Kinana anawageuzia kibao, kuwasuta wanaokoromea viongozi hadharani

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:38 AM Apr 24 2024
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana, akizungumza na wana CCM wa Mkoa wa  Mara.
Picha: Maulid Mmbaga
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana, akizungumza na wana CCM wa Mkoa wa Mara.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana, anawakumbusha wana-CCM, kuwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025,umoja na mshikamano katika utendaji kazi ni muhimu na kwamba tofauti miongoni mwao zitawarudisha nyuma badala ya kuwapeleka mbele.

Anawaambia:"Ukiona mtu anafanya vitu ambavyo si sawa hayo ni yake, pia tunaelekea kwenye uchaguzi ili tushinde viongozi lazima mtende haki tusimpendelee mtu, tusipandikize watu wala kupokea rushwa kwani ni adui wa maendeleo na malengo yetu."

Anatoa angalizo hilo ,mkoani Mara kwenye ziara iliyolenga kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM, akieleza kwamba endapo mifumo  ya ndani ya chama itafanya kazi kikamilifu wataendelea kuwa na nguvu, kuaminika na kukubalika na umma.  

Anasema chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata katiba, na kwamba kina kanuni kwa kila jambo ikiwamo uchaguzi, maadili na utumishi, akisisitiza kuwa ndani ya CCM kila kitu kinaangaliwa na kinaandikwa kwa utaratibu maalum.

AWATETEA VIONGOZI

Anawakemea baadhi ya viongozi wa CCM kuwadhalilisha watendaji wa halmashauri hadharani akieleza kuwa kama wana jambo wawaeleze madiwani, wenyekiti wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wabunge, kwakuwa viongozi hao wanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni za utumishi.

Anawasifu wakurugenzi kuwa wanafanya kazi nzuri na wanapolaumiwa wanabaki kusononeka kwa sababu hawana pakusemea, akisisitiza kwamba wanastahili kupewa heshima zao kama binadamu na watumishi kulingana na kazi wanazofanya.

Kinana anashauri inapobainika wakurugenzi hao wamekosea hawapaswi kuparamiwa kwenye mikutano ya hadhara bali mifumo ya kiutumishi inapaswa kuzingatiwa katika kuwawajibisha na si utaratibu unaotumika wa kuwasema hadharani.

“Usisimame kwenye mkutano wa hadhara ukaanza kumdhalilisha mtendaji wa serikali ambaye ni sehemu ya serikali ya CCM kwa jambo ambalo hata huna ushahidi au ni uzushi. Serikalini kuna utaratibu. Njia ya mawasiliano kati ya chama na halmashauri ni kupitia wenyeviti na wakuu wa wilaya.

“Wanastahili heshima …Siajabu wakati mwingine mambo unayoyaagiza kwenye kanuni hayakoe watakusikiliza, watarudi nyumbani na kuendelea kufanya shughuli zao nyingine,” anasema Kinana.

“Mnapokwenda kukagua miradi msianze tena kutoa kauli za kukashifu watu, ukiona kuna mapungufu mahali, muulize mkuu wa wilaya au mwenyekiti wa halmashauri, nao watamtafuta mkurugenzi watazungumza naye, lakini ukiitaja halmashauri wakati kuna serikali watakosa nguvu ya kufanya kazi, nawasihi tuache tabia hiyo wote tunakosea,” anasisitiza Kinana.

Kinana anasema hafurahishwi na namna watendaji hao wanavyoshambuliwa, akishauri kama mambo hayaendi sawa waende kwenye ofisi zao kuomba ufafanuzi badala ya kuwasema bila kujua jambo kwa kina.

“Hawa ni tofauti na sisi tunaweza kwenda kwenye mikutano ya hadhara tukaona watu wengi na tukapandwa na jaziba lakini hawa wanafuata kanuni na taratibu, na mkiona mambo yanachelewa mjue wanazingatia kanuni na sheria,” anaongeza.

 VIKUNDI KUCHAFUANA

Katika hatua nyingine Kinana anabainisha kuwa kuna  baadhi ya wana CCM wanaotengeneza vikundi vya Whatssap  vinavyotumika kudhalilishana, kutuhumiana na kusemana vibaya.

Alidhani vikundi hivyo ni vya kutengeneza na kuelezana habari njema za chama na shughuli za maendeleo, lakini anashwangazwa vinatumika kushambulia watu, akishauri visitumike kudhalilishana, kutuhumiana na kusemana vibaya.

“Nadhani itabidi tutengeneze utaratibu ndani ya chama chetu, hatuwezi kuwa na chama ambacho kuna vikundi, halafu mtu akikukosea humo humo kwenye kikundi unaanza kumsema vibaya  na wewe au yeye inabidi ajibu.” Anaongeza.

“Tena mnawagawa watu. Anaulizwa uko wapi wewe upo na mimi au na yeye? Akisema siko na yeyote anaambiwa hapana basi kama hauko na yeyote uko na mimi,” anaeleza.

Makamu Mwenyekiti Bara anasisitiza wanachama kushikamana  kwa umoja, akieleza kuwa atawaomba wakuu wa wilaya wamtafutie  madalali ambao hawataki utulivu wanaochochea mote ili watu wafarakane.

"Kuna watu mahali kukitulia wanakosa raha, mpaka wachochee, wakimuona diwani anafanya kazi vizuri hawakubali mpaka wamtafutie wa kumpinga, waambieni waache hizo kazi,” anaelekeza  Kinana

Anawataka wenyeviti wa wilaya na mikoa endadapo wataona mtu anajiandaa na uchaguzi kwa kuanza kampeni kabla ya muda wamdhibiti kwasababu kanuni za maadili zipo.

“Mkiona mtu anatafuta nafasi ya mtu ambaye tayari  nafasi hiyo ina mtu msimcheleweshe, tunataka nchi itulie mkiweka nguvu zenu katika kupambana kuleta maendeleo tutapiga hatua,” anashauri Kinana.

Katika mkutano huo, mjumbe wa Kamati Kuu ya  Taifa CCM, (NEC), Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Silanga, anasema ili chama hicho kitekeleze ilani yake kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi mshikamano baina ya chama na watendaji wa serikali ni muhimu.

 “Mnajua tunakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na mkuu ilitufanikishe jambo hili ni lazima madiwani na wabunge watekeleze ahadi kwa kuzingatia ilani ili tuendelea kupata urahisi …chama kushika dola,” anasema Silanaga.

Mwenyekiti wa CCM, Mara, Patrick Chandi, anasema mkoa huo umepokea Shilingi bilioni 600 kutoka serikalini  kutekeleza miradi ya maendeleo na kwamba wanachohitaji ni ushirikiano wa viongozi wa CCM na serikali kuisimamia.

 “Tunachohitaji hapa ni usimamizi kwa viongozi wetu kuanzia madiwani kwa sababu ilani ni mkataba na wananchi, tukisimamia vizuri tutaendelea kushinda na tutazidi kukiongezea chama chetu nguvu na mapato,” anasema Chandi.