KUKOSA ufahamu wa masuala ya usawa kijinsia na uhaba wa miundombinu muhimu shuleni ni miongoni mwa vichocheo vinavyowarudisha nyuma wasichana na kukwamisha maendeleo yao kielimu.
Ili kufikia usawa wa kijinsia kwenye elimu, wadau wameanzisha mkakati wa kuboresha miundombinu ya maji, usafi wa mazingira, kuondoa ukatili wa kingono na kijinsia shuleni ili wasichana wasikatishe masomo.
Taasisi ya HakiElimu imezindua mradi wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia katika Elimu (MMUKE), mkoani Tanga utakaofikia shule za msingi 16 na za sekondari 24 za mikoa minane ya Bara kwa gharama ya Sh.bilioni 7.8, ikishirikiana na Serikali ya Canada.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa HakiElimu, Dk.John Kalage, anasema lengo ni kuwekeza vifaa vya maji, usafi wa mazingira na wa mtu binafsi ili kufanikisha jitihada za wasichana kuendelea na masomo.
Anasema wanaotarajiwa kufikiwa ni wasichana 12,240 na wavulana 11,760 wenye miaka 10 hadi 19, walengwa wakuu kwenye wa mradi huo utakaofanyika kwa miaka minne.
Kwenye maji, anasema shule nyingi hazina vyanzo vya maji na mifumo ya uhakika, vifaa vya usafi wa mazingira na wa mtu binafsi.
“Kwa ushirikiano wa jamii, HakiElimu inaboresha mifumo hii ikizingatia mahitaji ya kijinsia kwenye shule 40 za mradi, kwa manufaa ya wanafunzi 24,000 wavulana na wasichana. Tunawekeza katika ujenzi wa visima vya maji na kujenga vyoo vya wasichana vilivyo na vyumba maalumu vya kubadilishia taulo na kujisitiri wakati wa hedhi,” anasema Dk.Kalage.
“Pia HakiElimu, tunaendesha mafunzo na kutoa elimu ya umuhimu na matumizi sahihi ya miundombinu ya usafi inayozingatia mahitaji ya kijinsia katika jamii za shule ikiwamo walimu, wanafunzi na wazazi.”
Dk.Kalage anasema lengo la kufanya hivyo ni ili kuwapo na ushiriki wa jamii yote na kwamba katika kufanikisha hili pia inawezesha vikao vya majadiliano katika jamii hiyo kwa lengo la kuhamasisha watu wa maeneo husika kuhusu usafi wa mazingira na usafi binafsi unaozingatia mahitaji ya kijinsia.
Jambo jingine ambalo anasema mradi huo utazingatia ni pamoja na kuimarisha klabu za jinsia kwa ajili ya kuwajengea uwezo wasichana walio katika umri wa kijalunga.
Kupitia klabu hizo, uelewa miongoni mwa wavulana na wasichana kuhusu haki zao sawa na usawa wa kijinsia utaongezeka na kuwa jukwaa la kuwaelimisha vijana kuhusu afya ya uzazi, hedhi na ukatili dhidi ya watoto.
Anasema klabu hizo zitakuwa na kazi ya kuhakikisha kwamba wasichana wanajua jinsi ya kujilinda na kwamba pia kutakuwapo na mafunzo ya kujenga uwezo kwa makundi hayo ambayo yatafanyika kwa ushirikiano na wauguzi wa eneo husika pamoja na dawati la jinsia la Jeshi la Polisi.
“Zaidi ya hayo, unalenga kuimarisha uwezo wa waangalizi wa wanafunzi shuleni (matroni) na walimu ili waendelee kutoa mwongozo kwa klabu za jinsia kuhusu mada kama za afya ya uzazi, namna ya kufanya maamuzi, haki za wasichana, shinikizo la rika, mipango ya maisha ya baadaye na mwongozo wa taaluma,” anasema Dk.Kalage.
