‘Wazazi, njaa shuleni, lugha visiki ufaulu’

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 04:23 PM Feb 11 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akisisitiza jambo katika mkutano wa wadau wa sekta ya elimu Wilayani Temeke
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akisisitiza jambo katika mkutano wa wadau wa sekta ya elimu Wilayani Temeke

USHIRIKIANO duni kutoka kwa wazazi, kushinda njaa shuleni kwa muda mrefu, lugha ya kufundishia, umbali mrefu hadi shule na makazi, vinatajwa kuwa visiki katika kuondoa sifuri darasani.

Ofisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Temeke, Mwanaidi Torroka, amesema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowakutanisha wadau wa elimu, wakiwamo wakuu wa shule, maofisa elimu kutoka halmashauri ya Temeke

Amesema upungufu wa walimu wa mchepuo wa sayansi  na ukosefu wa maabara mwa changamoto zinazoshusha ufaulu, kwa wanafunzi wa shule za sekondari manispaa ya Temeke.

Kadhalika, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Gift Kyando, aliongezea sababu zingine kuwa ni pamoja na hali duni za vipato za wazazi, changamoto ya usafiri wanafunzi wanaosoma mbali na shuleni, kuachwa vituoni na mabasi ya abiria ya umma.

Ufaulu duni, sababu zatajwa
“Lugha ya kiingereza ya kufundishia ni moja ya changamoto kubwa ya watoto kupata ufaulu hafifu kwenye mitihani yao, malezi ya upande mmoja (singleparent), hiyo ni changamoto inayopelekea ufinyu wa ufaulu,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewaagiza wakuu wa shule, wenyeviti wa bodi za shule, viongozi na wataalamu wa elimu, kuangalia kwa mapana zaidi miundombinu ya elimu, ili kukabiliana na kuondoa ufaulu duni na kuondokana na sifuri sekondari.

Amewataka wadau hao kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa kila mdau wa elimu na kushirikisha wazazi kujadili kwa pamoja nini kifanyike kuondoa sifuri na kuinua viwango vya ufaulu kwa wanafunzi.

“Fanyeni utafiti wa kina badala ya kutazama sababu chache zinazotolewa na kuonekana kusababisha ufaulu duni, fanyeni utafiti wa kina na washirikisheni wazazi, ili tupate mwarobaini wa hili,” RC Chalamila.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alisema katika kukabiliana changamoto ya ufaulu ndani ya manispaa hiyo, Baraza la Halmashauri lishapitisha bajeti ya kuajiri walimu 200 wa mchepuo wa sayansi na hesabu.

“Pia tunapokea walimu wa kujitolea wa mchepuo wa sayansi ambao ni wachache sana, waje katika halmashauri yetu tutawapokea na kuwawangalia, ili watusaidie kukabiliana na ufaulu hafifu,” alisema Mapunda.