Mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Bara katika namba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:30 AM Dec 30 2024
Fei Toto
Picha: Mtandao
Fei Toto

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara umemalizika kwa timu zote kucheza michezo 15 ya kwanza, huku chache zikiwa zimeshaanza kucheza mechi za mwanzo za mzunguko wa pili.

Hadi mzunguko huo unamalizika Simba iko kileleni, imemaliza mwaka 2024 ikiwa kwenye kilele cha msimamo na itaendelea kuwa hapo hadi Januari 20, mwakani, mechi za Ligi Kuu zitakapoendelea kwa mujibu wa ratiba.

Wakati Ligi Kuu ipo katikati, baadhi ya timu zimeweka rekodi na takwimu nzuri za kuvutia na zisizovutia.

Wachezaji nao hawapo nyuma, wamekuwa wakishindana kuweka rekodi nzuri ambazo zimewafanya waendelee kuzungumzwa na kuwa midomoni mwa mashabiki wa soka.

Katika makala haya, tunakuletea rekodi na takwimu mbalimbali za timu pamoja na wachezaji hadi kufikia mzunguko huo na kuziweka kwa mtindo wa namba...

40# Hizi ni pointi za Simba ilizokusanya hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa imeshacheza michezo 15 ya mwanzo.

36# Ni dadi ya pointi za Azam FC, ilizokusanya mpaka sasa ikicheza michezo 16 na kukamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.

33# Baada ya kufungwa bao 1-0 juzi kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida, timu ya Singida Black Stars ina idadi hii ya pointi, ikiwa kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu.

31# Namba hii inasimama kama idadi ya mabao ya kufunga ya Simba ambayo mpaka sasa ndiyo timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

29# Timu ya KenGold imefungwa idadi hii ya mabao na kuwa timu inayoongoza kwa kuruhusu mabao mengi kwenye Ligi Kuu hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

25# Namba hii ni idadi ya mabao iliyofunga Azam FC mpaka sasa kwenye ligi, ikiwa inashika nafasi ya tatu kwa timu iliyofunga mabao mengi kwenye ligi, baada ya Simba na Yanga.

19# Ni pointi za Mashujaa iliyo kwenye nafasi ya saba na JKT Tanzania iliyo kwenye nafasi ya nane.

17#  Ni idadi ya pointi zinazomilikiwa na timu mbili. Coastal Union na Namungo zote zina pointi hizi kila moja, lakini Wanamangushi wanashika nafasi ya 10 na wenzao Namungo ya 11 kwenye msiamamo wa ligi.

13# Namba inayosimama kama idadi ya mechi za ushindi ambazo Simba imeshinda mpaka kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

12# Hizi ni 'clean sheets' za kipa wa Simba, Moussa Camara, akiwa ni golikipa anayeongoza kwa kukaa langoni bila kuruhusu wavu wake kuguswa.

9# Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum anaongoza kwa kutoa pasi za mwisho za mabao kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, akiwa amefanya hivyo mara idadi hii.

8# Straika wa Singida Black Stars, Elvis Rupia, ndiye anaongoza kwa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, akiwa na idadi hii ya mabao.

7# Namba hii inasimama kama idadi ya mabao ambayo timu za Prisons na Pamba Jiji zimefunga. Ndizo timu zilizofunga mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza. Prisons inashika nafasi ya 13 na Pamba Jiji ya 14 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

6# Hizi ni pointi za KenGold, timu ambayo inashika mkia wa ligi mpaka kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

5# Ni idadi ya mabao ya Prince Dube kabla ya mchezo wa jana kati ya Yanga na Fountain Gate, lakini pia inasimama kuwa ni idadi ya 'asisti' za kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua, akifikisha idadi hiyo juzi kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars.

3# Kipigo cha mabao 1-0 ilichokipata juzi dhidi ya Simba, kimeifanya Singida Black Stars kupoteza mechi mara idadi hii. Ilifungwa pia dhidi ya Yanga bao 1-0 na Azam mabao 2-0.

2# Ni idadi ya mechi ambazo Yanga na Azam zimepoteza kwenye ligi mpaka sasa, kabla ya Wanajangwani kushuka dimbani jana dhidi ya Fountain Gate.

1# Namba hii inasimama kwa Simba ambayo imepoteza mechi moja na sare moja tu hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu. Pia inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu mpaka sasa.

0# Kabla ya mchezo wa jana wa Ligi Kuu kati yake dhidi ya Fountain Gate, Yanga ndiyo ilikuwa timu pekee ambayo haijatoka sare.