“Tunaamini mambo yote haya yatawajenga wasichana kujiamini na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi. Kwa hiyo wasichana wa klabu za jinsia, wanahimizwa kutumia mbinu ya rika katika kujifunza, kushirikiana walichojifunza na vijana wengine kupitia mikutano iliyoandaliwa, ziara za kielimu, matukio mbalimbali pamoja na shughuli zinazojumuisha michezo na maigizo.”
Anasema kupitia mradi huo, HakiElimu inandaa kampeni za kujenga uelewa wa jamii kwa ajili ya kuongeza ufahamu wa jamii zinazozunguka shule kuhusu madhara na athari za ukatili wa kijinsia na kingono shuleni kupitia sanaa za maonesho ya jukwaani, ujumbe mfupi wa maandishi, ujumbe wa sauti na vipindi vya redio za kijamii.
Katika kuimarisha mbinu za kuzuia ukatili dhidi ya watoto katika shule za mradi, Dk.Kalage anasema shule zote zinazoshiriki zinakuwa na mifumo inayofanya kazi ya kuzuia ukatili huo wa kijinsia na kingono na ukatili dhidi ya watoto.
“Hii inajumuisha usimikaji, wa masanduku ya kutoa taarifa yanayoitwa ‘sauti yangu’ katika maeneo yanayofikika kwa urahisi ndani ya shule. Masanduku haya hufungwa kwa usalama na hufunguliwa kila wiki na timu ya marafiki wa elimu, matroni patroni na angalau wasichana wawili wa vilabu vya jinsia.
“Kwa pamoja wanapitia taarifa wanakubaliana hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji, iwapo tukio la unyanyasaji linaripotiwa mamlaka husika hujulishwa mara moja kwa hatua zaidi, tunatambua kazi inayofanywa na marafiki wa elimu katika kufuatilia mara kwa mara kesi zinazoripotiwa,” anasema Dk.Kalage.
Anasema katika kufanikisha kazi ya kupambana na vitendo va ukatili, wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama pamoja na mashirika mengine katika kuhakikisha kwamba kesi za watoto dhidi ya ukatili zinashughulikiwa ipasavyo na kufikia tamati kwa kupata suluhisho stahiki.
Anasema wanaunga mkono ujenzi na ukarabati wa hosteli za wasichana katika shule zilizochaguliwa ili kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu na kuhakikisha wasichana wanakuwa katika mazingira salama.
Katika ngazi za wilaya anasema utatekelezwa wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Kilosa Morogoro, Mpwapwa Dodoma, na Babati mkoani Manyara.
Dk Kalaghe anazitaja wilaya nyingine kuwa ni Iramba mkoani Singida, Muleba Kagera, Musoma Mara na Korogwe mkoani Tanga.
“Mbali na wanafunzi, pia utagusa walimu 100 kutoka shule 40 na wajumbe 16 wa vikundi vya marafiki wenye mtazamo wa kijinsia wanaosimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku shuleni katika jamii,” anasema DK. Kalage.
Kadhalika, aansema utawafikia wanajamii 140 na maofisa 320 wa mamlaka za serikali za mitaa kupitia mijadala ya kijamii na mafunzo ya kujenga uwezo yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu kuzuia ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kukuza usawa wa kijinsia katika elimu.
Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Canada, Carol Mundle, anasema wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya uanzishwaji wa mradi huona kwamba wanaamini mradi huo utasaidia kongeza ufaulu wa wanafunzi katika maeneo unakotekelezwa.
Anaipongeza Tanzania kufikia usawa wa kijinsia kwenye maeneo ya kuandikisha wanafunzi shuleni na kuwahimiza wazazi na walimu kushirikiana na HakiElimu kwa sababu na wao ni sehemu ya uendeshaji wa mradi huo.
Mkuu wa Wilaya Korogwe, William Mwakilema, anasema wataendelea kutoa ushirikano kupitia mradi huo ili kufanikisha utekelezaji na upatikanaji wa matokeo yaliyokusudiwa.
Anasema ni muhimu kwa wananchi na halmashauri hiyo kuuelewa na kuendelea kufuatilia na kutoa ushirikano katika maeneo unakotekelezwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED