Mwenge Uhuru wakagua kilichoagizwa RUWASA, kunakolengwa ‘maji bombani’

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:54 AM Aug 29 2024
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava, alipozindua mradi wa majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria katika vijiji vya Seseko na Ngundangali, wilayani Kishapu, na kuwanufaisha wakazi 15,500 mwezi huu.
PICHA: MARCO MADUHU
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava, alipozindua mradi wa majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria katika vijiji vya Seseko na Ngundangali, wilayani Kishapu, na kuwanufaisha wakazi 15,500 mwezi huu.

MTU anapotaja msamiati ‘maji’ una tafsiri pana, kwamba ni kitu chenye mustakabali mpana sana katika maisha ya umma na viumbe hai vingine.

Ni hatua maji yanabaki na tafsiri ya maendeleo ya kijamii, hadi kiuchumi, huku mwongozo wa Sera ya Maji ya Mwaka 2002 nchini, inasema wananchi wa vijijini wanapaswa kupata huduma ya maji kwa asilimia 85 huku mijini ikibaki asilimia 95. 

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, naye akiweka katika ajenda zake kuu ya malengo kitaifa, katika tafsiri ya kumletea unafuu Mtanzania na hususan mwanamke aliyeko kijijini akifuata maji umbali mrefu, ameibebesha msamiati ni ‘Ajenda ya kutua ndoo.’ 

Katika sura ya utekelezaji kuanzia mzizi wa sera  tajwa, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), ilianzishwa mwaka 2019 na tangu hapo imekuwa inatekeleza miradi ya maji vijijini, lengo mojawapo ‘kumtua ndoo kichwani mwanamke, kumwondolea adha ya kufuata maji  umbali mrefu.” 

Mnamo Agosti 10 mwaka, mbio za Mwenge wa Uhuru zikiwa mkoani Shinyanga, zikazindua miradi mitano ya maji safi na salama katika halmashauri tano za mkoa; Kishapu,Wilaya ya Shinyanga, Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama, zinazotekelezwa na Ruwasa.

 Meneja wake wilayani Kishapu, Mhandisi Dicksoni Kamazima, anasema mradi ambao umezinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru ukiwa Seseko hadi Ngundangali, kwa maji kutoka Ziwa Victoria, ukinufaisha wananchi 15,500, akifafanua: “Mradi huu wa maji, chanzo chake ni Ziwa Victoria na gharama zake ni shilingi bilioni 2.8.” 

Meneja wa Ruwasa wilayani Kahama, Mhandisi Maduhu Magili, anasema katika eneo lake, miradi mitatu ya maji imezinduliwa na Mwenge wa Uhuru, ikiwanufaisha wananchi 2,400 kwa gharama shilingi milioni 64.6 na upanuzi wake hadi kwa wanavijiji 9,268 wa Manispaa ya Kahama; pia katika Halmashauri ya Ushetu, utanufaisha wananchi 7,563 katika vijiji viwili. 

“Wananchi wa vijiji hivi hawakuwa na maji kabisa, lakini Ruwasa tukaona tutoe kipaumbele,” anasema Mhandisi Magili. 

KIKOHOZI CHA WABUNGE

Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo, anasimulia mateso ya muda mrefu ya wananchi wake waliokosa maji safi na salama, sasa kukishuhudiwa mageuzi kuwapo huduma ya majisafi na salama.

 Huku akidokeza yamebakia maeneo machache kufikiwa na huduma rasmi za maji, Butondo anaeleza: “Wilaya ya Kishapu ni kame sana! Kipindi cha kiangazi, wananchi walikuwa wakipata shida ya kupata maji na hata kuchangia maji na mifugo...” 

Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, anasema wananchi wa jimbo lake bado wako katika hali mbaya ya ukosefu wa maji safi na salama, akiiomba Ruwasa iongeze juhudi za usambazaji mtandao wa maji, ili kuvifikia vijiji, kufanikisha “kumtua ndoo kichwani mwanamke.’ 

Naye, Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum, anasema katika vijiji 126 vilivyopo wilayani Shinyanga, matarajio yaliyoko kwamba hadi kufikia mwakani 2025 vyote vitakuwa na maji safi na salama kutoka Ziwa Vitoria.

 Anasema hadi mwaka huu 2024, vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma ya maji safi na salama, viko 97 na tayari viko kwenye mchakato wa kupelekewa huduma hiyo.

 WAKIMBIZA MWENGE

 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Godfrey Mnzava, anasema katika utekelezaji miradi hiyo ya maji, wananchi wanapaswa kuvutiwa maji majumbani mwao, ili kutekeleza dhana ya Rais Dk. Samia ya ‘kumtua ndoo kichwani mwanamke, kwa kuchota maji bombani nyumbani kwake na siyo kwenye vituo.’

 Anasema Rais Samia amekuwa akiidhinisha fedha za miradi ya maji ili kumtua ndoo kichwani mwanamke na akaitaka Ruwasa iongeze kasi ya kusambaza huduma ya maji kwa wananchi katika maeneo mengi vijijini.

 “Huduma ya maji haina mbadala, na kama kauli yenu ya Ruwasa inavyosema “Ruwasa maji bombani” endeleeni kusambaza maji zaidi kwa wananchi, na pia kuwaunganishia majumbani mwao ili kumtua ndoo kichwani mwanamke,” anasema Mnzava.

 Anawasihi pia wananchi ambao wametekelezewa miradi hiyo ya maji kwamba waitunze miundombinu yake na kutoifanyia hujuma, ili waendelee kupata kuhuma ya majisafi na salama kwa muda mrefu.

 WANUFAIKA WALONGA

 Mwanamke Sabina Lukas mkazi wa kijiji cha Chona Halmashauri ya Ushetu, anasema upataji wa majisafi na salama kijijini humo umewaondolea matatizo ambayo wamekuwa wakikumbana nayo, kwamba licha ya kuteseka kubeba ndoo kutoka umbali mrefu zaidi hata kilomita tatu pia ndoa zao zilikuwa mashakani wakisingizwa ‘kuchepuka.’

 Anasema ukosefu wa maji maeneo ya vijijini, wanaoteseka ni wanawake, kwa sababu ndiyo wanaolea familia, kuhakikisha anachokitafsiri “familia imekula na baba ameoga.”

 Pia, anasema inapokuwa wakichelewa kurudi kutoka safari ya kuchota maji, nako wanaulizwa maswali mengi hata kuishia ugomvi.

 “Upatikanaji wa maji vijijini ni furaha kubwa sana kwetu sisi wanawake kwa sababu hata ndoa zetu zinakuwa na amani sana, licha ya kuteseka kubeba ndoo ya maji kichwani umbali mrefu,”anasema Sabina.