Yanga yafunika Ligi U-20, Azam, Simba zinasuasua

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:07 AM Nov 22 2024
Yanga yafunika Ligi U-20
Picha: Mtandao
Yanga yafunika Ligi U-20

TIMU ya soka ya vijana ya umri chini ya miaka 20 ya Yanga (u-20), inaongoza katika Kundi A, ikicheza michezo minne, ikishinda mitatu, sare moja, ikifunga jumla ya mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.

Kwa mujibu wa msimamo uliotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa timu za vijana ambazo timu zao kubwa zipo Ligi Kuu, Yanga inafuatiwa na Azam FC yenye pointi tisa, ikicheza michezo minne, lakini ikifunga mabao tisa tu na kuruhusu matano.

Msimamo unaonyesha Dodoma Jiji inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba, huku Pamba Jiji,  Tabora United, na Kagera Sugar zote zina pointi sita kila moja, Mashujaa FC nafasi ya saba ikiwa na pointi nne, na Singida Black Stars ikiburuza mkia ya kundi hilo, licha ya kucheza michezo minne, lakini haina pointi.

Kundi B linaongozwa na JKT Tanzania ambayo imejikusanyia pointi tisa katika michezo minne waliyocheza, ikishinda tatu na sare moja, ikifuatiwa na Prisons ambayo ina pointi saba.

Simba, inashika nafasi ya tatu ya kundi hilo, ikiwa pia na pointi saba, lakini ikizidiwa na uwiano wa mabao ya kufunga na Prisons.

Maafande hao wamefunga mabao saba na kuruhusu saba, huku Simba ikifunga matano na kuruhusu pia matano.

Coastal Union na KenGold zote zina ponti sita kila moja, Fountain Gate nafasi ya sita ikiwa na pointi tano, KMC na Namungo zina pounti tatu kila moja, lakini Namungo ikiwa mkiani kutokana na kufunga mabao manne tu, huku KMC ikifunga saba.