Tume Madini na undani wa alichonadi Rais kununuliwa mashine mpya, Pato Taifa zaidi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:23 AM Nov 08 2024
•	Rais Samia Suluhu Hassan akipata maelezo alipotembelea soko la madini mkoani Geita, hivi karibuni.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
• Rais Samia Suluhu Hassan akipata maelezo alipotembelea soko la madini mkoani Geita, hivi karibuni.

NI wiki mbili na nusu zimepita, tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aatamke kuhusu uwekezaji wa kisasa katika uchimbaji madini, kwa kuletwa mitambo ya kisasa itakayoiboresha izalishe zaidi.

Hapo akasisitiza matumizi ya madini kubaki sura chanda na pete kisera na miongozo ya nchi, akinena: “Mitambo hii ikifika nchini itagawanywa pote. Ila nimemtaka Waziri (Anthony Mavunde - Madini), atenge mitambo miwili kwa ajili ya vijana na mmoja wanawake.”

Kauli ya Rais Dk. Samia, ni mwendelezo wa dhamira ya serikali yake kusukuma Sekta ya Madini nchini inaendelea kuongeza mchango ukuaji wake kiuchumi, kuchangia asilimia 10 au zaidi ya Pato la Taifa ifikapo mwakani. 

Hadi sasa inaelezwa mitambo mitano imewasili nchini na 10 iko njiani kurahisishia wachimbaji wadogo kupata taarifa za uchimbaji na kuwanusuru na hasara.

Inaelezwa, sehemu ya manufaa yake inawanusuru wadau husika kulanguliwa na hadi sasa, takwimu kitaifa zinarejea kipindi cha miaka mitatu na nusu ya uongozi wa Rais Dk. Samia, kumekuwapo maboresho ya ukuaji sekta ya madini nchini. 

Hiyo inatajwa kuongezeka kutoka asilimia 9.4 ya uchumi wa nchi mwaka 2021 hadi asilimia 11.3 za mwaka jana.

TUME YA MADINI

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, anafafanua ni matokeo ya maboresho ya sheria husika, kanuni na miundombinu husika, ikiwamo umeme migodini katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Samia.

Anasema, kati ya mwaka 2021 hadi 2023, kampuni hizo zilizalisha ajira 19,356, kati yake 18,853 ni za Watanzania, sawa na asilimia 97.40, huku wageni wako 503 sawa na asilimia 2.60 ya ajira hizo mpya.

Lwamo anasema, hilo linaendana na kuwapo bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 3,780,161,183.28 zilizouzwa na kusambazwa kwenye migodi mbalimbali nchini.

Katika orodha yake, kampuni za Watanzania ziliuza bidhaa za thamani ya Dola za Marekani 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya mauzo tajwa na na huduma zilizotolewa migodini.

MAKUSANYO JUU

Mhandisi Lwamo anasema maboresho ya sheria, kanuni na miundombinu ikiwamo ya umeme migodini ndani ya miaka mitatu ya mikakati na uongozi wa Rais Dk. Samia kupitia Tume ya Madini, makusanyo ya maduhuli ya serikali migodini yamepanda kutoka shilingi bilioni 624.61 za Mwaka wa Fedha 2021/22 hadi shilingi bilioni 753.82 za mwaka uliopita, 2023/24.

Hapo anafafanua kwamba makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 kwa miaka mitatu iliyopita.

“Mathalan, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 tulipewa lengo la kukusanya shilingi trilioni moja. Hadi kufikia Oktoba 21 mwaka huu, Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 312.75 sawa na asilimia   31.28 ya   lengo la mwaka,” anasema Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.

Lwamo anawaambia wahariri wa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam kwamba, Pato la Taifa mwaka 2021 kwa madini iliingiza asilimia 7.2, huku mwaka jana ikapanda kufika asilimia tisa, kutokana na kuimarika usimamizi wa shughuli zake nchini. 

MWELEKEO KISEKTA

Lwamo anasema, mwelekeo wa sekta kuchangia Pato la Taifa inadhamiria kuzidi asilimia 10 mwaka 2025, kama inavyofafanuliwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya  mwaka 2020 na Tume ya Madini wa Mwaka 2024/25, hadi 2025/26.

Anasema, tume hiyo ina mikakati endelevu inayoimarisha usimamizi na udhibiti wa maeneo ya uzalishaji madini, ujenzi na madini ya viwandani.

Hilo analitaja linaongezewa na Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMA), vitendea kazi na kushirikisha mamlaka nyinginezo za serikali zinazosimamia rasilimali hizo, ili kuongeza makusanyo na rasilimali yanayotokana na madini, pia ujenzi na mifumo na viwanda vya madini.

Anataja ushirikiano wa vyombo vya kiserikali; halmashauri zilizopo, Polisi, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) zimechangia kupigwa hatua hizo.

Lwamo anaataja mkakati mwingine ni kudhibiti biashara haramu za madini, hususan utoroshaji, serikali ikihamasisha utumiaji masoko na vituo vya madini nchini.

Pia anataja kuimarishwa vituo vya ukaguzi mipakani, bandarini na viwanja vya ndege, ili kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi na mapato.

Hilo linaendana na maboresho na usimamizi wa mfumo wa utoaji leseni za madini, kupunguza migogoro itokanayo na mwingiliano wa maombi ya leseni, muda wa utoaji huduma na kuongeza idadi ya leseni kila mwaka, wakihamasisha uwekezaji zaidi.

Lwamo pia anataja kuimarishwa ukaguzi wa uchimbaji migodini, lengo ni kuwa na uchimbaji endelevu ulio salama, ikiwamo kiafya na mazingira, ikiongezwa mapato, kuimarisha uchimbaji endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Lwamo, anasema kwa kuimarisha Ofisi za Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMO) na maabara katika maeneo ya uzalishaji nchini,  kutasogeza huduma karibu na wadau,  hivyo kuchochea uwekezaji utakaowezesha serikali kuongeza mapato yatokanayo na madini.

Mikakati mingine inajumuisha kuimarishwa utafiti wa kutambua vyanzo vipya vya mapato ya madini na kuiwezesha tume kuongeza wigo wa makusanyo yake,  ikiimarisha uwekezaji kwa wachimbaji, ajira zao na sekta endelevu.

• Wachmbaji wadogo wakiwa kazini, wakitumia stadi za asili.

MAUZO YANAPAA

Lwamo anasema kupitia Wizara ya Madini, tume hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini, imeendelea kusimamia utendaji kazi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi. 

“Katika Mwaka wa Fedha 2023/24 mauzo ya madini katika masoko na vituo vya ununuzi wa madini yalikuwa Shilingi bilioni 2,592.02 na mapato yaliyopatikana kutokana na mauzo hayo ni kiasi cha shilingi bilioni 180.13 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2021/22 ambapo ilikuwa shilingi bilioni 2,361.80.

 “Mapato ya Serikali yaliyopatikana ni shilingi bilioni 164.09, yalihusisha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini,” anasema Lwamo.

WATANZANIA KUNUFAIKA

Lwamo anasema tume yake inahakikisha wananchi wananufaika, ikiendelea kusimamia na kuwasilisha mipango ya ushirikishwaji kisekta kutoka kwa wamiliki, waombaji leseni za madini na watoa huduma, kwa mujibu wa sheria inavyowaelekeza. 

Anarejea kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023, wamewasilisha mipango 1,050 ya ushirikishwaji wananchi katika sekta hiyo na 1,036 ilikidhi vigezo, 14 pekee haikukidhi na kwa marekebisho.

 Kwa mujibu wa Lwamo, tume katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023, kampuni za madini zilizalisha ajira 19,356, kati yake, 18,853 ni Watanzania  sawa na asilimia 97.40 na 503 wageni asilimia 2.60 ya ajira hizo zilizozalishwa.

Anasema bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa kwenye migodi mbalimbali nchini.

Kati yake kampuni za nchini ziliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya mauzo yote na huduma zilizotolewa migodini.

Hiyo ikaendana na kutolewa 34,348 sawa na asilimia 92.04 zilizopangwa kutolewa, akizitaja leseni hizo ni za uchimbaji mkubwa, kati, mdogo, biashara ya madini na uchenjuaji wake.

KUDHIBITI UTOROSHAJI 

Lwamo anasema kuanzishwa masoko ya madini nchini, kumedhibiti utoroshaji  madini na kuongeza uwazi katika sekta hiyo.

 Anasema hadi sasa kuna masoko 44 na vituo 106 vidogo vya ununuzi wa madini vimeanzishwa nchini, pia kudhibiti bei zake kwa kutolewa bei elekezi shindani, ikilinganishwa na soko la dunia. 

“Masoko haya yamesaidia kuweka mifumo ya kufuatilia na kusimamia biashara ya madini, ikiwamo teknolojia za kidijitali kusaidia kurekodi taarifa za madini kutoka kwa wachimbaji hadi kwa wanunuzi,” anasema Lwamo. 

“Masoko haya yamesaidia kuongeza mapato ya serikali kupitia tozo na ada  zinazotozwa kwenye masoko haya,” anafafanua.

MINADA YARUDISHWA

Akizungumzia minada, Lwamo anasema serikali kupitia tume inatarajia kurejesha minada ya ndani ya madini ya vito katika maeneo ya uzalishaji.

 Maeneo hayo ni pamoja na Mirerani, Mahenge, Tunduru, Dar es Salaam, Arusha na Tanga na ya kimataifa katika mji wa Bangkok na Jaipur nchini India.

 “Uendeshaji wa minada hii ni fursa muhimu ya kutangaza madini ya vito vinavyozalishwa nchini hususan kwenye masoko ya kimataifa,” anasema.