RAIS mteule wa Marekani, Donald Trump, anadai kuwa Waafrika ‘hawajatimia’ wana upungufu kuanzia fikra, matendo na kumudu maisha yao.
Wanahitaji kuongozwa na Wazungu zaidi, kwa kuwa wana kila rasilimali lakini hawawezi kupanga wala kujipatia maendeleo. Wanazaliwa maskini na ombaomba hadi kufikia kifo wamebaki fukara.
Inawezekana analosema likapingwa au likachukuliwa kila mmoja kwa mtazamo wake, lakini hili la Afrika kuwa karakana ya kubeti na vijana wake kutegemea kupata pesa nyingi kwa mkupuo bila kufanyakazi msingojee Trump awaambie.
Viongozi wa Afrika wakumbuke kuwa kazi ni nguzo muhimu katika maisha na ndiyo ufunguo wa kila kitu kuanzia mtu binafsi, familia na taifa kupata uchumi na maendeleo endelevu.
Hakuna usawa kwenye jamii pasipo kila mtu kufanya kazi. Mataifa yaliyoendelea ya Ulaya, Asia kama China na Japan, Amerika mfano Marekani na Canada yameweka juhudi nyingi na kuongeza ufanisi kwenye kufanya kazi.
Watu wa jinsia zote watoto, wazee kwa vijana wanajituma kwenye kazi. Leo wanajivunia mafanikio na maendeleo makubwa ambayo Afrika inayoyasikia hata kuyaona.
Linapokuja suala la kazi hali kwa Afrika na Tanzania ni kichekesho. Dunia ya leo watu wanahimizwa kusaka pesa bila kufanya kazi kwa kuhamasishwa kucheza kamari au kubeti. Ndiyo michezo ya kubahatisha.
Katika majiji, mijini na vijijini kamari ndiyo habari mubashara kila mahali ni mabango na matangazo kwenye runinga na redio.
Vijana wanahamasishwa kuwa mmoja akicheza kwa Shilingi kadhaa, mathalani Kenya, Tanzania na Uganda atapata milioni nyingi kuanzia tano,10, 50 na zaidi.
Kwa buku tu unalala maskini unaamka tajiri. Afrika inapohimiza raia wake hasa vijana wasifanye kazi wategemee kubeti au kamari ili wawe matajiri ‘imelikoroga’.
Ni muhimu kusema ukweli kuwa ni lazima kufanya kazi ili kupata pesa na hakuna zaidi. Kama ni mfanyakazi wa kuajiriwa atapokea mshahara au ujira mwisho wa mwezi.
Kadhalika, kwenye biashara utapata faida ndiyo pesa unazotaka.
Aidha, unaweza kupata fedha kwa kupewa urithi na mzazi au mlezi na zaidi unajipatia fedha unapokopa kutoka taasisi za fedha au za serikali kama ulivyo mkopo wa halmashauri ukitoa fedha kwa mfumo wa asilimia 4:4:2 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Ukweli ni kwamba hakuna mapato halali nje ya kazi halali. Vijana wanaopanga misururu kubeti hawawezi kuondoa umaskini na sio rahisi kutumia ‘buku’ siku moja ukapata milioni 10 papo hapo.
UKWELI USEMWE
Kwa mujibu wa Shiŕika la Kazi Duniani (ILO), nguvu kazi ya vijana katika nchi za Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa inatarajiwa kufikia milioni 72.6 kati ya mwaka wa 2023 na 2050.
ILO inasema ukuaji huo unaweza kuandaa fuŕsa ya kuwa na nguvukazi kubwa duniani ya uzalishaji na kubadili sura ya bara hili kutoka kwenye ufukara na kuwa nchi ya asali na maziwa.
Hata hivyo, nchi nyingi za Kiafrika hazitengenezi ajira za kutosha kwa ajili ya vijana, badala yake zinaruhusu kampuni za kubashiri na kubeti au kuendesha pikipiki na kupata ajali zinazowaua vijana hao kila siku.
Afrika ina ‘kichaa cha kubeti’ na kubashiri matokeo ya mpira wa miguu au ‘match fixing’. Kwa upande wa eneo la Kusini ya Sahara Nigeria inaongoza kwa kubeti na kubashiri matokeo ya kandanda viwanjani.
Hata hivyo, ni wazi vijana hawaambiwi ukweli, kuwa buku au 1,000 haiwapi milioni 50, wanadanganywa kuwa kwa shilingi au hela chache wanamaliza umaskini. Ni wakati sasa waambiwe kuwa kubeti kunasababisha wengi kupoteza fedha zao kila siku. Kama watabeti 1,000,000 kwa Shilingi alfu kila mtu, itapatikana bilioni (1,000,000,000) hapo itachukuliwa milioni 100 wakapewa washindi wachache.
Na nyingine milioni 900 zikabakia mikononi mwa kampuni wachezeshaji au za kubeti, hivyo vijana wengi wanapoteza mamilioni yao. Pesa kidogo haiwezi kuwapa mabilioni kama wanavyoambiwa.
Fedha nyingi kuanzia kucheza dubwi, kubeti mitandaoni, kwenye simu na kwenye ofisi zinapotea kila siku.
