Maagizo ya Rais yajibu mazito katika matamasha ya Utamaduni, Majimaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:13 AM Oct 29 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akikagua Makumbusho ya Songea, alipotembelea Tamasha la Majimaji, mwezi uliyopita.
Picha:Ikulu
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akikagua Makumbusho ya Songea, alipotembelea Tamasha la Majimaji, mwezi uliyopita.

NI wastani wa mwezi mmoja sasa kuna matukio makuu kitaifa na kimataifa yanayobeba sura ya historia, pia utalii wa nchi, ambayo yamefanyiwa sherehe maalum.

Hapo kunatajwa matamasha ya utamaduni kitaifa katika jozi na linalokukumbuka miaka 119 tangu kutokea vita vya Majimaji nchini, sasa pakibaki historia inayoipa nchi heshima na mvuto mkubwa wa taifa kitalii.

Wakati rekodi ya Tamasha la Vita Majimaji likiwa mara ya 10, kwa Tamasha la Utamaduni, ufafanuzi wake anautoa Naibu Waziri wa Waziri wa Sanaa, Michezo na Utamaduni, Hamisi Mwinjuma maarufu ‘Mwana FA’, Juni mwaka huu, akieleza:

"Rais (akiwa Mwanza 2021) aliagiza kufanyike kwa Tamasha la Utamaduni kila mwaka, ili kurithisha mali na utamaduni wa kitanzania...”

Pia, ni hivi karibuni nchini kulikuwapo ugeni mkubwa kutoka Ujerumani, taifa lililokuwa mahasimu vitani, wakienzi na kujutia yaliyojiri katika vita vya Majimaji, nao wakizuru mkoani Ruvuma kwa heshima ya kipekee.

Katika matukio ya mkoani Ruvuma, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mwanasheria Dk. Damas Ndumbaro, ndiye mwenyeji wake kipindi chote, akiwa kwenye jimbo analowakilisha, pia wizara yake ni mdau mwenye dhamana ya tukio 

Ulipofika ugeni wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ziarani mkoa wa Ruvuma, akijumuisha safari na ukaguzi wa maendeleo Kusini na Nyanda za Juu Kusini mwezi uliopita, akatembelea Makumbusho ya Vita vya Majimaji yaliyoko mjini Songea.

Hapo kukafafanuliwa lengo mahsusi kwa Rais kutembelea mahali hapo Makumbusho, ilikuwa kutoa heshima ya Kumbukizi ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji vilivyopiganwa kuanzia mwaka 1905 mpaka 1907.

Viongozi wenyeji waliompokea wamo wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiongozwa na Waziri Balozi Dk. Pindi Chana, Katibu Mkuu, Dk. Hassan Abbas na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk. Noel Lwoga.

Nao wakaambatana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma, Chifu wa Wangoni - Zulu Gama 1, wazee wa mila, pia dini mkoani.

Mzunguko wake Rais kwenye Ukumbi wa Historia ya Vita ya Majimaji, ukafikia Onyesho la Nyumba ya Inkosi (Chifu) wa kabila la Wangoni, alikoweka shada la maua katika Kaburi la Halaiki la Mashujaa 66 wa Vita ya Majimaji na Kaburi la Chifu Msaidizi (Nduna Songea Luwafu Mbano.

Historia iliyoko ni kwamba, vita vya Majimaji mizizi yake inaanzia eneo la Nandete Kipatimu, mkoani Lindi, ambako jamii la kabila la Matumbi zikajitokeza kwa ujasiri dhidi ya ukandamizaji huo wa kikoloni.

Hisia hizo za upinzani zikachochea moto ulioenea hadi Ruvuma, ambako nako umma ukichochewa na ujasiri wa majirani zao, wakaanza kuungana katika mapambano yao, dhidi ya uhasimu huo, wakiziharibu barabara walizolazimishwa kujenga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, akifunga sherehe hiyo ya kuadhimisha miaka 119 ya Vita ya Majimaji eneo la Nandete, Kata ya Kipatimu, Kilwa mkoani Lindi, anamsifu Rais Dk. Samia kuenzi mchango wa wapigania uhuru, ikiwamo historia ya vita vya Majimaji.

 “Wazee wetu walioongoza vita vile chini ya Jemedari Mkuu Mzee Kikwako Mbonde na mwanafalsafa wake mkuu na mhamasishaji Mohammed Ali Kinjekitile Ngwale, walipandikiza mbegu ya ari ya uhuru na uzalendo ambayo leo Rais wetu Dk. Samia Suluhu anaienzi kwa kuleta maendeleo. 

“…serikali yake (Dk.Samia) imeyatangaza rasmi kupitia GN 163 na 166 maeneo ya Nandete yaliyohusika na vita hiyo kuwa urithi wa Taifa na Kimataifa,” anatamka Dk. Abbas.

Mbali na viongozi wa kiserikali, pia maadhimisho hayo yalihudhuriwa familia za wapigania uhuru hao na mamia ya wananchi ambayo Dk. Abbas akaahidi kumwomba Rais Samia mahali hapo pajengwe Makumbusho Maalum ya Vita vya Majimaji.

Katika maadhimisho hayo, wadau mbalimbali wamechangia vitu na kuahidi vyakula zikiwamo kilo 1,500 za mchele, itakapotimu miaka 120.

