UKAME unaotokana na kukata miti ovyo kupata nishati, malisho na makazi yanayogeuza ardhi kuwa jangwa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi yanawalazimisha wafugaji kuhama hama kusaka malisho huku wakisababisha migogoro kwa wakulima.
Ni jambo lililotesa wengi lakini sasa ni amani kufuatia ujio wa kampeni ya ‘Tutunzane Mvomero– Mfugaji Mtunze Mkulima na Mkulima Mtunze Mfugaji ili Kulinda Mazingira Yetu.”
Ni mradi unaoasisiwa na viongozi na kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli, ukizinduliwa mwezi uliopita na Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Morogoro.
Kampeni hii ni darasa muhimu katika jitihada za kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani Mvomero kupitia kuwapa elimu makundi hayo mawili ili kuondoa uadui dhidi yao kwani kila mmoja anamtegemea mwenzie katika shughuli zao.
Mvomero ni sehemu ndogo ya Tanzania hii kubwa yapo maeneo mengi yenye migogoro ya ardhi huku yakichagizwa na ugomvi baina ya wakulima na wafugaji, elimu iliyo ndani ya kampeni hiyo ya tutunzane inapaswa kusambaa na kuvuka mipaka ikienea nchi nzima.
Kuwaelimisha na kuwahamasisha wakulima kutaihakikishia nchi amani na kumaliza ugomvi kati ya wakulima na wafugaji na kuchangia maendeleo kwani sekta mbili hizo za kilimo na ufugaji ni muhimu katika maendeleo kwa vile ndiko kinapotoka chakula na malighafi viwandani.
Makundi haya mawili yanategemeana. Kwa mfano, anayefuga hawezi kuishi kwa kula nyama na maziwa pekee, vilevile mkulima hawezi kuishi kwa kutegemea mazao ya shambani kwake tu, kwani kuna wakati anahitaji nyama, maziwa na mifugo kutoka kwa wengine na huo ndiyo mlo kamili kama wanavyoshauri wataalamu wa lishe.
Lakini hata katika maisha ya kawaida, wakulima na wafugaji wanapaswa kuishi kwa amani kwa miaka mingi, makundi haya mawili wamekuwa ni ndugu wanaoishi pamoja na kufanya mambo mengi kwa ushirikiano wala hakuna aliye bora zaidi ya mwenzake kama kampeni inavyosema kutunzana kwa sababu wanahitajiana na wanategemeana pia.
Kutokana na ukweli kuwa, ardhi ni nyenzo muhimu ya kimaendeleo, ni lazima kuwe na matumizi endelevu ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara inayohatarisha amani na ustawi wa maendeleo kwa kuhakikisha wakulima wanakuwa na maeneo yao kwa ajili ya kilimo, hali kadhalika wafugaji nao ili kila kundi liepuke kuingia katika eneo la mwenzake.
Kampeni ya tutunzane imelenga kuhamasisha wakulima na wafugaji kurasimisha ardhi zao kwa gharama nafuu ili kupata hati miliki za mashamba yao, wapewe mbegu za malisho na mazao mengine ili kupanda.
Katika ardhi zao zilizopimwa, wafugaji watakuwa na uwezo wa kupanda malisho mazuri kwa ajili ya chakula cha mifugo yao na kuepukana na kadhia ya kwenda kulisha wanyama kwenye mashamba ya wakulima ambapo inaleta ugomvi, uhasama na kuwatia hasara wakulima kwa kupoteza mazao yao na hivyo kuendelea kuishi maisha duni.
Kampeni inasisitiza ufugaji wa kisasa, kuondokana na migogoro kati yao na wakulima na watumiaji wengine wa ardhi. “Kampeni hii ni muhimu kwa sababu inataleta amani, ongezeko la malisho, tija na wafugaji waweze kukopesheka,” anasema Rais Samia katika uzinduzi.
Aidha, kampeni hii pia inachochea maendeleo kwa kuweka mkazo wa kuwa na eneo dogo lakini lenye uzalishaji mwingi unaotokana na teknolojia kwa kufuata mbinu za kisasa za kiuzalishaji kwani utaalamu unaonesha kuwa, ili kuwe na tija kwenye kilimo, hakuna haja ya kulima eneo kubwa au ili kuzalisha nyama na maziwa mengi si lazima kuwa na mamia ya mifugo.
Changamoto ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia sasa hayana budi kukabiliwa kupitia mbinu za kisasa za kiuzalishaji:
“Lazima tuwe wabunifu wa kuja na mbinu zitakazofanya ardhi tuliyonayo izalishe zaidi. Kama ni mkulima avune kwa wingi kwa kipande cha ardhi alichonacho vivyo hivyo kwa mfugaji”, anasema Rais Samia.
R4 NDIYO TUTUNZANE
Rais Samia anazungumzia falsafa yake ya R4 ya kwanza ‘reconciliation’ au maridhiano, ‘resilience’ au ustahimilivu, ‘reform’ ndiyo mabadiliko na ‘rebuilding’ au kujenga upya.
Kutokana na uwapo wa uhasama kati ya wakulima na wafugaji, kumekuwa na haja ya kuwa na maridhiano baina yao, kwa kuweka mikakati madhubuti ikiwamo kampeni na elimu ya tutunzane ili kuleta amani.
Kampeni inasisitiza umuhimu wa kuleta mabadiliko kwa kulima na kufuga kisasa ili kuondoa migogoro na kuchochea maendeleo.
Vilevile, kampeni hiyo inalenga kujenga upya mahusiano mazuri baina ya wakulima na wafugaji kwani makundi haya yanahitajiana katika maisha ya kila siku.
Kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, Rais Samia anawaita mbele wawakilishi wa wakulima na wafugaji akawapatanisha kwa kuwaambia washikane mikono kama ishara ya kumaliza tofauti zao na kuanza ukurasa mpya.
“Mlime, wanaolima na mfuge wanaofuga, na kwamba tunategemeana wote. Ninyi ndiyo mnaotupa sisi uhai, mnatupa vitowe, chakula, hakuna haja ya kugombana, kuuana, wote ninyi ni wanadamu” anasisitiza Rais Samia.
Hili ni darasa la kujifunza kuwa na amani na maelewano lisambae wilaya nyingine ili kujifunza kutoka Mvomero waasisi wa kampeni ya tutunzane, ili kupunguza wingi wa kampeni tutunzane iwe ya kitaifa kwani ina manufaa mengi na imegusa maeneo mengi ya kimaendeleo. Sekta za kilimo na ufugaji zinategemewa katika ukuzaji uchumi na kutoa ajira nyingi kwa wananchi, hivyo zisikie anachosema Rais zifanye kazi bila migogoro na zione matunda.
Mwandishi ni mwalimu wa Sekondari ya Mlali ya mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED