TANGANYIKA na Zanzibar zilipoungana na kuunda Jamhuri ya Muugano Tanzania, Rais Dk. Samia Suluhu Hasan, ana ufafanuzi wake kuhusu mitaji yake ya maendeleo, akiitaja kadhaa; ushirikiano wa kihstoria, umoja wa pande hizo mbili na kundi la vijana.
“Fikra zangu hutawaliwa na picha ya vijana wanne kutoka pande zote mbili za Muungano. Vijana hao, wawili wa kiume na wawili wa kike, waliomsaidia Mwalimu Julius Nyerere kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar, kutoka kwenye vibuyu viwili …” anatamka.
“Baada ya kuuchanganya, hakuna teknolojia inayoweza kuurudisha udongo ule,” anaongezea, katika hotuba ya Muungano, Aprili mwaka huu, akiusifu:
“Ni ‘Muungano maalumu na wa kipekee’ katika misingi ya utu, udugu, na umajumui wa Afrika (Pan-Africanism), umeweza kushinda majaribu mengi ya kuuvunja,” anatamka.
Rais Dk. samia anakumbusha wakati wa Muungano, Tanganyika na Zanzibar zilikuwa katika viwango duni vya maendeleo, wananchi wengi walikuwa masikini, akiongeza:
“Sekta za uzalishaji hususan kilimo kilikuwa chenye tija ndogo na hapakuwa na miundombinu ya kutosha ya usafiri na usafirishaji. Huduma za kijamii, elimu, afya, maji na umeme pia zilikuwa adimu na za kibaguzi.”
Anataja jukumu la kwanza baada ya Muungano lilikuwa kujenga uchumi endelevu na unaowanufaisha wananchi wote bila ya ubaguzi, wakiimarisha na kupanua huduma za kiuchumi na kijamii, kuwaongezea kipato wananchi.
“Jitihada zilizofanywa ndani ya miaka hii 60 zimesaidia kukuza Pato la Taifa kufikia Shilingi Trilioni 170.3 kwa takwimu za mwaka 2022, na pato la mtu mmoja mmoja kufikia wastani wa shilingi milioni 2.8 kwa mwaka 2022.
YALIYOIBUA MAENDELEO
Hapo Rais Dk. Samia, mzaliwa wa Zanzibar, anataja eneo mojwapo lilioibua maendeleo ni imani na dhamira ya waasisi na viongozi wake, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
“Walikuwa mstari wa mbele katika kudai uhuru kupitia vuguvugu la Umajumui la Afrika Mashariki na Kati, yaani Pan African Movement of Eastern and Central Africa, au kwa ufupi PAFMECA.
“Lengo la PAFMECA lilikuwa kujenga umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watu wa Afrika waliokuwa chini ya utawala wa kikoloni wakidhamiria kuunganisha nchi zao mara baada ya kupata uhuru,” anasema.
Pia, anatafsiri suala la undugu wa kihistoria, Tanganyika na Zanzibar, waliotenganishwa na mipaka ya ukoloni, lakini kwa asili walikuwa jamii moja.
KINACHOENDELEA SASA
Rais Dk. Samia anataja kuwapo Tume ya Pamoja chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, inayosikiliza na kutatua changamoto za Muungano zinapojitokeza.
Hapo anataja kuanzia mwaka 2021 hadi Aprili mwaka huu, kuwapo hoja 15 kati ya 18 zimeshapatiwa ufumbuzi. Tume iliyoundwa inafanya kazi ya kulinda dhamira ya udumishaji muungano nchini.
Eneo lingine Rais Dk. Samia analitaja katika Muungano, ni kuiwezesha Tanzania kuwa na ushawishi mkubwa kikanda na kimataifa, akinena kupitia nguzo ya Diplomasia ya Uchumi, imevuta mitaji, uwekezaji, teknolojia, soko la bidhaa na huduma zitokazo nchini.
Hapo ndipo anataja zao mojawapo ni Tanzania kuufikia Uchumi wa Kati, tangu zama Serikali Awamu ya Tano, Dk. Samia akiwa Makamu Rais.
Hapo ana ufafanuzi, kupitia hotuba yake : “Nafarijika kwamba kwa sasa nchi yetu imefikia Uchumi wa Kati katika ngazi ya chini na jitihada zetu zote sasa kufikia uchumi wa kati, ngazi ya juu.
“Wastani wa umri wa kuishi (life expectancy) wa Mtanzania umeongezeka kutoka wastani wa miaka 45 mwaka 1964 hadi wastani wa miaka 67 mwaka 2024.
“Sensa ni moja kati ya mambo ya Muungano. Hadi sasa, zimefanyika sensa za watu na makazi mara sita. Sensa ya kwanza ilionyesha Tanzania kuwa na watu milioni 9.6 na ile ya mwisho 2022 imetuonyesha idadi ya Watanzania kuwa milioni 61.741,” anaeleza.
Anaitaja kuwa ni taarifa yenye msaada mkubwa kwa mipango ya kiserikali na kutuongoza matumizi ya rasilimali:
Pia, anataja serikali mbili nchini, zimeendelea kuibua na kutekeleza programu na miradi inayolenga kupunguza umaskini wa kipato, inainua ubora wa maisha na ustawi wa jamii kwa pande zote mbili za muungano.
Kwa upekee, anaugusa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), uliotekelezwa kwa awamu tatu sasa, umeonyesha uwezo wa kaya kumudu gharama za mahitaji ya msingi umeongezeka.
“Vilevile matumizi ya pembejeo yameongezeka, hivyo kuongeza tija kwenye kilimo, na matumizi ya huduma za afya pia yameongezeka na mahudhurio shuleni kwa watoto nao umeongezeka,” anasema.
Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia, miradi mingine iliyotekelezwa katika pande zote mbili, inajumuisha Programu ya Usimamizi wa Bahari na Pwani (MACEMP) na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na
Sekta ya Mifugo (ASDP – L).
Vilevile, anaitaja Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani ya Mazao na uboreshaji wa Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF); Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (ERPP); na Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Maeneo ya Pwani (LDCF).
Ni orodha ndefu inayojumuisha, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF), mfumo wa Wabunge, unaowanufaisha wananchi katika sekta za afya, maji, ajira, elimu na miundombinu.
Katika elimu ya juu, Rais Dk. Samia akataja kuwapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pekee wakati nchi zinaungana mwaka 1964, lakini kutimu miaka 60 ya Muungano kuna vyuo vikuu 49, vikiwamo 19 vya umma na 30 binafsi. Kati yake, 46 viko Tanzania Bara na vitatu Zanzibar.”
“Mwaka 2023/24, kulikuwa na jumla ya wanafunzi wa elimu ya juu 240,523, ikilinganishwa na wanafunzi 14 tu waliokuwapo wakati nchi zetu zinaungana” anatamka Rais Dk. Samia.
“Tangu kuanzishwa Bodi ya Mikopo mwaka 2004, wanafunzi wapatao 705,622 wamepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 6.69, wanufaika wanawezeshwa kusoma kwenye vyuo vya Serikali na binafsi,” anasema Rais Dk. Samia.
JINSIA NA UTUMISHI
Katika eneo hilo, akiweka rekodi kuwa rais wa kwanza nchini mwanamama, anasema: “Suala la usawa wa kijinsia zote liliingizwa kwenye Katiba, hatua iliyowezesha uwakilishi wa wanawake bungeni kuongezeka.”
Anafafanua ni kutoka watatu mwaka 1964 kwenye bunge la kwanza la Muungano, hadi wanawake 148 (asilimia 37.75) ya wabunge wote 392.
Rais Dk. Samia anaendelea: “Wakati huo, hapakuwa na mwanamke yeyote kwenye uongozi wa mihimili ya dola, yaani Serikali, Bunge na Mahakama.
“Leo hii, kati ya mihimili mitatu ya dola, wanawake wanaongoza mihimili miwili, Serikali na Bunge, jambo linalothibitisha kuendelea kuimarika kwa usawa wa kijinsia,” anafafanua
MAPINDUZI YA MAWASILIANO
Rais Dk. Samia anaeleza kushamiri miliki ya simu za mkononi kwa umma, wamiliki wakiongezeka, ikikadiriwa kuwapo laini za simu zaidi ya milioni 72 na watoa huduma wameongezeka hadi watano, wakiwa na huduma zenye kasi mpya inayoitwa 5G.
“Kiasi cha laini milioni 53 zimesajiliwa kutumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi,” anaongeza Rais, akiitolea ufafanuzi, ngazi ambayo sasa asimilia 98 ya Watanzania vijijini wananufaika.
“Maendeleo haya yamechangiwa na uamuzi wa serikali kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, maarufu UCSAF wenye jukumu la kuimarisha miundombinu ya mawasiliano vijijini.
“Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 UCSAF imeweza kujenga minara 1,435 iliyowezesha zaidi ya wananchi milioni 16 katika kata 1,306 na vijiji 3,838 kupata mawasiliano ya uhakika…. na sekta binafsi zimewezesha kuimarika kwa huduma.”
CHANGAMOTO ZAKE
Rais anataja katika miaka 1970 hadi 1980, Muungano nchini ulikumbwa na changamoto kama; ukame na njaa (hasa 1974 ), mtikisiko na anguko la uchumi duniani, bei ya mafuta na vyakula kupanda duniani, ukiumiza uchumi nchini.
Lingine linaloambatana nayo, mwaka 1977 Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilivunjika, hata kuilazimu serikali kugharamia upatikanaji huduma za EAC, huku mwaka mmoja baadaye, ikazuka vita dhidi ya utawala wa Idd Amin wa Uganda.
Hapo Rais anaitolea ufafanuzi: “Fedha zilizotengwa kwa maendeleo yetu na rasilimali nyingine zikaelekezwa kugharamia vita hivyo.
“Vilevile, kwa nyakati mbalimbali, katika soko la dunia tulikumbana na anguko kubwa la bei za mazao yetu ya biashara kama vile chai, mkonge, kahawa, karafuu na pamba, hali iliyoathiri ukuaji uchumi wetu uliokuwa unaimarika vizuri.
“Aidha, magonjwa kama vile UKIMWI, Kipindupindu, Homa ya mafua ya ndege, na hivi karibuni Uviko 19, nayo yalitikisa Taifa letu.
Kwa upande mwingine, miaka ya 2001 hadi 2007 tulipata changamoto ya kisiasa Zanzibar, iliyosababisha baadhi ya washirika wetu wa maendeleo kusitisha misaada.
Mambo haya yote, yalitufanya tuunge nguvu kitaifa, tuimarishe umoja na mshikamano wetu, uliotujengea uwezo wa kuhimili kadhia zote hizo, na kulivusha Taifa letu likiwa salama na imara zaidi.”
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED