Kukariri nadharia pekee hakutoshi wajue udereva

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:12 AM Dec 31 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, akiwa na baadhi ya vijana wanaokwenda kufanyakazi nje ya nchi kwa mfumo wa utarajali
Picha: Restuta James
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, akiwa na baadhi ya vijana wanaokwenda kufanyakazi nje ya nchi kwa mfumo wa utarajali

ELIMU ya darasani pekee haitoshi kumletea mafanikio mhitimu wa chuo kikuu, anahitaji vitu vingine hasa nidhamu ya muda na kazi, ujuzi wa ziada, uthubutu na ubunifu ambavyo ni nyenzo muhimu katika ulimwengu wa ajira.

Utafiti wa mashirika ya elimu mara kadhaa unabaini kuwa upungufu uliopo kwa baadhi ya watoto wanaohitimu elimu ya msingi hasa kutojua kusoma kwa ufasaha na kuhesabu, vyuoni hali ni tofauti, wahitimu wanakosa ujuzi mdogo ambao ungewawezesha kuogolea kwenye soko la ajira.

Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Ushirika cha Wajasiriamali Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUGECO), Revocatus Kimario, anasema moja ya pengo lililopo kwa wahitimu wa vyuo vikuu ni kutokuwa na uwezo wa kupambanua mambo hasa kutatua changamoto ndogo zinazowazunguka.

Ni ujumbe unaosikika wakati wa kuwaaga wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo ya utarajali katika mataifa mbalimbali.

Anasema vijana hawajui lugha za kimataifa, udereva, elimu ya fedha na ujasiriamali, ujuzi ambao anasema unatanua fursa zao kuajiriwa na kujiajiri.

 “Kuna mapengo mengi na hili nimelisema mara nyingi. Vijana hawa hawana uthubutu na uwezo wa kufanya tathmini. Kuna utafiti umetoka karibuni unaonesha kwamba asilimia 69 ya wahitimu hawana uwezo wa kuchambua kitu. Hili ni tatizo kubwa mno,” anasema.

Kimario anaeleza kuwa baada ya kuona pengo hilo, ushirika huo ambao unapeleka mamia ya vijana kwenye ajira za muda mfupi nje ya nchi, unawapa ujuzi huo wa kuchambua.

“Tumesema lazima tuwafundishe biashara ili waifahamu na waweze kuona fursa na kuitumia elimu yao ya chuo kikuu kujiajiri na wengine kuajiriwa, ujasiriamali, elimu ya fedha na kuwapa nafasi ya kutekeleza kile wanachokijua. La tatu na kubwa zaidi ni hizi programu za utarajali (internship), ili wakienda nje ya nchi wapate maarifa ya teknolojia na utendaji kwa ujumla,” anasema Kimario.

Anasema vijana wengi wanaopata fursa ya kufanyakazi nje ya nchi na wa sekta za kilimo na mifugo, wakiwamo madaktari wa mifugo, sayansi ya mimea na chakula, teknolojia na utalii, kilimo cha bustani na madawa, ambao wanalazimika pia kujua lugha za kigeni.

Kimario anatoa mfano kwamba mwaka jana, vijana 360 walishindwa kwenda Ujerumani kwa kuwa hawajui Kijerumani.

“Shida siyo maarifa. Wanakosa yale ya ziada yanayohitajika. Viwanda vya wenzetu vinatumia mashine za kisasa zilizo kwenye lugha ya Kijerumani. Wanahitaji wanaojua walau ngazi ya kwanza ya lugha hiyo,” anasema.

Anaongeza: “Wanakwenda kuongeza maarifa, kuiona dunia na namna watu wengine wanavyofanya kazi na kutengeneza kipato. Tunawaambia unakwenda, ‘unakopi, unaediti na unapest’.”

Akimaanisha 

Kimario anashauri kwamba vyuo vikuu viongeze masomo ya ziada hasa ya lugha ili wanafunzi wapate urahisi wa kujifunza.

“Tukibaki tu na Kiswahili chetu tunabaki hapa ndani wakati sisi tunataka tuende huko duniani tukapanue uwezo wa vijana wetu. Ningetamani vyuo viwe na maabara za lugha au language lab,” anasema Kimario.

Pengo la lugha linaungwa mkono na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ambaye anasema ni muhimu vijana wakajua lugha za kimataifa bila kujali kozi mahsusi anayosoma chuoni.

“Nataka nieleze hili kwa masikitiko makubwa sana. Zimewahi kutoka nafasi za madereva wanaotakiwa kwenda kufanya kazi katika nchi za Ghuba mataifa ya Kiarabu, ambazo wengi walijitokeza lakini walichukuliwa wachache kwa sababu ya kutojua lugha ya Kiarabu. Tutaendelea kushirikiana na wadau ili kuona kama vyuo vinaweza kutenga muda wa ziada kwa ajili ya lugha,” anasema.

Kimario anasema wanafunzi wanaopata fursa hizo ni wa vyuo vikuu na wale wa vyuo vya kati, ambapo kwa mwaka jana vijana 535 wamekwenda Ujerumani, Norway, Denmark na Sweden.

Anasema lengo hilo ni kutengeneza watu wenye ujuzi wa kutosha katika sekta ya kilimo na mifugo, ukiwamo usindakaji wa vyakula kama nyama na maziwa.

“Wanakwenda kwenye teknolojia nyingi ambazo zimetuzidi, wanapata ujuzi na kipato. Kwa wastani hawa wanaokwenda wanapata Yuro  2,500 hadi 3,000 kwa mwezi ambazo ni karibu Sh. milioni sita mpaka tisa. Wakiwa na nidhamu ya fedha, ndani ya mwaka mmoja na nusu wanaokaa kule, wanaweza  kupata mtaji wa  kujiajiri hapa nyumbani ,” anaeleza.

Anasema elimu ya fedha waliyopewa inawawezesha kufungua akaunti ya diyaspora ili waweze kutunza fedha  kwenye benki za ndani na hivyo kuiwezesha nchi kuwa na fedha za kigeni.

Anasema taarifa ya fedha ya mwaka jana, inaonesha kwamba kwenye ajira (remittance), kulikuwa na mzunguko wa dola za Marekani bilioni 625 duniani, ambazo dola bilioni bilioni 125, zilikwenda India na Afrika Mashariki, Kenya iliingiza  bilioni 4.1, ambazo zilirudi nchini humo kupitia Wakenya wanaofanya kazi nje.

“Kwenye data hizo, nchi yetu ilipata dola bilioni 0.316, naamini tukishirikiana na benki tunaweza kupata mzunguko mkubwa wa fedha za kigeni. Tunaweza kupata remittance kubwa kama vijana wetu watatumia vizuri muda wao wa ziada vyuoni, kupata ujuzi wa ziada ili waweze kufanya kazi nje na nchi kuweka mifumo sahihi ya kuwawezesha,” anasema.

Anatoa rai kwa serikali  kuwatambua vijana waliopata mafunzo hayo na kuandaa mpango wa baada ya utarajali nje ya nchi.

Anasema SUGECO inashirikiana na Taasisi ya CRDB, kuwawezesha kimtaji, waliomaliza utarajali nje ya nchi.

“Zaidi ya vijana 40 wamewezeshwa kwa kupewa mtaji unaozidi Sh. milioni 460 ndani ya mwaka mmoja na biashara zao zinafanya vizuri. Tuna nafasi zaidi ya 1,500 za vijana kwa mwaka. Tunaamini tunaweza kutengeneza biashara nyingi zaidi, tutaongeza mzunguko wa fedha za kigeni kupitia akaunti ya diaspora na kutengeneza rasilimali watu yenye ujuzi mkubwa,” anasema.

Anasisistiza umuhimu wa vijana kujifunza walau lugha mbili za kimataifa, bila kujali kozi anayosoma chuoni, kwa kuwa ni nyenzo ya mawasiliano kwa wale wanaofikiria kwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Kimario anatoa mfano kwamba amekuwa akipeleka wanafunzi na wahitimu wa vyuo vikuu kufanyakazi katika nchi za Ulaya na Marekani na changamoto kubwa inayomkabili ni wahitimu kutojua lugha na kushindwa kuendesha gari.

Kwa mujibu wa Kimario, nchi ambazo ushirika huo unapeleka wafanyakazi ni Ujerumani, Denmark, Marekani, Uholanzi, Sweden, Norway na Israel.

Anasema mwaka jana SUGECO ilipeleka vijana 500, lakini zaidi ya nafasi 300 zilipotea kutokana na wahitimu hao kutojua Kijerumani.

Waziri Ridhiwani akiwafunda vijana hao kuwa weledi na bidii ya kazi, wanapokuwa nje ya nchi kuwaongezea fursa vijana wengine kupata mafunzo hayo.

Anawataka vijana kujiepusha na uhalifu ili wasiharibu taswira ya Tanzania ughaibuni.

“Serikali itashirikiana na SUGECO kuandaa mpango wa baada ya utarajali, ili vijana hawa waweze kutumia mafunzo waliyoyapata katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu,” anasema.

Anasema maandalizi ya rasilimali watu wenye ujuzi, yanahitaji ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi mbalimbali.

Mhitimu wa SUA, Harold Mulugu, ambaye amepata fursa ya kwenda Ujerumani, anasema amelazimika kujifunza Kijerumani kwa kuwa ni moja ya kigezo cha kufanya kazi nchini humo.

Levina Kiwango ambaye amehitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kozi ya sayansi ya chakula na teknolojia, anasema amelazimika kujifunza Kijerumani baada ya kubaini kwamba ili kufikia soko la ajira nchini humo, inahitaji ajue lugha hiyo.