Ni sehemu ya ziara, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akitoka katika nyumba ya mfano kwenye Tamasha la Utamaduni, Songea mwaka huu.
TAMASHA UTAMADUNI

Wakati awali akitangaza kilichotarajiwa kuajiri katika Tamasha la Utamaduni mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa akaahidi lingekuwa na mitazamo mikuu sita, akiitaja ni:

Mirindimo ya kiasili kuanzia mavazi, maonyesho, visasili na visakale; mdahalo wa kitaifa kuzungumzia mapambano dhidi ya viashiria vya mmomonyoko wa maadili na mchango wa jamii katika kupunguza na hatimaye kuondoa viashiria hivyo.

Eneo lingine ni onyesho maalumu la matumizi ya khanga ikiwa vazi la utamaduni wa Mtanzania; pia vikundi 25 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar; vikundi sanaa ya asili, ubunifu, utamaduni na muziki wa kizazi kipya.
 
 Aidha, kukatajwa mashindano ya uhifadhi wa ngoma za asili kwa vikundi 25 vya Tanzania Bara na Visiwani na kliniki ya sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katika hilo, Naibu Waziri Mwinjuma anatamka: “Tanzania ina utajiri wa makabila zaidi ya 120, tofauti yake inajenga umoja na yanaunganishwa na lugha ya Kiswahili….

"Kudumu kwa Utamaduni inategemea namna inavyorithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na kwamba urithi wa utamaduni ni kivutio kikubwa cha utalii, watalii wamevutiwa sana."

MILA, TAMASHA BIASHARA

Akifunga tamasha hilo Septemba 23 mjini Songea, Rais Dk. Samia, akatoa rai kwa wananchi na wadau wa sekta za utamaduni na utalii, kuufanya utamaduni kuwa biashara, ulete manufaa ya kiuchumi kwa nchi.
 
 Anataja madhumuni ya matamasha ya utamaduni yanayofanyika nchini, ni kuendeleza, kuenzi na kulinda utamaduni na mila za nchi, pia kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania kupitia kazi za sanaa na utamaduni.
 
 Kuhusu lugha ya Kiswahili, Rais Dk. Samia anasema, ni vigumu kwa Tanzania kujadili utamaduni wake, pasipo kugusa lugha anayotumia- Kiswahili, inayowaunganisha wananchi, hata kuwafanya kuwa na utamaduni mmoja.

Kwa mujibu wa Rais, ni mazingira yanayofungua fursa mpya za kiuchumi na kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, serikali imejipanga kufungua vituo vya lugha 100 vya Kiswahili, kwa kushirikiana na diaspora kote duniani.
 
 Anayeelekeza suala la mmomonyoko wa maadili kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ushirikiano na taasisi na wadau mbalimbali kulifanyia kazi suala, ili kuja na mapendekezo ya namna bora ya kulishughulikia.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas, akaitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuwachukulia hatua kali wote wanaohujumu mila na desturi za nchi kwenye mitandao ya kijamii.

“Ili Taifa liwe hai, lazima tuenzi na kuendeleza utamaduni wetu, na lazima turithishe utamaduni wetu kwa vijana na watoto na lazima tuwafundishe watoto wetu mila na desturi za Kitanzania, Kiswahili. Tuwafundishe miiko mbalimbali na historia yetu kwa kuwa hawa watoto ni taifa la kesho,” anahimza.

Anaendelea:“Sasa hivi duniani kuna suala linaitwa haki za binadamu. Ni jambo linalopaswa kuliheshimu na kulizingatia, lakini tusitumie haki za binadamu kuingiza utamaduni wa kigeni zisizofaa katika jamii yetu.

“Taasisi za elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu ni muhimu kurithisha utamaduni wetu una mila zetu katika kupambana na mmomonyoko wa maadili.

“Tuwafundishe maadili mema watoto wetu, viongozi wa dini mna kazi kubwa sana na maadili mengi ya dini yanatusaidia kulinda utamaduni wetu,” anasema Dk. Ndumbaro.

Akakumbusha kuwa mnamo Septemba 8, 2021 katika maadhimisho ya utamaduni wa Bujora mkoani Mwanza, Rais Samia Hassan Suluhu alitoa maelekezo kwa wizara hiyo kuandaa tamasha la kitaifa litakalofanyika kila mkoa.

“Maelekezo yale yametufanya tuwe Songea leo, uwepo wetu hapa ni maelekezo ya Rais Samia kudumisha tamaduni zetu,” anasema, akitaja Tanzania imebarikiwa kuwa na makabila zaidi ya 120 na lugha za kijamii zaidi ya 150 na ni utajiri wa kiutamaduni.

“Utamaduni wetu unategemea nguzo zifuatazo moja ni upendo, mshikamano, umoja, amani na utulivu, yote tunayoyafanya ili kuendeleza nguzo hizi,” anasema.

WAZIRI UTALII

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi, anasema, serikali inaendelea kushirikiana na jamii kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni, ikiwamo ujenzi na ukarabati wa nyumba za asili za Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam.

Akizungumza katika tukio la Tamasha la Utamaduni la Watu wa Kigoma, mwezi uliopita,  Dar es Salaam, Waziri akasema: “Ni dhahiri kwamba kwa mashirikiano haya ya serikali na wanajamii ya mkoa wa Kigoma katika tamasha hili hapa Kijiji cha Makumbusho.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Makumbusho ya Taifa, Dk. Oswald Masebo, anasema Tamasha la Siku ya Utamaduni wa Mtanzania ni la 30 tangu kuanzishwa mwaka 1994.

Ni takribani makabila zaidi ya 37 nchini ambayo yamefanya maonyesho yao tangu kuanzishwa utaratibu huo, kati ya makabila zaidi ya 120 yaliyopo nchini. 

Tamasha hilo lilipambwa na ngoma za asili, nyumbani, vyakula na vinywaji, mavazi ya asili.