Leo ikitimu siku marufuku kuni na mkaa, utekelezaji kiza kinene

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 09:00 AM Jan 31 2025
taalam wa Misitu na Mazingira Dk. Felicia Kilahama,akifafanua jambo kuhusu marufuku ya matumizi ya kuni na mkaa.
PICHA ZOTE: BEATRECE MOSES
taalam wa Misitu na Mazingira Dk. Felicia Kilahama,akifafanua jambo kuhusu marufuku ya matumizi ya kuni na mkaa.

UTEKELEZAJI marufuku ya matumizi ya kuni na mkaa iliyotolewa na serikali kitaifa kwamba ifikapo Januari 31, 2025, iwe mwisho wa matumizi ya nishati hiyo. Huku ikiendeshwa kwa awamu.

Hiyo ni kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa taasisi zote za umma na binafsi nchini zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku, kusitisha utumiaji nishati hizo kwa tarehe hiyo.

Marufuku hiyo pia ikawahusu watu wenye taasisi zinazoandaa kwa ajili ya watu zaidi ya 300 kwa siku, mamalishe na babalishe wanatakiwa kusitisha ifikapo Januari 31, 2025, ambayo ni leo.

Kurejea tulikotoka, mnamo Juni Mosi 2021, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa tamko la Wiki ya Mazingira Duniani na kuzielekeza taasisi, mashirika ya serikali na sekta binafsi, zianze kutumia nishati rafiki wa mazingira badala ya kuni na mkaa. 

UTEKELEZAJI WAKE

Kuna juhudi zimefanywa, zikiwamo manispaa tofauti kusambaza matangazo ya kusisitiza marufuku hiyo, pamoja na kugawa na kukopesha majiko na mitungi ya gesi kwa baadhi ya mamalishe na babalishe waliosajiliwa kwenye masoko rasmi.

Baadhi ya mama na babalishe, wameeleza hawana uwezo kununua majiko ya gesi, kutokana na kushindwa kumudu gharama zake.

Majiko ya mkaa wanayotumia baadhi ya mamalishe na babalishe, katika Soko la Simu 2000 lililopo wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
Ofisa Mauzo wa kampuni moja inayouza gesi nchini, , Antony Martin, anasema kurahisisha utekelezaji wa matumizi ya nishati jadidifu, walitoa mkopo wa masharti nafuu wa majiko kwa baba na mama lishe. 

“Tuliwakopesha kwa shilingi laki moja na hamsini jiko la gesi lenye sehemu mbili za kupikia, lakini ulipaji wa fedha umekuwa na changamoto,” anasema Antony.  

Said Juma, muuza chipsi na ‘nyama choma’ Mwenge wilayani Kinondoni, ameonesha mshangao akihoji marufuku hiyo, akisema. 

“Sijui hiyo marufuku, sijui nitafanyaje maana mtaji wangu ni mdogo, kumudu kununua jiko la gesi ni mtihani kwangu, ngoja nisubiri tu itakavyokuwa.”

Asha Omari, mamalishe katika Kituo cha Mawasiliano Simu 2000, Dar es Salaam,  anasema alipewa jiko, lakini amelazimika kulipeleka nyumbani kwa kukosa usalama wa pa kupaweka.

“Tulipewa majiko watu kama 23 siku hiyo, lakini angalia mazingira yalivyo hapa siyo salama, nimelazimika kulihamishia nyumbani, hapa naendelea kupika kwa kutumia mkaa,” amesema Asha. 

Mariam Hemed maarufu ‘Mariam Mdigo’ anasema hana taarifa za kuwapo katazo la matumizi ya mkaa na kuni, pia hajapata jiko la gesi na mtaji wake ni mdogo.

Meneja Soko la Mawasiliano Simu 2000 Ahetwe Mkamba, anasema soko hilo lina mamalishe na babalishe 30 waliosajiliwa, baadhi yao tayari wamepewa majiko na mitungi ya gesi, kwa hatua za awali kuwawezesha kubadilika. 

Ofisa Habari wa Manispaa ya Ubungo, Joina Nzali, anasema wamegawa mitungi 1200 zilizotolewa na wadau, mitungi 800 imegawanywa kwa mamalishe na babalishe waliosajiliwa.

“Tumetoa tangazo kuwakumbusha kuhusu utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa mama na baba waliopo kwenye masoko ya manispaa yetu, tunaamini wamepata taarifa wameshajiandaa,” anasema Joina.

MTAALAMU MISITU 

Mtaalam wa Misitu na Mazingira Dk. Felician Kilahama, pia Mkurugenzi mstaafu wa Misitu na Nyuki, anasema: “Hili ni jambo ambalo tulipaswa kuanza kulitekeleza mapema, ili kulinda misitu na mazingira kwa ujumla. Kikwazo kilikuwa ni miundombinu jinsi ya kufanikisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika.”

