Ni mapinduzi ya utunzaji ardhi na misitu kipitia elimu kwa watumiaji

By Beatrice Philemon , Nipashe
Published at 08:54 AM Jan 16 2025
Ni mapinduzi ya utunzaji ardhi na misitu kipitia elimu kwa watumiaji.
Picha: Mtandao
Ni mapinduzi ya utunzaji ardhi na misitu kipitia elimu kwa watumiaji.

KUNA darasa la kurejesha thamani ya ardhi na misitu mkoani Tanga linaendelea, chini ya uratibu wa kiserikali, kupitia nguzo za Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA).

Alhamisi wiki iliyopita, ilikuwa na safu ya mada hii, ikiwa na dodoso la ziara yenye ushuhuda wa mwandishi katika wilaya za Kilindi, Handeni na Pangani, kuhusu mageuzi kwenye utunzaji ardhi na misitu. Fuatilia nyenzo elimu kwa jamii ilivyovusha malengo, hadi mapinduzi katika nafasi ya jinsia......

Hao wamekuja na mfumo unaowasaidia wananchi katika wilaya za Pangani, Handeni, Kilindi na Mkinga, kuvuna misitu kwa njia endelevu na rafiki wa mazingira.

Sasa wananchi wanaelimishwa matumizi bora ya ardhi na kutenga misitu ya hifadhi ya vijiji kwenye ardhi zao, ili kuboresha usimamizi endelevu wa misitu na uzalishaji endelevu wa nishati iitwayo tungamotaka, ikiwamo mkaa na mbao kwa njia endelevu. 

Elida Fundi, Ofisa Utawala Bora na Uragabishi kutoka Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), anaiambia Nipashe kwamba, uvunaji endelevu ni unaokidhi mahitaji ya sasa, bila kuathiri mahitaji ya kizazi kijacho.

“Ili kukidhi mahitaji ya sasa na kizazi kijacho, serikali ya kijiji inaruhusiwa kutenga asilimia 10 mpaka 20, kwenye eneo la msitu kama eneo la uvunaji mkaa endelevu na asilimia 80 inabaki kama eneo la uhifadhi,” anasema.

Pia, anaendelea: “Huyo sasa hatakiwi kufanya shughuli yoyote ya uvunaji mkaa, kilimo na shughuli nyingine, kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

KINACHOPATIKANA

Inatajwa hadi sasa, Suluhisho la Ujumuishaji Misitu na Nishati Endelevu ya Tungamotaka Tanzania (IFBEST), wananchi katika vijiji vya Lusane, Mnkonde, Gendagenda na Mseko ndami ya wilaya za Pangani, Kilindi na Handeni wametenga misitu ya hifadhi ya vijiji kwa uzalishaji mkaa endelevu.

Hiyo inatajwa kusaidia kuongezea kipato, kupunguza uharibifu misitu na usimamizi shirikishi, kutekeleza miradi ya maendeleo katika vijiji vyao.

Uamuzi wao wanavijiji, wametenga misitu ya hifadhi ya vijiji, baada ya kupata mafunzo ya uvunaji endelevu wa mazao ya misitu na uzalishaji mkaa endelevu, matumizi bora ya ardhi na usimamizi shirikishi wa misitu kutoka MJUMITA na TFCG.

Mafunzo yametolewa kwa wajumbe wa kamati za maliasili, viongozi wa vijiji, wafugaji nyuki, wenye misitu binafsi na wanaotaka kutetea misitu, pia wazalishaji mkaa endelevu.

Elida Fundi, ni Ofisa Utawala Bora na Uragabishi wa MJUMITA Ni mradi wa miaka mitatu unaofadhiliwa na fedha za kigeni, kupitia Wizara ya Fedha na hadi sasa unatekelezwa katika vijiji kadhaa.

Anaviorodhesha kuwa; Lusane, Mnkonde, Mswaki, Nghobore, Mkalamo, Gendagenda, Mmbogo, Mapanga na Mseko katika wilaya za Pangani, Kilindi na Handeni.

Lengo la mradi ni kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira kwa kuboresha usimamizi endelevu wa misitu na uzalishaji endelevu wa nishati ya tungamotaka.

Tukio mojawapo la upandaji miti wilayani Kilindi. PICHA:MTANDAO
KWANINI MAFUNZO? 

Waratibu mafunzo, MJUMITA kwa kushirikiana na TFCG, wanafafanua sababu mahsusi wa mafunzo hayo ya umma, yanaangukia kuwezesha wenyeji kujua haki zao, kusimamia na kujitetea wanufaike na rasilimali zao za misitu na mazao yake.

Eneo lingine, analitaja ni zao la mafunzo liwakweze kwa uelewa na utendaji, wakazi hao kugombea nafasi mbalimbali za kiuongozi na kutendaji.

