TAARIFA za habari kwenye televisheni, redio, mitandao ya kijamii zinaarifu kutekwa kwa mtoto wa miaka sita, Macaire, mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule moja Mbezi Dar es Salaam. Mashuhuda wanasema alinyakuliwa na mwanaume mmoja aliyeshiba, kujaa misuli na kukimbilia kwenye gari lililokuwa pembeni mwa barabara ya Bagamoyo, Dar es salaam, ambalo mlango wake ulikuwa wazi.
Wazazi wa mtoto wanapigiwa simu na watekaji wakitaka kiasi cha Sh. Milioni 15 ili wamuachie. Jeshi la Polisi linaingia kazini kumsaka au kuwasaka watekaji. Walichogundua ni kisa cha kushangaza, kusisimua ambacho utakipata utakaposoma kila aina ya nakala ya gazeti hili, ili kuupata mkasa mzima wa tukio.
***************************************
"Afande mimi naogopa kwa sababu watekaji wameniambia mambo mengi ambayo yamenitisha. Wameniambia hizi pesa ni za polisi nilizowapelekea, hawazitaki kwa sababu zina namba ambazo mnazinakili, hivyo mtawakamata hata kama wakifanikiwa kuzichukua. Wanataka ambazo ndugu tutachanga wenyewe. Na wameniambia kama nikiwaambia watamchinja mtoto wangu ni kuambia tu sehemu ambayo maiti yake wataitupa." Hata hivyo afande Chacha alimhakikishia kuwa Jeshi la Polisi litatumia nguvu, ujanja, weledi na raslimali zote walizonazo ili kumuokoa mtoto kutoka mikononi mwa watekaji.
Hilo lilimtia moyo na kuamua kumwambia kila kitu. Afande Chacha aliwatia moyo Macky pamoja na mzazi mwenzake Dora kuwa wasihuzunike, mtoto atapatikana.
"Kama yupo hai kama ulivyosema na wewe mwenyewe umemsikia kwenye simu, basi hao nia yao ni pesa tu. Safari hii hatutochukua pesa za polisi. Kwa sababu za polisi ni mpya sana. Tutachukua kwa mtu mmoja hivi, atatuazima, tena tutachukua zile zilizochakaa ili wasijue kama zetu halafu utawapelekea. Kwa mara ya kwanza hatutumia simu kuwasiliana kuhusu jambo hili, tumeitaka hapa. Tumeamua pia kutomwambia Mwalimu Mkuu kuhusu hili suala. Ni kwa sababu mara ya kwanza habari zilivuja zikafika kwa watekaji. Safari hii tumeamua kama Jeshi la Polisi siri ibaki kwa wazazi na sisi polisi ili tuone nini kitatokea. Siyo kama tunamtuhumu Mwalimu Kisanga, hapana, ila inawezekana kuna watu wa karibu anawafahamu anaongea nao, inaweza ikawa ndiyo watekaji, au wana uhusiano nao, maana utekaji umetokea kwenye shule yake." Afande Chaha aliwaambia wazazi hao jinsi walivyoamua kutovujisha siri.
"Na nyinyi msimwambie chochote kile kuhusu hili, na siyo huyo tu mwalimu, msizungumze chochote kwa ndugu zenu na majirani ili tuone jaribio la pili la kuwakamata watekaji kama litafanikiwa," alisema afande Chacha.
***************************************
Saa sita usiku akiwa na mkoba wake wa pesa kiasi cha Sh.Milioni 15 begani. Alikuwa ameteremka kwenye basi kwenye kituo cha Magomeni Mikumi. Hakukuwa na watu wengi sana, ingawa walikuwepo baadhi wachache walevi, wanaotoka kwenye starehe na wateja wa chips.
Alianza kuambaambaa upande wa kushoto wa barabara ya Kawawa kuelekea kwenye makutano ya barabara hiyo na Kigogo. Kila alipokuwa anavuta hatua mbele ndipo watu walipokuwa wanazidi kupungua na kujiona yupo peke yake.
Alifika kwenye mteremko ambao juu yake kulikuwa na daraja akashuka taratibu. Alikokuwa akielekea hakukuwa na taa nyingi. Na zilizokuwepo pembeni ya barabara zilikuwa hafifu. Ilikuwa ni hali ya kuogofya, lakini tayari alishaanza kuzoea mazingira kama hayo.
Ile hali aliyoiona siku ya kwanza pale kwenye mteremko wa Kinondoni Mkwajuni ulimomaza na kumfanya kitu woga ukae pembeni. Pia alikuwa hakuwa peke yake, bali maafande walikuwa nyuma yake wakimlinda kwa chochote ambacho kinaweza kumtokea.
