Ligi Kuu ilivyoondoka na 'vichwa' vya makocha 18

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:02 AM Jun 17 2024
Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria, ni mmoja wa makocha 18 waliotimuliwa hadi kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu 2023/24, akiwa anaifundisha Simba.
Picha: Mtandao
Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria, ni mmoja wa makocha 18 waliotimuliwa hadi kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu 2023/24, akiwa anaifundisha Simba.

LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/24, ilioanza kutimua vumbi, Agosti 15 mwaka jana na kutamatika, Mei 28, ilisababisha makocha 18 kutimuliwa au kujiuzulu kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kufanya vibaya kwa timu zao.

Kwa mujibu wa rekodi za dawati letu la michezo, Singida Fountain Gate, ndiyo timu iliyoongoza kwa kutimua makocha wengi kuliko timu zote, huku timu tano tu kati ya 16, ndizo zilizoanza na kumaliza msimu wa makocha wao.

Jumla ya makocha 13 wazawa ndiyo waliopata nafasi ya kufundisha timu za Ligi Kuu msimu uliomalizika 2023/24.
 Mwandishi wa makala haya anakuletea taarifa za timu zote 16 zilizocheza Ligi Kuu na idadi ya makocha waliowatumia, huku akiorodhesha wote 19 ambao waliondoka kwenye vikosi vyao kabla ya kumalizika.
 
 1. Yanga
 
 Ndiyo timu iliyochukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa kukusanya pointi 80. 

Kiwango chake, ushindi iliyokuwa inaupata, wala haikushangaza kubaki kwa kocha wake yule yule, raia wa Argentina, Miguel Gamondi.
 
 2. Azam FC
 
 Licha ya kukamata nafasi ya pili kwa pointi 69, lakini ikiendelea kuwa kocha wake yule yule inayomtambua kama Kocha Mkuu, Msenegal, Youssouph Dabo, mwanzo wa ligi hadi mwisho.
 
 3. Simba
 
 Imeshika nafasi ya tatu hadi kumalizika kwa Ligi Kuu msimu uliomalizika. Mpaka inamaliza ligi tayari ilikuwa imeshaondokewa na makocha wawili. Ilianza na Roberto Oliveira raia wa Brazil, lakini alitimuliwa baada ya kipigo cha fedheha cha mabao 5-1 ilichokipata dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, Novemba 5 mwaka jana.

Jahazi likachukuliwa na kocha raia wa Algeria, Abdelhak Benchikha. Hata hivyo naye kabla ya mechi chache tu kukamilika kwa ligi, 'rigwaride' likamshinda, akabwaga manyanga mwenyewe, baada ya kuona jahazi linakwenda mrama, Kocha Mtanzania, Juma Mgunda ndiye alichukua jukumu la kumalizia ligi.
 
 4. Coastal Union
 
 Nafasi ya nne haikupatikana kwa lelemama, ilibidi viongozi wa timu hiyo kumtimua kocha, Mwinyi Zahera, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Wakati wanamtimua walikuwa chini kwenye msimamo msimamo wa Ligi Kuu, wakati wa mzunguko wa kwanza. 

Ikaamua kumleta Mkenya, David Ouma. Ikabaki hitoria. Leo hii imekata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
 
 5. KMC
 
 KMC ni timu moja kati ya timu tano ambazo zilianza na kocha wao mkuu na kumaliza naye Ligi Kuu msimu uliomalizika. Ilianza na Abdulhamid Moalin, raia wa Somalia, ambaye ameifanya timu hiyo kumaliza nafasi ya tano.
 
 6. Namungo FC
  
 Mpaka inamaliza ligi, ikikamata nafasi ya sita, tayari ilikuwa imetimua makocha wawili. Wa kwanza ni Mrundi Cedric Kaze aliyewahi kuifundisha Yanga, akaja Denis Kitambi ambaye awali alikuwa msaidizi, naye baadaye akaonyeshwa mlango wa kutokea, mwishoni wakamchukua Zahera akitokea Coastal Union, akamalizia ligi. 
 
 7. Ihefu FC
 
 Timu hii ambayo kwa sasa inaitwa Singida Black Stars, ikihama kutoka Mbarali, Mbeya na kwenda kufanya maskani wake mkoani Singida, ilianza na kocha Zubari Katwila. Hata hivyo katikati ya msimu aliondolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Mecky Maxime, aliyemaliza msimu, akaifikisha nafasi ya saba.
 
 8. Mashujaa FC
 
 Timu ya Mashujaa inaunda mtandao wa timu tano ambazo hazikuwagusa makocha wake msimu huu. Ilianza na Mohamed Abdallah 'Bares' na ikamaliza naye, japo ilianza kwa kusuasua muda mrefu wa ligi, lakini ikamaliza kwa kishindo ikiwa nafasi ya nane.
 
 9. Prisons
 
 Hadi msimu wa kwanza unamalizika, ilikuwa moja kati ya timu zilizokuwa hoi bin taaban, zikitabiriwa kushuka msimu uliomalizika. Ilichofanya, pamoja na usajili wa dirisha dogo, ikimtimua kocha wake, Fred Felix Minziro na kutwaa, Ahmad Ally. Ni kocha aliyefanya kazi kubwa na imeonyesha kwa kuimalika ikiwa kwa timu katika msimamo wa Ligi Kuu iliyomalizika.
 
 10. Kagera Sugar
 
 Hapa kulikuwa kama kuna mabadilishano ya makocha tu. Baada ya kuona mambo yanakwenda mrama, Kagera Sugar ikaachana na Maxime, ikamchukua Minziro ambaye alikuwa ameoshwa mlango wa kutokea na Prison.
 Wakati Mexime akienda Ihefu, Minziro alimaliza msimu akiwa na timu hiyo, akiwezesha kumaliza nafasi ya 10.
 
 11. Singida Fountain Gate
 
 Hii ndiyo timu iliyotia fora ya kutimua makocha wengi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/25. Imetimu makocha watano tofauti kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kufanya vibaya.

Ilianza na Mholanzi, Hans van Pluijim, ikamtimua, akaja Mjerumani, Ernst Middendorp ambaye hakukaa hata mwezi, kaingia Mbrazil Ricardo Heron Ferreira, naye pia hakukaa sana, kocha msaidizi Msauzi, Thabo Senong akashika usukani. Wala haikusaidia, naye akatimuliwa, Jamhuri Kihwelo akashika hatamu, yakamshinda, mwishoni akamalizia Ngawina Ngawina.
 
 12. Dodoma Jiji
 
 Ilimaliza nafasi ya 12, yenyewe ilitimua kocha mmoja, Melis Medo, ikamtwaa Mkenya, Francis Baraza ambaye alichukuwa jukumu hilo hadi mwisho.
 
 13. JKT Tanzania
 
 Timu hii inakamilisha timu tano ambazo hazikutimua kocha yoyote tangu mwanzo mwa ligi, ikiwamo Yanga, Azam, KMC na Mashujaa FC. Ilikuwa na Malale Hamsini, mwanzo hadi mwisho wa ligi.
 
 14. Tabora United
 
 Ilianza na kocha wa zamani wa Simba, Goran Kopunovic, lakini ikaachana naye, ikamtwaa, Mfaransa, Lauren Goevec, akawa mmoja wa makocha waliokaa muda mfupi zaidi, akaja Masoud Djuma akamalizia ligi, ikienda kwenye 'play off'. Hata hivyo ametimuliwa baada ya ligi kumalizika na hakwenda kwenye 'paly off', hivyo anahesabika kama alimaliza nayo kwani hakutimuliwa kabla kama wengine.
 
 15. Geita Gold
 
 Awali ilikuwa na Hemed Morocco, lakini baadaye hawakuelewana, akaondoka na kulewa Denis Kitambi ambaye alikuwa ametimuliwa kutoka Namungo. Matokeo ya yote ikashuka daraja. 
 
 16. Mtibwa Sugar
 
 Habib Kondo ndiye aliyeanza nayo ligi, lakini chombo kilipoonekana kwenda mrama, akachukuliwa Katwila ambaye alikuwa ametimuliwa Ihefu. Haikuwa dawa, tangu awali ilionekana kama itashuka daraja na kweli ikawa hivyo.