Hapo inaorodheshwa mifano ya nafasi, kama vile kamati za maliasili, uongozi wa vijiji na masuala ya misitu, ukiwa na ajenda  ya kijinsia kuacha dhana ‘misitu ni kazi ya wanaume’ na kuleta tofauti.

Nipashe ikiwa katika ukaguzi wa kihabari eneo hili, ikashuhudia matokeo; wanawake wanashika nafasi kubwa kiungozi katika vijiji vyao kama vile Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji cha Mnkonde, wilayani Kilindi.

Vilevile, MJUMITA imezijengea uwezo asasi nyingine za kiraia za mkoani Tanga, kuweza kushawishi kuwapo mazingira wezeshi kisera, usimamizi misitu na uvunaji endelevu wa nishati tungamotaka.

Pia, wanamtandao wa MJUMITA wamejengewa uwezo wa kufanya ushawishi na kutetea usimamizi shirikishi wa misitu na uvunaji endelevu wa nishati tungamotaka kutoka kwenye misitu ya vijiji iliyohifadhiwa kisheria.

Manufaa mengine, ofisa Elida anayataja ni kuwapo uzalishaji endelevu wa nishati za kuni, mkaa, wakitumiwa wanasiasa na viongozi serikali, kutatua changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa usimamizi shirikishi wa misitu kwenye ardhi ya vijiji.

“Tumeamua kutoa mafunzo haya baada ya kugundua kuwa misitu mingi katika mkoa wa Tanga inazidi kutoweka, watu wanazidi kuvuna miti hii kiholela kwa uchomaji mkaa, mbao, shughuli za kilimo, uchimbaji madini, ujenzi wa makazi na shughuli nyingine za kibinadamu,” anasema.

MJUMITA kwa kushirikiana na TFCG zinataja kusaidia kuanzisha ‘mpango wa matumizi bora ya ardhi’ katika vijiji vya; Lusane, Mapanga na Gendagenda, hata kutatua migogoro kati ya vijiji iliyodumu kwa muda mrefu.

OFISA MISITU KILINDI

Peter Mtoro, ni Ofisa Usimamizi Shirikishi wa Misitu kutoka TFCG wilayani Kilindi, anasema kupitia mradi, wananchi wamefanikiwa kutenga hekta 13,537.9 za misitu.

Hizo zinajumuisha, misitu ya hifadhi ya vijiji kwa ajili ya usimamizi shirikishi wa misitu na kusaidia wananchi kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika vijiji vyao.

Anasema, kati ya hekta hizo, jumla ya hekta 2, 304 za misitu zimetengwa kwa ajili ya uzalishaji mkaa endelevu katika wilaya ya Kilindi, Handeni na Pangani.

“Jumla ya hekta 279.1 za misitu zimetengwa katika kiijiji cha Mapanga, hekta 270 zimetengwa katika kijiji cha Lusane, hekta 695 zimetengwa katika kijiji cha Mseko, hekta 800 zimetengwa katika kijiji cha Gendagenda, hekta 260 zimetengwa katika kijiji cha Mkalamo,” anasema.

Anasema Wilaya ya Kilindi itazalisha tani 185.9 za mkaa endelevu kwa mwaka, wilaya ya Pangani tani 133.2 na wilayani Handeni itazalisha tani 233.3 za mkaa endelevu kwa mwaka.

Pia katika kijiji cha Mseko TFCG imewawezesha wananchi kuelewa Mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu na sheria ndogo zake. Pia, wamewasaidia kuandaa mpango wa uvunaji.

“Tunashukuru Umoja wa Ulaya (European Union) kutoa fedha ambazo zimesaidia Shirika la TFCG na MJUMITA kusaidia vijiji kufanya matumizi bora ya ardhi, kutenga misitu ya hifadhi ya vijiji, kutenga maeneo kwa ajili ya makazi, mifugo, kilimo, huduma za kijamii, vyanzo vya maji na huduma nyingine, anasema.

UVUNAJI MKAA ENDELEVU 

Anasema tathmini iliyofanywa na TFCG katika msitu wa hifadhi ya kijiji cha Mseko, jumla ya vitalu 2,780 vimetengwa katika msitu wa hifadhi ya kijiji kwa ajili ya uvunaji mkaa endelevu.

Vitalu vitakuwa na uwezo wa kuzalisha magunia 2664 kwa mwaka na mapato yenye thamani ya shilingi 33,302,083 ikiwamo pia hewa ukaa.

Mbali na hilo, TFCG iliwezesha kijiji cha Mseko kufanya tathmini kujua misitu iliyopo katika kijiji chao inauwezo wa kuzalisha tani ngapi za mkaa endelevu.

Pia jumla ya wataalamu 32 kutoka halmashauri za wilaya na Tanzania Forest Services (TFS) walipewa mafunzo ili kusaidia jamii kuanzisha usimamizi shirikishi wa misitu.

OFISA UFUATILIAJI 

Ewald Emil, ni Ofisa Ufuatiliaji, Utafiti na Mawasiliano wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), anasema watekelezaji mradi katika vijiji husika, wameshauri kuwa vibali vyote vitakavyotolewa na halmashauri au serikali ya kijiji kwa ajili ya uvunaji endelevu wa mkaa, vitaje wavunaji weaankonda.

Anasema ni mapendekezo, baada ya kugundua vibali vinavyotolewa kusafisha mashamba, vimekuwa vikitumika kinyume na sheria.

Emil anasema, baadhi ya watu wamekuwa wakitimia vibali hivyo kuingia kwenye maeneo ya hifadhi ya misitu ya vijiji na kuchoma mkaa holela na kuchangia uharibifu misitu, huku kijiji kikikosa mapato yake.

Wameshauri utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa misitu na wananchi wapatiwe shughuli mbadala ili waache kutegemea zaidi misitu kwa ajili ya kujiongezea kipato.

Pia, elimu ya uhifadhi misitu imeshauriwa iendelee kwa jamii zinazozunguka misitu, kuongeza elimu ya mpango hisa kwa vikundi mbalimbali, ikiendana na usafiri, vitendea kazi kwa kamati ya maliasili na wilaya hasa maofisa misitu na mazingira.

Pia, kuna kufanya doria kwa watu wanaoingia kwenye hifadhi ya misitu kinyume na sheria kwa ajili ya uchomaji mkaa na kilimo.

Limo, pendekezo la wananchi wanaozunguka mradi wapewe miti wapande, TFCG na MJUMITA waendelee kutoa mafunzo kwa wamiliki wa mashamba makubwa ya misitu.

Pia, viongozi wapya katika maeneo ya mradi wantakuiwa wajengewe uwezo kuhusu mradi na uhifadhi wa misitu ya asili, kama ilivyo kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.

Hiyo inatajwa kusaidia kushughulikia migogoro iliyopo kati ya vijiji, wilaya na a na kushirikisha wadau wote katika utatatuzi wa migogoro hiyo.  

Mbali na hilo, uhamishaji wa mifugo, taratibu na sheria zote zizingatiwe, pia uvunaji endelevu ufanyike kwa watu wanaomiliki mashamba makubwa ya miti ili nao waweze kunufaika na mradi wa carbon.

KUTOKA KIJIJINI 

Mlezi wa MJUMITA, katika Kijiji cha Mkonde, Mwanaidi Gwalu, anaeleza: “Kupitia uhifadhi, wananchi wamejenga kisima cha maji kwa ajili ya wananchi kupitia uhifadhi wa misitu, wamepata mafunzo jinsi ya kuanzisha ‘Village Community Banks’ (VICOBA).

“Kutokana na mafunzo hayo, wameanzisha vikundi viwili vya VICOBA, kikundi cha Upendo na Chekanao na wameanzisha miradi ya aina mbalimbali ili kupunguza ukataji wa misitu.” 

Anafafanua, kabla ya kupata mafunzo, mwanzoni walikuwa wanafanya uchomaji holela wa mkaa katika msitu na kuleta madhara katika afya zao.

“Sasa hivi hawaendi kukata kuni na kuchoma mkaa ndani ya msitu, sasa hivi wanachukua mikopo kwenye VICOBA na wanafanya biashara zao,” anasema

MNUFAIKA MAFUNZO

Lucia Msongela, Katibu wa Kikundi cha Chekanao ni mufaika wa mafunzo yaliyotolewa na Shirika la MJUMITA na TFCG kupitia mradi wa IFBEST.

‘Kupitia elimu niliyoipata, nimefanikiwa kukopa shilingi 500,000 kwenye kikoba na kulipa ada, hivi sasa mtoto wangu anasoma,” anasema.

Hadi sasa kikundi chao kina hisa yenye thamani ya shilingi milioni tatu, yeye anafanya biashara ya kuuza na kukopesha kukopesha vitenge.

Mwanakijiji Lucia anasema, wanawake wengi hivi sasa katika kijiji chao hawaendi tena kukata miti msituni.

“Kabla ya VICOBA, hali ilikuwa ngumu, watu walienda porini kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kuharibu msitu, sasa hivi hali ni nzuri, VICOBA vimetusaidia…” anasema.

Kuna baadhi ya wanawake wanauza bidha kama nyanya, ndizi, mboga, badala ya kutegemea kuuza kuni na mkaa. 

Pia, kupitia mafunzo hayo, anataja kuwa wamefanikiwa kuanzisha mfuko wa jamii ambao hivi sasa una kiasi cha shilingi 700,000- na kuna wanachama 30, kati yao, wanaume ni wawili.

Lucia anahitimisha, kwamba kwenye biashara ya kuuza vitenge, alianza na mtaji wa shilingi 300,000 na sasa uko shilingi milioni 1.5.