Alipofika katikati ya mtereko alilikuta daraja ambalo linatenganisha Magomeni na Kigogo. Ramani ilionyesha hapo ndipo kulipokusudiwa. Haikuhitajika kupanda kilima kwenda kwenye mzunguko wa makutano ya barabara ya Kawawa na Kigogo. Alikata kushoto kutoka kwenye njia ya watembeayo kwa miguu aliyokuwa akiifuata.
Wadudu walikuwa wanarukaruka kutoka kwenye majani wengine wakimpiga machoni. Kulikuwa na maeneo yenye maji, hivyo kuna wadudu ambao walikuwa kama wanawaka taa na kuzima, maarufu kama vimulimuli.
Chura nao hawakuwa nyuma, waliendelea kulia na kuhanikiza, lakini kila alipokuwa akipiga hatua kwenda mbili sauti zao zilipungua. Alipofikisha hatua tatu tu kabla ya kufika simu iliita. Akashtuka. Alijua kabisa wanaopiga ni wale wake watekaji. Ni staili kama ile ile iliyotokea Kinondoni Mkwajuni.
"Ndugu yangu nadhani wewe hatuelewani. Kila siku nakwambia usiwaambie askari siku ya kuleta pesa... "Sijawaambia" Akaropoka Macky. Alisikia sauti inayomsemesha ikicheza kwa dhihaka. "Hivi unajua unachokiongea wewe? Tulikwambia sisi tuna mtandao mpana. Kwanza kabisa tulikwambia usiwaambie polisi, ukaja nao kule Mkwajuni. Tena na pesa zilikuwa za mtego. Tukakukanya. Lakini umeenda tena kukwambia. Walicjobadilisha safari hii ni kwamba hizo pesa wamezikusanya tu kutoka kwa watu mbalimbali. Wamekusanya pesa chakavu ili kutuzuga. Na tayari wapo nyuma yako, wanakulinda. Hawapo mbali kutoka hapo ulipo. Wanachotaka ni kwamba ukishatoka tu waje kutukamata. Isingekuwa tuna mtandao mpana tungekamatwa zamani sana. Nadhani hutaki urafiki na sisi. Tumekuvumilia sana, lakini naona unatufanyia masihara. Kwa taarifa yako, kesho saa kama hizi uje hapo hapo, utakuta maiti ya mtoto wako." "Hapana hapana ha..." Alikataa Macky kwa sauti. Awali alikuwa akizungumza tararibu kutokana na mazingira yenyewe aliyokuwepo. Suala la mtoto wake kuuawa lilimshtua na kuamua kuongea kwa sauti. Wakati akitaka kuomba msamaha, tayari simu ilikuwa imekatwa kitambo.
Alijua hatompigia tena leo na si kwenye namba hiyo tena. Hata yeye akijaribu kupokea haitopatikana tena kama kawaida yao.
**********************************
Si Macky na mzazi mwenzake Dora walioonekana kustushwa na hilo, bali hata Jeshi la Polisi. Mwalimu Kisanga ametengwa kwenye mpango wa pili wa kupeleka pesa kwa watekaji, kwa nini wamefahamu?
"Tena leo wameniambia niende pale pale nilipoenda jana nikachukue maiti ya mwanangu..." Alisema Macky huku akitokwa machozi.
Afande Chacha na wenzake walimbembeleza na kumhakikishia hawawezi kufanya hivyo, ilikuwa ni harira zao tu baada ya kukosa pesa.
Dora yeye aligaragara kwenye sakafu ya ofisini, ilibidi waitwe askari watatu wa kile waje kumwinua na kumpeleka ofisi nyingine kwa ajili ya kumbembeleza na kumliwaza.
"Mama mwanangu watamuua leo." Alilia na kuomboleza baada ya kusikia maneno kutoka kwa mzazi mwenzake.
"Unasikia Macky. Sisi tuna uzoefu katika kazi hii kwa miaka mingi. Tayari lengo la hawa watu siyo kuua, siyo viungo vya binadamu. Hawa wanachohitaji ni pesa. Yaani kuwepo hai kwa mtoto kwao wana matumaini makubwa ya pesa. Kifo cha mtoto wako ina maana biashara yote ya kupata pesa kwao itakuwa imekwisha. Hawawezi asilani kwa sababu bado wana nafasi ya kupata pesa kwani mtoto yupo mikononi mwao." Maneno hayo yalimfariji Macky. Aliona kuwa ni kweli kabisa watekaji bado watakuwa wanahitaji pesa kutoka kwake, hivyo hawatumdhuru mtoto kwa sababu wakifanya hivyo, hawatoipata tena.
"Sasa kwa nini wanajua? Kwa nini wanapata habari? Kwa nini kila tunachofanya wanajua? Yaani wale jamaa inaonekana kama hata kama tukifanya kikao hapa wanajua." Akaongea Macky kwa sauti ya msisitizo iliyowashtua maaskari wengine, wakatazamana.
(0716 350534)
Itaendelea Jumapili
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED