi TZS 2,800 kwa kilo moja.
Hata hivyo, serikali iliona haja ya kuchukua hatua zaidi kwa kuandaa sheria bungeni za kuvunja ukiritimba wa viwanda vya sukari.

Kwa manufaa ya wamiliki matajiri watano wa viwanda vya sukari, serikali haiwezi kushikilia mateka watu wake milioni 65 na wakaendelea kuumia na bei ya sukari kwa manufaa ya wachache.

Kwa lengo la kushinikiza serikali kubatilisha mabadiliko hayo, wamiliki wa viwanda hivyo walirejea katika vitendo vyao vya kifisadi kwa kuhonga baadhi ya wanasiasa wapige kelele dhidi ya hatua hizi nzuri za serikali.
 
Ni nini kibaya ikiwa kampuni ndogo au kubwa ziliruhusiwa kuagiza na kuuza sukari sokoni ili kushusha bei je ni kampuni kubwa pekee ndizo zinazostahili fursa ya kuagiza na kuuza sukari?

Swali la kujiuliza, je baadhi ya watu wanataka serikali isichukue hatua yoyote huku makundi ya kifisadi yakiendelea kuwanyonya wananchi wake?

Ni dhahiri kuwa tatizo hili lingeachwa bila kudhibitiwa, gharama kwa uchumi ingekuwa kubwa sana.

Mfumuko wa bei ya sukari ungeathiri sekta mbalimbali za uchumi na ingesababisha kuongeza gharama za maisha kwa wananchi na kupunguza uwezo wa kununua bidhaa nyingine muhimu.

Hii ingeweza kusababisha madhara makubwa kwa ustawi wa kiuchumi wa taifa.

Ni wakati wa kusema hapana kwa hujuma na kulinda maslahi ya wananchi na kwa kuwa serikali ipo kwa ajili ya wananchi na iendele kuhakikisha haki inatendeka kwa wote.

Idd Salum mkazi wa Tandika anasema serikali imefanya jambo jema kuhakikisha inaingilia kati suala la sukari na kuruhusu wafanyabiashara wengine waagize sukari ili kuondoa ukiritimba.

“Zikiachwa kampuni kubwa mbili tu kuagiza sukari tutakuwa tunarudi kule kule bidhaa hii itaadimika na bei itapanda kwa hiyo hatua ya serikali kuingilia kati na kuruhusu kampuni ndogo na kubwa kuagiza sukari ni jambo la neema sana kwa watanzania,” alisema

Mmoja wa wafanyabiashra wa sukari Tandika, haule Shangu alisema biashara ya sukari isiachwe kwa kundi dogo kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kutumia nafasi hiyo kuwaumiza wananchi.

Alisema biashara ya sukari inafedha nyingi kwa hiyo serikali inapaswa kuiangalia kwa jicho la pekee kwani watu wachache wanataka kujimilikisha sekta hiyo ili waweze kucheza na bei ya sukari wanavyotaka.

“Kwanza napongeza hatua ambazo serikali ilichukua baada ya kubaini kuwa watu wachache wanaweza kucheza na bei ya sukari na kuamua kuruhusu kampuni zingine kuagiza sukari naomba mwendo uwe huo huo kampuni nyingine ziruhusiwe ili watu wachache wasiwe na uwezo wa kucheza na bei ya sukari,” alisema

Alisema ameshangazwa na kauli ya Mbunge wa Kisesa CCM kupinga kampuni zingine kupewa vibali vya kuagiza sukari kwani anataka kuendeleza ukiritimba ambao unaweza kupaisha bei ya sukari.

“Binafsi nampongeza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa namna alivyoshughulikia suala la sukari na kuamua kutoa vibali kwa kampuni zingine kuagiza sukari ili kupunguza uhaba wa sukari na kuhakikisha bei ya sukari haishuki,” alisema