USAFI wa mazingira na ulinzi shirikishi ni mambo yanayowahitaji wananchi kuchangia fedha za kulipa makandarasi wanaosafisha na sungusungu wanaowalinda usiku, ni jambo lisilokubalika kwa baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam.
Eneo mojawapo ni Mtaa wa Machimbo uliopo Segerea wilayani Ilala, huko kinachotokea ni baadhi ya wakazi kukaidi kulipa ada ya kuzoa taka na ya ulinzi shirikishi pia.
Ukaidi huo husababisha maeneo ya wakorofi hao kukithiri uchafu na uhalifu hasa wizi na vibaka wanaoranda randa wakati wote.
Kukwepa kulipa ada hizo, kumesababisha mitaa wanakoishi wanaokataa kuchangia gharama kuitwa mtaa wa ‘wagumu’.
Ni jina linalotumiwa na vijana waliopewa kazi ya kuzoa taka katika mtaa huo wa Machimbo wakati wakipeana ishara wanapofika kuhimiza kulipa ada hiyo.
Wafanyakazi hao wanadai kuwa kitendo hicho cha wagumu kinakwamisha kampeni ya kuweka mazingira ya mitaa kwenye usafi, kutokana na taka kuzagaa kwenye makazi yao na nyingine kutupwa majumba ambayo ujenzi wake haujakamilika hasa mapagale.
Ukifika Machimbo unakutana na taka zikiwa zimejaa kwenye viroba, nyingine hutelekezwa barabarani, vichochoroni, mitaroni, nje ya nyumba za watu na maeneo ya wazi, kama viwanja vya mpira na vya mafurushi hayo yakitupwa nyakati za usiku.
Ofisi ya mtaa huo na wafanyakazi wa kandarasi hizo, wanapita mitaani kuutangazia umma kwa vipaza sauti kuhamasisha wananchi kuzoa taka walizokusanya kwenye makazi yao.
Kitendo hicho kimezua malalamiko pia baadhi ya wakazi wa mitaa hiyo wanadai kudhalilishwa kwa kuitwa wa wagumu, wakisema wanatoa ushirikiano kwa kuchangia pesa baada ya kutangaziwa, lakini magari hayafiki kwenye makazi wanapozikusanya kutokana na ubovu wa barabara.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Machimbo, Mariamu Machicha, katika mikutano na wananchi hivi karibuni, anasema changamoto hiyo ni moja ya nyingi zinazoukabili mtaa wao.
Kwa mujibu wa Mariam amekuwa akiwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa makandarasi na walinzi shirikishi kwa kukusanya taka na kuchangia walinzi.
Anasema pamoja na jitihada ambazo ofisi yake imekuwa ikifanya baada ya kupokea malalamiko, kukutana nao kwa kuwafuata kwenye makazi nao na mikutano ya hadhara, bado wapo ambao wanakaidi kulipa ada ya taka na kupelekea baadhi yao kukamatwa na kutozwa faini kwa kutupa taka ovyo.
“Mkandarasi chini ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ameondoa kero ya takataka kwa kiasi,” anasema Mariam na kuongeza kuwa bado kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi.
MACHIMBONI NINI?
Baadhi ya wakazi wa Machimbo wanasema asili ya jina la Machimbo linatokana na mtaa huo katika miaka ya nyuma kutumika kuchimba mchanga ambao ulikuwa ukitumika kwenye ujenzi na kupiga matofali maeneo mengine Dar es Salaam.
Baadhi ya maeneo yaligeuka mashimo ambako kuna nyumba zimejengwa na kukabiliwa na chemichemi zinazotiririsha maji kwa mwaka mzima na kuwa kero kwa watu wanaoishi kwenye maeneo hayo.
Sehemu hizo zimekuwa vilindi vya maji taka kutoka vyooni na kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa ya milipuko.
Akizungumzia kuhusu maji taka hayo, Mariam, anasema kamati ya mazingira ya mtaa, ofisa mtendaji kata na ofisa afya wanashirikiana kuondoa tatizo la maji yanayotiririshwa barabarani na kuzidi kukera wakati wa mvua.
Mariam anasema wanakagua kubaini ukweli wa malalamiko wanayopokea, kutoa maelekezo na wakati mwingine kuchukua hatua, lakini malalamiko bado yapo sehemu nyingine na yanayosababishwa na chemchemu.
BARABARA
Akizungumzia barabara anasema Mtaa wa Machimbo una barabara moja iliyojigawa kwenye kuhudumia makazi na ofisi mbalimbali, lakini ingawa serikali iliiwekea kifusi bado kuna mashimo.
Aidha, anasema kamati ya mtaa imeendelea kupunguza mashimo kwa kuweka vifusi na kuvisambaza kwa nyakati hasa pale barabara zinaposhindikana kupitika.
Kuhusu utiririshaji maji taka barabarani, Mariam anasema nayo ni changamoto inayoukabili mtaa wa Machimbo na kuendelea kuchafua mazingira.
Anasema changamoto hiyo inasababishwa na maeneo mengi kukosa barabara za kuingia kwenye makazi kutokana na ujenzi holela, hivyo magari kushindwa kupita kwenye kutoa huduma ya kunyonya maji hayo na mengine baadhi ya mashimo kufurika.
“Kijiogrofia, maeneo mengi ya mtaa huu ni chemchem, pia kuna ujenzi holela wa makazi na kukosekana kwa barabara," anasema Mariam na kuongeza:
‘’Kutiririsha maji barabarani kumesababisha barabara nyingi kuharibika na kubaki mashimo, adha ya usafiri kwenda kwenye makazi ya watu kutokana na magari kushindwa kupita.’’
Anasema barabara nyingi za Machimbo zimeharibika vibaya na kupelekea wakati mwingine kutopitika kutokana na madereva kunusuru vyombo vyao na uharibifu.
UHALIFU
Anaelezea kuwa kuna uhalifu na kutishia usalama akiitaja changamoto nyingine inayoukabili mtaa huo kuwa ni wananchi kukaidi kulipa ada ya ulinzi.
Mariam anasema ada hiyo ambayo ipo kwa mujibu wa sheria, ni fedha ambazo hutumika pamoja na mambo mengine kuwalipa askari jamii wanaolinda mtaa wake au makazi ya wananchi.
Anasema kitendo hicho kimechangia ulinzi ‘kusinzia’ kwenye baadhi ya maeneo, licha ya baadhi ya wananchi kulalamika kukithiri kwa vitendo vya wizi, ukiwamo wa kukata madirisha na kuiba simu, nguo na runinga.
Mtaa wa Machimbo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, una watu 10,333 kati ya hao, wanawake 5,568 na wanaume 4,765.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED