Kujibu matusi kwenye mitihani kunavyozidi kuwa fedheha

By Dk. Felician Kilahama , Nipashe
Published at 08:30 AM Feb 11 2025
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed
Picha: Mtandao
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed

BADO tunaendelea kutafakari mitihani ya kuhitimu kidato cha nne, inayofanyika Novemba mwaka jana na matokeo yake kutangazwa mwezi uliopita na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), ambayo yanafurahisha na pia kushangaza.

Matokeo yanaonyesha kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia tatu, watahiniwa wengi wamefaulu na kwamba kati ya wanafunzi 516,695, idadi kubwa ambao ni 477,262 wamefaulu kwa madaraja ya I, II, III na IV.

NECTA inasema ni ufaulu wa asilimia 92.37 ukilinganishwa na matokeo ya mitihani ya 2023 yenye ufaulu wa asilimia 89.36. Kadhalika, ufaulu kwa madaraja ya I, II na III ni watahiniwa 221,952 sawa na asilimia 43 wakati 2023 walikuwa watahiniwa 197,426 sawa na asilimia 37.4.  

Vilevile, matokeo yameonyesha kuwa waliopata daraja la nne pamoja na sufuri wamepungua kulinganisha na matokeo ya 2023, hivyo kuashiria ongezeko la asilimia 5.6 kwenye ubora wa kufaulu. 

Hata hivyo, NECTA inabainisha kuwa kwa matokeo ya 2024, watahiniwa 67 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu wakati wakifanya mitihani.

Pamoja na hao pia wamo watahiniwa watano wajuaji walioandika matusi kwenye karatasi za mitihani. Taarifa ya NECTA ikihitishwa kwa kuonyesha kuwa watahiniwa 459, hawakufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kiafya.

Kinachosikitisha ni vitendo viovu kwa baadhi ya watahiniwa kuandika matusi eti ndiyo majibu kwa maswali waliyotakiwa kuyajibu.

Mwanafunzi humaanisha mtu anayejifunza kwa kukaa darasani akafundishwa na wataalamu wa masomo ambao, rasmi tunawafahamu kuwa ni mwalimu au waalimu.

Wakati wa kufanya mitihani unapowadia, lengo kuu, huwa ni kupima ufahamu au uelewa wa wanafunzi kwa kuzingatia waliyojifunza kama ni miaka miwili  au  minne  inawezekana ikawa miaka pungufu au zaidi kutokana na mitaala husika. 

Binadamu anayefundishwa huitwa mwanafunzi au wanafunzi, wakati wa kufanya mitihani huitwa mtahiniwa au watahiniwa. Kufuatana na kanuni za mitihani kila kituo chenye watahiniwa huwekwa msimamizi (invigilator) aliyeteuliwa rasmi kusimamia na kuhakikisha mitihani inafanyika kwa utulivu, haki na amani bila udanganyifu kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa. 

 Taarifa za watahiniwa kuandika matusi zinasikika kila mara na mwaka huu wa kidato cha nne walioandika matusi kwenye karatasi za mitihani. Tunajiuliza inakuwaje miaka minne darasani ndicho walichojifunza? 

Au ni kutokana na changamoto za afya ya akili au kukengeuka? Iwapo ni binadamu wenye utashi, akili timamu na maarifa, kuandika matusi eti ndiyo majibu ya mitihani waliyoifanya ni fedheha kubwa kwa taifa. Inabidi lipigwe vita.

 Hata hivyo, siyo mara ya kwanza kusikia watahiniwa wakitumia lugha chafu kwenye karatasi za mitihani. 

Inapotokea hali hiyo isiyopendeza, viongozi tusifumbie macho vitendo kama hivyo maana ni kudhalilisha utu wa binadamu.

Kwa muktadha kama huo, wanafunzi hao watano wakibainika kuwa walifanya hivyo kwa utashi wao uliosheheni ujinga wasiachwe bali adhabu kali zitolewe ili iwe fundisho kwa wengine ikizingatiwa kuwa ni mambo yanayotokea mara kwa mara.

Miaka ya 2017 na 2018, nilitembelea maeneo kadhaa ya mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na kufika kwenye vijiji na vitongoji kadhaa zaidi ya 10 pamoja na shule za msingi.

Katika mazungumzo na walimu juu ya ufaulu wa watahiniwa wa darasa la saba hali ikaonekana siyo wa kuridhisha, nikataka kufahamu sababu za kutofanya vizuri.

 Iwapo walimu wapo, miundombinu bora  madarasa, vyoo, nyumba za walimu, maji na chakula kwa kiwango cha kuridhisha hivyo, kuwepo mazingira wezeshi kiasi cha wanafunzi kufundishwa wakiwa na utulivu na amani na kuelewa anachojifunza changamoto gani wamekumbana nazo? 

Walimu wakajibu wapo wanafunzi waliokuwa bora darasani na waliotarajiwa, kwa namna yoyote ile, wakifanya mitihani watafaulu na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, lakini hali ilikuwa kunyume chake.

Wanajibu kuwa walikumbana na hali iliyowashangaza  maana sababu watahiniwa waliokuwa wanategemewa kufanya vizuri wakafanya vibaya. 

Wanapowadadisi wahusika ili kuelewa kilichojiri kiasi cha kutochaguliwa kuendelea na masomo zaidi, wakagundua kuwa kikwazo ni wazazi na walezi wao. 

Kwa mazingira ya maendeleo ya sasa na dunia ya  kidijitali inakuwa vigumu kuamini kuwa wazazi na walezi wanakuwa kizingiti cha aina yake kwa vijana wao kuendelea na masomo, wazazi kama hao wanahitaji sana rehema zake Mungu.

Kadhalika, walimu wanafafanua kwa kusema kuwa watahiniwa wanaagizwa   wafeli mitihani kwa kujibu ovyo ovyo tu, wasiandike majibu sahihi.

 Vijana hao kwa kutii sauti za wazazi na walezi wanatekeleza na mchezo ukaishia hapo, wakafeli kwa kujitakia. 

Katika karne hii ya kujiletea maendelea, na kwa kuwa tunaamini kwamba elimu ndiyo  ufunguo wa maisha na kwa kuwa taifa linakazania watoto wote wa Tanzania wasome na kupata elimu kadri itakavyowezekana.

Kwa ufahamu na uelewa hadi kushinda mitihani vizuri na kusonga mbele kielimu, kiakili na maarifa, bado wanajitokeza wazazi wenye roho za ajabu kiasi cha kufurahia watoto wao kubaki duni kama wao walivyokuwa ni hali hatarishi kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya taifa na watu wake.

Huu ni wakati wa viongozi, kwa ngazi zote, tangu vijijini hadi taifa kuchukua hatua za msingi kuhakikisha masuala hayo yenye sura anayoaibisha  zinakomeshwa. 

 Watahiniwa watano waliojibu matusi kwenye karatazi za mitihani, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. 

Napendekeza yafuatayo, mosi Baraza la Mitihani Tanzania lisiishie tu kufuta matokeo bali hatua zaidi zichukuliwe maana wanafunzi walioandika matusi wanafahamika pamoja na shule walizotoka.

Hivyo watafutwe na hatua za kisheria zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuwapima afya ya akili kupitia wataalamu wenye ujuzi huo. Pili, shule wanazotoka pia zifuatiliwe kubaini ilikuwaje wanafunzi wakawa na ujasiri kiasi hicho wa kuandika na kutukana badala ya kujibu  mitihani.

Wakumbuke shule zinagharamiwa na fedha za walipakodi na ndiyo wanaowasomesha. Huenda kuna utovu na ukosefu wa nidhamu na wa maadili wa hali ya juu.

 Tatu, kuwepo na mkakati kitaifa, kukomesha tabia hiyo inayoripotiwa mara kwa mara. Wahakikishe haijitokezi tena kwa kuweka mkazo elimu ya malezi bora na maadili mema kwa katika shule zote pamoja na wananchi wote.