KIAFYA, Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Abdallah Chaurembo, leo hii anasimama kuwa shujaa wa ugonjwa wa kisukari.
Kisukari hasa cha aina ya pili, ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), ambayo chanzo chake kinatajwa kuwa ni mtindo wa maisha.
Chaurembo, ana simulizi yake kuhusu ugonjwa huo, akifafanua kwa hatua namna alivyoanza kuumwa, kufikia matibabu na safari ya Hija huko Mekka, kulivyobadili mtindo wake wa maisha.
Prof. Mohamed Janabi, mwanataaluma, tabibu na bingwa aliyebobea kwenye magonjwa yaliyomo kwenye kundi la NCDs, katika kitabu chake cha ‘Mtindo wa Maisha na Afya Yako’, anamuelezea baada ya kukutana na mbunge huyo huko Mekka, akimpa mbinu na tiba lishe ambayo Chaurembo anaitumia hadi sasa.
Msomi huyo wa afya, anaeleza zamani matibabu ya kisukari yalikuwa ni mgonjwa akishaanza kutumia dawa za kisukari, ataendelea na utaratibu huo maisha yote.
“Lakini kuanzia mwaka 2021, imekuja kugundulika kwamba uzito ukipungua na masharti yote yakifuatwa, kuna uwekezano wa mgonjwa kuachana na dawa na badala yake akawa anazingatia zaidi mtindo wa ulaji,” anasema Prof. Janabi.
SIMULIZI YA CHAUREMBO
Abdallah Chaurenbo anasimulia madhila ya ugonjwa huo, akitoa ushuhuda kwamba inawezekana kuachana na dawa za kisukari na masharti ya ulaji chakula yakazingatiwa sawasawa.
Aidha, anasema kwamba, mara ya kwanza kugundua kwamba anaugua kisukari ilikuwa mwaka 2010.
Anakumbukua kwamba ilikuwa ni majira ya saa l1 jioni akajikuta kila baada ya dakika 10 anakwenda haja ndogo.
Hatua ya kwanza aliyoichukua, ni kumpigia simu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani Temeke, Amani Malima na kumweleza hali aliyokuwa nayo.
Dk. Malima akamtaka atafute hospitali iliyokuwa karibu naye akapime sukari. Anasema alipata mahali pa kupima zahanati iliyokuwa jirani na kipimno kilionyesha kuwa sukari iko 35.8.
Baada ya muda Dk. Malima alimtafuta kujua anaendeleaje na kipimo kinasemaje. Chaurembo alimpa taarifa kuhusu kipimo. Taarifa hizo zilimshitua Dk. Malima na alimtaka aende Hospitali ya Temeke mara moja.
Hata hivyo, Chaurembo hakujishughulisha, kwa kuwa hakujua kwa kina madhara ya kisukari
Chaurembo anasimulia kwamba, Dk. Malima aliendelea kumpigia simu na mwishowe aliamua kumfuata mwenyewe nyumbani kwa gari la kubeba wagonjwa na kumpeleka hadi hospitalini.
Alipofika hospitalini Temeke, alimpima tena sukari na kukuta ikiwa 32.5. Alilazwa na kuwekewa dripu kwa siku tatu akiwa na fahamu. Baadaye sukari ilishuka mpaka 12 ndipo aliporuhusiwa kurejea nyumbani. Hapo aliishauriwa atafute mtaalamu wa kisukari, ili amsaidie kujua jinsi ya kuishi na ugonjwa huo.
Chaurembo, aliendelea na maisha akipata matibabu ‘hapa na pale’, mpaka alipokutana na Prof. Mohamed Janabi mwaka 2012 walipokuwa wamekwenda Hija Mekka.
Hata hivyo, wakiwa Mekka alipima sukari ikawa 22, ndipo alipopata fursa ya kumsikia Prof. Janabi kuhusu ugonjwa wa kisukari.
Anasimulia kwamba Prof. Janabi alimatahadharisha kwamba kisukari ni ugonjwa hatari, lakini mtu anaweza kuudhibiti.
Hata hivyo, anasema akammpa angalizo kwamba dawa za kisukari zilizopo ni za kushusha sukari, sio kumaliza tatizo.
“Jambo kubwa la kufanya ili kukabiliana na kisukari ni kubadili mtindo wa maisha. Kama mgonjwa wa kisukari hatabadili mtindo wa maisha katika ulaji wa chakula, atatumia dawa hizo milele,” akamwambia mbunge huyo.
Akamuongezea kwamba kama mgonjwa akifuata masharti ya wataalamu, anaweza kuacha kabisa dawa wakijadiliana na daktari wake akimtaka kitaalamu ‘it's a reversible disease’.
Chaurembo anaeleza katika siku 21 walizokaa huko Mekka, Prof. Janabi alimsaidia sana kujua ale chakula gani na muda gani, pamoja na muda wa kufanya mazoezi, ili kukabiliana na sukari mwilini.
Baada ya kumaliza Hija, Prof. Janabi alisema afike anakotibu, yaani Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ili waone jinsi anavyoweza kuendelea kuishi na kisukari.
Hata hivyo, anasema baada ya kurudi nchini aliendelea na shughuli zake na hakwenda kumuona, mpaka Prof. Janabi alipomtafuta na kumkumbusha kuhusu miadi yao ya kukutana kwa kumsisitiza ufuatiliaji wa karibu, kabla ya kusimamisha matumizi ya dawa kabisa.
MWANZO WA MASHARTI
Chaurembo anasimulia kwamba, Prof. Janabi, alimtaka mbunge huyo aende na familia yake mahali hapo, jambo ambalo Chaurembo alitii, akichukua wake zake wawili na watoto wakaenda kumwona Prof. Janabi
Kwa pamoja aliwafundisha kwamba, daktari na kliniki ya kwanza ya mgonjwa wa kisukari ni familia na akawauliza wanapata faida gani kwa baba yao (Chaurembo), mume wao akiwako na walijieleza kuwa huduma anawapatia kama vile nguo, pesa za matumizi na mambo mengine.