Anatahadharisha, upatikanaji nishati ukiwa wa gharama, wakati kipato cha wananchi kipo chini, utekelezaji mabadiliko itakuwa vigumu. 

“Kuwe na ruzuku kama ikiwezekana, pia kuwe na uhakika wa kupatikana hiyo gesi, je ni ya asili hapa nchini au inaagizwa kutoka nje, hayo ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa...” anasema. 

Dk. Kilahama anafafanua changamoto ya utekelezaji ni jambo la wazi, kutokana na uhalisia wa mfumo wa maisha umezoeleka kama vile kupalia mkaa kwenye wali, inabidi kuwa makini na usimamizi wa misitu. 

Katika andiko la Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) lililochapishwa Mei mwaka jana kwenye tovuti, inabainisha nishati na teknolojia sahihi inayotakiwa. 

Nishati zinazopendekezwa zinatajwa kuwa zenye kiwango kidogo cha sumu, zinapotumika kwa usahihi, lengo ni kuhakikisha usalama uendelevu na upatikanaji rahisi wa nishati ya kupikia.

Hapo inatajwa kuokoa muda, kupunguza gharama, athari za kimazingira na kiafya kwa watumiaji, pia nyenzo muhimu  kutekeleza makubaliano ya kitaifa na kimataifa kufikia mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji gesi joto. 

Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unatokana na hitaji la kuwa na mpango jumuishi kitaifa, kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya, kiuchumi na kijamii, zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.

 “Kutokana na suala la nishati ya kupikia kuwa mtambuka, kumekuwa na changamoto ya utekelezaji wa mikakati ya kupunguza athari hizo. 

“Tangu Tanzania ipate uhuru Mwaka 1961, haijawahi kuwa na mpango jumuishi wa kitaifa wa kupunguza matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia,” inaelezwa. 

PICHA KITAIFA

Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 inataja azma ya kuongeza matumizi ya nishati tungamotaka na teknolojia yenye ufanisi kupikia, kuepuka uharibifu wa mazingira na matatizo ya kiafya yatokanayo na moshi.

 Ni mkakati ulioandaliwa kutekeleza Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015. Inayonuia kuboresha matumizi ya nishati za kisasa za kupikia.

Pia, kuna matamko kitaifa kama:Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998 yenye lengo la kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mazao, na huduma za misitu kwa kudumishwa  eneo la kutosha chini ya usimamizi madhubuti.

Pia, Sera ya Taifa ya Afya ya Mwaka 2007 inaelekeza utaratibu bora na endelevu wa kuhifadhi, kutunza na kulinda mazingira kwa faida ya afya ya wanachi na vizazi vijavyo;

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Mwanamke na Jinsia ya Mwaka 2000, nayo inalenga kutunza mazingira kwa kumpunguzia mwanamke mzigo wa kutafuta kuni na maji, ili kuwezesha kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi. 

Kupitia uzoefu wa nchini India, sekta binafsi inashirikishwa kusambaza gesi asilia, serikali yake ikigawa maeneo maalumu kwa sekta hiyo kufanya usambazaji.

 Vilevile, programu za kutoa ruzuku katika nishati safi ya kupikia kwa kaya za vipato vya chini, ni uzoefu uliochukuliwa, sasa serikali nchini imeandaa programu yenye lengo la kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hiyo inaendana na kuanzishwa viwanda vya bayogesi, kuwezesha kuzalisha nishati safi ya kupikia nchini.

Takwimu za Benki ya Dunia za Mwaka 2023, inawataja Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia inaongezeka kiwango, kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi asilimia 6.9 mwaka 2021. 

Inaelezwa, kiwango hicho kiko chini ya wastani cha dunia, asilimia 71 kwa Mwaka 2021.

Mbali na gesi, nishati zingine zinazotumika kupikia nchini ni pamoja na kinyesi cha wanyama na mabaki ya mimea, kuni, mkaa, mafuta ya taa, mkaa mbadala, bayoethano, LPG, gesi asilia, bayogesi, umeme, majiko banifu na majiko ya nishati ya jua. 

 Kwa mujibu wa mkakati uitwao Cooking Energy Action Plan ya Mwaka 2022, asilimia 82 ya nishati kuu inayotumika nchini inatokana na tungamotaka (biomass).

Kwenye mapishi, asilimia 90 ya kaya nchini hutumia nishati kuni na mkaa kama nishati kuu ya kupikia ambapo matumizi ya kuni ni asilimia 63.5 na mkaa ni asilimia 26.2. 

Asilimia 10 zilizobaki zinajumuisha asilimia 5.1 za LPG, asilimia 3 za umeme na asilimia 2.2 za nishati nyingine. 

Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa Mwaka 2017/18, nishati ya kuni yamekithiri hasa maeneo ya vijijini ambako asilimia 84.8 ya kaya hutumia nishati hiyo ikilinganishwa na maeneo ya mijini ambapo matumizi ni asilimia 17.4.