Kifungu kilichomng'oa Malisa CCM hiki hapa

By Enock Charles , Nipashe
Published at 04:45 PM Feb 11 2025
Dk. Godfrey Malisa
Picha: Mtandao
Dk. Godfrey Malisa

JANA Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kilimanjaro, kilitangaza kumfukuza uanachama, Dk. Godfrey Malisa, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoa matamko ambayo yanadaiwa kuvuruga umoja ndani ya chama hicho.

Dk.  Malisa amepinga hadharani kupitishwa kwa mgombea wa urais wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu Dk. Samia Suluhu Hassan katika mkutano mkuu, uliofanyika mwezi uliopita akieleza kwamba alipaswa kushindanishwa na wengine.

Hata hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 100 ibara ya 5(b) cha Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 toleo la Mwaka 2017, Mkutano Mkuu unayo mamlaka ya kupitisha jina moja la mwanachama atakayesimama kama mgombea wa urais. 

Pia kwa mujibu wa katiba hiyo Mkutano Mkuu ndiyo wenye mamlaka ya mwisho kabisa.  

Dk. Malisa si wa kwanza kufukuzwa katika chama hicho, kwa kupingana na uamuzi wa chama hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu. 

Mwaka 2020 marehemu Bernard Membe, alifukuzwa baada ya kutaka kuwania urais dhidi ya Rais wa wakati huo, hayati Dk. John Magufuli.

Akitangaza uamuzi baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya chama Mkoa, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel, alisema kikao hicho kimemfukuza uanachama kada huyo, kwa kubeza uamuzi wa chama mara kwa mara, hivyo kukosa sifa kuendelea kuwa mwanachama.

“Kwa mujibu wa kanuni za maadili za chama chetu kifungu cha 6 kifungu kidogo cha tatu (b) kinasema mwanachama atakayekataa maamuzi halali ya chama atakuwa ametenda kosa la utovu wa nidhamu na ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni”. Alisema.

Katika Mkutano Mkuu wa CCM wa Januari 19, Mwaka huu, ulimpitisha Dk. Samia, kuwa mgombea urais wa Tanzania, huku Dk. Hussein Mwinyi. akipitishwa kugombea Zanzibar.