Prof. Janabi aliwaeleza kwamba ugonjwa wa kisukari una masharti ya kuishi nao na ni hakika kama yasipofuatwa, mgonjwa anaweza akapunguza uhai wake.
Aliwaambia wanafamilia hao kwamba wasipofuata masharti watampoteza baba au mume wao.
Pia, Chaurembo, alipewa masharti ya chakula ambacho mgonjwa wa kisukari kinamfaa, kikubwa ni kukaa mbali na lishe ya wanga ana akamtaka kuwa na kipimo cha sukari.
Akawashauri, wasile vyakula vya wanga nyumbani wakati Chaurembo akiwapo, kwamba ni hali itamsaidia kutokutamani na mwishowe hatokula.
Chaurembo anasimulia kwamba, vyakula vya wanga akiwa nyumbani vinaliwa kwa kificho, yeye kwake vinatawala ni ‘mbogamboga’, samaki, bamia, mlenda, ndizi bokoboko zikiwa mbichi tena changa na mtori kidogo.
Kutokana na kuendelea kupima sukari kila wakati, mkewe alimshauri kwamba kuna uwezekano wa kujikuta katika shinikizo kutokana na utaratibu wa kujipima kila wakati.
Badala yake, Prof. Janabi alimshauri ajenge tabia ya kujisikiliza mwill ili kugundua vitu ambavyo vikitokea atajua sukari mwilini haiko sawa.
Muda wote Prof. Janabi alisisitiza kwamba tutibu kisukari na siyo sukari kwa lugha yake “lets treat diabetes, not controlling sugar.’
CHAUREMBO ANAVYOJITAMBUA:
Chaurembo anasema dalili kama Kuna hitilafu ni kupata haja ndogo kila mara, koo kukauka (kiu), kuhisi ganzi; na mwili kuwaka moto.
Kwa kuwa shughuli zake nyingi za kiuchumi alikuwa anafanya mkoani Lindi na kuhudhuria Bunge, Jijini Dodoma, alipanga ratiba zake kwamba, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma bungeni, akienda haja ndogo mara moja ndani ya saa nane, anajua sukari yake iko vyema,
Akisafiri kati ya Dar es Salaam na Lindi, akienda haja ndogo mara moja, hapo anatambua sukari iko sawa;
Vilevile anasema, usiku inapomtokea analala na kuamka kwenda haja ndogo zaidi ya mara mbili, atajua sukari yake haiko sawa mwilini na
Akienda mara moja au kutokwenda kabisa usiku kucha, atajua kuwa sukari iko sawa.
Chaurembo anatoa ushahidi kwamba, mgonjwa wa kisukari akifuata masharti, hana sababu ya kutumia dawa. Anasema kwa sasa sukari yake huwa kati ya 4.7 ama 5.8, kiwango ambacho ni cha kawaida.
Hata hivyo, anatoa angalizo kwamba kuna wakati inakuwa 5.7, lakini baada ya kula inashuka zaidi hadi 4.5.
Baada ya kuzungumza na wataalamu wa tiba, aliambiwa kwamba asiache kabisa kula wanga, ila azingatie anakula saa ngapi na kwa kiasi gani. Hiyo, ni kutokana na ukwel mwili unahitaji wanga, ili uweze kujiendesha,
SOMO LA MUDA
Chaurembo anasema kuwa mtu akila wanga saa moja usiku, analala ni kuzalisha sukari.
Binafsi, yeye huwa anakula wanga kama ugali au wali saa nne asubuhi, kisha anaenda kwenye shughuli zake za kila siku.
Jioni huwa anakula matango, parachichi na mboga au ndizi mbichi za kuchemsha.
Vilevile, anaserma ingawa wapo matabibu wanashauri watu kula wanga (kama wali) sawa na ukubwa wa ngumi zao, kwake ilikuwa vigumu kwani ilionekana kuwa ni kiasi kikubwa kingesababisha kuibuka kwa sukari,
Yeye anaweka konzi moja ya wanga kisha anakula na samaki mkubwa, matunda mboga za majani kama matembele na mchicha.
Chaurembo anashauri kwamba, ni vyema kujiepusha na vyakula vya sukari, kwani madhara yake mwilini ni makubwa, kama kusababisha ugonjwa wa kisukari ambao nao husababisha magonjwa kama ya figo, ambayo matibabu yake ni ghali sana.
Anawashauri watu wanaoishi na wagonjwa wa kisukari, kuepuka kula mbele yao vyakula walivyokatazwa, kwani watawatamanisha na mwishowe nao watakula, hivyo kujiongezea matatizo ya ugonjwa huo.
“Mwisho, nashauri wagonjwa wa kisukari kuacha kutumia dawa za meno zenye utamu na badala yake watumie zenye chumvi chumvi na pilipili.”
NJIA KUEPUKA NCDs
Prof. Janabi katika kitabu hicho anasema, ni vyema ikajulikana wazi njia ya kujiepusha na magonjwa hayo ni rahisi na isiyokuwa na gharama.
Kikubwa zaidi anataka, ni kuepuka magonjwa hayo na mtu anapata faida na nafuu kubwa ya maisha. Kwa hiyo watu wanashauriwa wafanye yafuatayo:
Kubadili mtindo wa maisha kuhusu ulaji: Chagua unakula chakula gani; tambua unakula saa ngapi; fanya mazoezi, walau tembea hatua 10,000 kwa siku.
Bingwa huyo anasema pia kuepuka pombe na kuacha kuvuta sigara ni muhimu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED