Kitete Afrika Trump anaposhika hatamu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:10 AM Jan 22 2025
Rais wa Marekani, Donald Trump
Picha: Mtandao
Rais wa Marekani, Donald Trump

DONALD Trump amekula kiapo na sasa ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Marekani kwa awamu ya pili.

Wakati anaingia White House Afrika inajitafuta kufahamu hatima yake wakihofia itakuwaje? Utawala huo mpya wa Trump utakuwa na manufaa kwa bara lao?

Itakumbukwa kuwa wakati wa uongozi wake wa awamu ya kwanza anadaiwa kuwa aliipuuza Afrika na kuna wakati alisema Afrika ni wavivu, wasiojituma na kwamba itapendeza kama watatawaliwa tena kwa miongo mingine na kuongeza kuwa ni ‘shithole’

‘Shithole’ si shimo la kinyesi kama ambavyo Watanzania wengi wangetafsiri, maana halisi ni kwamba ni kitu kilicho katika hali mbaya, kibovu, kilichokosa matunzo kilicho taabani kwa ubovu na kukosa uangalizi.

Rais Trump hakufanya ajizi, aliupunguza baadhi ya fedha za miradi ya ufadhili, kuwazuia na kuwakomesha wahamiaji kuingia Amerika na kulaumu kuwa wanapaswa kujitahidi kujiletea maendeleo.

Kwa ujumla Trump anachosema ni kuitaka Afrika iamke na kuachana na ‘uombaomba’ lakini pia ikitumia vibaya fedha za maendeleo inayopewa. Afrika ina karibu wastani wa miongo sita ya uhuru lakini kiwango cha maendeleo ni kidogo mno licha ya kuelemewa na deni kubwa kutokana na mikopo iliyochukuliwa kwenye taasisi za fedha, hazina za nchi mbalimbali na hata mashirika ya maendeleo.

Kama ilivyokuwa kwa utawala wa Joseph Biden, wa Democrat Marekani ambaye aliiweka Afrika kuwa kwenye washirika muhimu wa Marekani, Trump kipaumbele chake ni ‘Amerika kwanza’ au Make ‘America Great Again’.

Kwa mujibu wa BBC mwaka 2023, Marekani ilieleza kuwekeza zaidi ya Dola bilioni 22 (Sh. Trilioni 55.3) tangu Biden aingie madarakani na kwamba kuna wasiwasi kuwa Trump anaweza kuondoa uwekezaji na biashara hiyo.

 Rais wa hivi karibuni ana mtazamo wa kulinda zaidi maslahi ya nchi yake, usio wa kawaida kuliko Biden moja ya kauli mbiu za muhula wake wa kwanza ilikuwa "Amerika Kwanza".

Mkataba wa Ukuaji na Fursa ya Afŕika (AGOA), ambao umewezesha nchi za Afŕika kuuza nje baadhi ya mazao yao kwenda Maŕekani bila kulipa kodi tangu mwaka 2000, ni chanzo kikuu cha wasiwasi kuwa kitaondoka.

Mkataba wa Ukuaji na Fursa ya Afŕika (AGOA)
Mkataba wa AGOA, utawala wa Trump hakuupenda alisema hautaongezwa muda wakati utakapoisha mwaka huu 2025.

Na wakati wa kampeni yake mwaka jana  aliahidi  kuongeza  ushuru wa mapato wa asilimia 10  kwa bidhaa zote zinazotoka nje. Hii itafanya bidhaa zikiwamo za AGOA kutozwa ushuru na kuwa  ghali zaidi, na hivyo wafanyabiashara wa Afrika watakuwa wamefungiwa nje kuuza kwenye soko kubwa la Marekani. Yote hayo yataiathiri Afrika.

UKANDA WA LOBITO

Mradi wa Lobito Corridor,  ni uwekezaji mkubwa wa miundombinu wa nchi za Afrika na Marekani ambazo ni Marekani, Angola, DRC  na Zambia na Tanzania kwa upande mwingine.Ndicho kitu kikubwa ambacho Marekani ya Biden ilidhamiria kuuendeleza. Sehemu muhimu ya mradi huo ni kuunganisha huduma ya reli kati ya nchi hizo tatu na Bandari ya Lobito iliyoko Angola kwenye ufukwe wa Bahari ya  Atlantic Angola.

Lengo la mradi huo umekuwa sehemu kuu ya Sera ya Ushirikiano ya  Marekani na Afrika katika miaka ya hivi karibuni.Lobito Coridor inatarajiwa kuenea hadi Tanzania katika siku zijazo ili kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam  na ya Lobito. Mpango huo unahusisha kusahihisha njia za reli zilizopo na kujenga kilomita 800 za njia mpya, hasa nchini Zambia.

Malengo ya Lobito  ni pamoja na kukuza maendeleo ya uchumi wa ndani na ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda lakini kubwa zaidi ni Marekani kupata madini muhimu ya kimkakati (critical minerals)  yanayohitajika sasa kutengeneza bidhaa za kielektroniki na kufanikisha maendeleo ya teknolojia ya kidijitali na kulinda mazingira.Kwa umuhimu zaidi Marekani inataka kubadilisha mnyororo wake muhimu ya kupata madini hayo na kuachana na utegemezi wa China  ili kujipatia shaba, kobalt, nikeli  na madini mengine muhimu kwa uchumi wa Marekani na msingi wa mali ghafi za viwanda vya usalama na ulinzi vya nchi hiyo. 

MADINI YA KIMKAKATI

Madini muhimu au ya kimkakati ni  shaba, lithiamu, nikeli, kobalti na Rare Earth Elements  ambao ni mchango wa madini mbalimbali. Madini hayo ni muhimu katika teknolojia nyingi za kielektroniki na kwenye kuunda mitambo ya kuzalisha nishati safi. Madini hayo hutengeneza ‘paneli’ za umeme jua na  upepo, simu, ndege  hadi betrii za magari ya umeme na mnyororo wa thamani.

Kwa ujumla  kusaidia miundombinu ya Afrika kama reli na  barabara haijawahi kuwa kipaumbele cha Marekani licha ya kwamba  Shirika la Changamoto za Milenia (MCA) limefadhili miradi ya barabara na  umeme lakini kwa Lobito ndiyo mara ya kwanza kuanzisha ushiriki mkubwa zaidi wa  miundombinu barani Afrika, Trump akiuzima itakuwa jambo la kuhuzunisha.

Sio tu mradi wa reli ni zaidi kwa sababu unahusisha kuunganisha nchi za Ushirikiano wa Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) kidijitali, kuongeza urahisi wa usafirishaji wa watu na shehena, kujenga viwanda na kuongeza ajira kwa vijana hasa kwenye kuchimba madini ya kimkakati na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ukanda huo, kuendeleza kilimo, ufugaji na kuimarisha mnyororo wa thamani.

Ni wazi kuwa kuboresha reli kunahitajika nchini DRC, Angola, Zambia na Tanzania 

BBC inasema kuwa ingawa Trump hakutaka AGOA, na tena ameahidi kuongeza kodi bidhaa za kigeni anakabiliana na ushawishi wa kiuchumi wa China,  Afrika, ambao ni mkubwa hivyo analazimika  kudumisha ushirikiano.

Mwaka 2018 utawala wa Trump ulizindua Prosper Africa mpango ambao unaowezesha kampuni za Marekani zinazotaka kuwekeza Afrika na Shirika la Fedha la Maendeleo (DFC), ambalo linafadhili miradi ya maendeleo Afrika na duniani kote. 

Biden aliendelea kuuendesha baada ya kuchukua wadhifa wake na DFC inasema hadi sasa imewekeza zaidi ya Dola bilioni 22 (Sh. Trilion 55.3). Ikizingatiwa kuwa China bado ina nguvu kubwa barani Afrika na kwamba Trump alianzisha sera hizo mwenyewe, kuna uwezekano mkubwa wa kutafakari zaidi kabla ya kuziondoa.