Tamaa ya kupata fedha nyingi kwa kutumia fedha kidogo tena bila kufanya kazi inawaangamiza vijana Afrika.
Inawezekana kwa mtindo huo, wezi wakawa wanaongezeka kila leo wakiiba mali na vitu mitaani, mijini na katika maji yanajaa wahalifu na waporaji.
Kadhalika, inawezekana maduka na biashara mbalimbali zinafilisika kwa sababu fedha zinaporwa kuelekezwa kwenye kubeti.
Afrika inazidi kuwa bara la dhiki, vijana wake wakizamishwa baharini hasa Mediterranean kila wakati wakikimbia nchi zao kwenda Ulaya na Amerika kutafuta maisha bora kisa kuna hali mbaya kwenye mataifa yao.
Wengi hawafanyi kazi badala yake wanataka mafanikio na utajiri kupitia kubeti na kujipatia fedha nyingi kwa njia rahisi bila kutoka jasho.
Itakumbukwa kuwa katika vyuo vikuu, posho za kujikimu za mabweni na za kugharamia masomo zinazotolewa na bodi za mikopo ya elimu ya huu za mataifa mbalimbali hutumiwa kubeti, kadhalika pensheni na hata mikopo inawekezwa kwenye kubashiri.
Ukweli ni kwamba, mamilioni ya Waafrika hasa vijana wanageuka maskini kwa kisingizio cha kutaka kupata pesa bila kufanya kazi.
Ni vyema Afrika ijitafakari kwenye hili la kuhamasisha umma kupata pesa nyingi bila kufanya kazi. Yote hayo yakifanikishwa na kampeni za kubet.
Watu waachane na mtindo huo unaochochea uvivu na kupotosha dhana nzima kwamba kazi ndiyo msingi wa maendeleo na sio kuwekeza kwenye kamari.
Vijana ambao hawana kazi hujiingiza kwenye vituo vya kamari kujaribu bahati zao, wapo wanaotumia simu wote wakilenga kupata pesa za chap chap kwa kubashiri.
Yote hayo yanachochewa na ahadi za kupata mamilioni kwa kutumia pesa ndogo au ‘buku’ tu ambacho ndicho kivutio kikubwa zaidi kwa wachezaji hao ambao kila mara wanatoka patupu licha ya kwamba wamekuwa waraibu wa kamari.
Kamari ya elektroniki kwa vijana wengi inakuwa kama kazi ya kila siku, hofu ni kwamba huenda hawafahamu kuwa kubeti ni biashara na watu wazito duniani wamewekeza hela zao.
Wanachotafuta ni wachezaji wapoteze fedha ili wafanyabiashara hao wazipate ambayo ndiyo faida wanayoitaka na ni ukweli kuwa kupoteza pesa ni jambo la kawaida kuliko kuzipata kwa wachezaji hao.
Hivi vijana hawa wasio na kazi kwanini wahatarishe fedha zao chache walizo nazo?
MUDA UNAOPOTEA
Ni wazi kuwa mara nyingi Afrika haiwezi kufanya kampeni bila kuwa na msaada kutoka kwa washirika wa nchi zilizoendelea wakiitwa wadau wa maendeleo.
Kampeni hizo zinaweza kuwa kutokomeza magonjwa au kuelimisha umma kuhusu tatizo ndani ya jamii.
Na pengine muda wa matangazo ya kuelimisha umma ni kidogo, lakini cha kushangaza muda au (air time) inayotumiwa kutangaza kubeti ni mwingi mno.
Vyombo vya habari hasa redio na televisheni ndani ya saa 24 zinaweza kutumia pengine saa 10 nzima kutangaza matangazo ya kubeti na kuelekeza watu jinsi ya kubeti.
Kwa hakika ‘air time’ au muda unaotumiwa kutangaza matangazo ya kubet ni mwingi, lakini kama ungetumiwa kuhamasisha vijana kufanya kazi, kuwa wabunifu, kufikia masoko ya bidhaa zao, kujilinda na magonjwa, kuacha ulevi wa dawa haramu za kulevya, pombe na ulevi kupindukia huenda kungekuwa na mabadiliko ya tabia.
Karibu nchi zote za Afrika karibu zina bodi za kudhibiti na kutoa leseni ya michezo ya bahati nasibu ni hilo limeshika kasi.
Michezo ya kamari inayoendelea Afrika miongoni mwa mashabiki wa soka na vijana ni uwekezaji wenye thamani ya matrilioni ya dola kwa kampuni zinazoiendesha lakini kwa wanaocheza hali si ya kujivunia.
AFRIKA ISHTUKE
Bara hili lijue ukweli kuwa wakati wanawaachia vijana wake kupoteza hata dola moja walionayo kwenye kamari au kubeti, vijana wengine duniani kama nchini China wanatengeneza bodaboda ambazo zinauzwa kila mahali Afrika.
Vijana wa Kusini ya Sahara ndiyo wanaouza vitu visivyo na thamani kama mitumba ya viatu, nguo, vyombo vya nyumbani, runinga na hata redio.
Afrika nguvu kazi yake inapotea kwa kuwaacha vijana kuendelea na kazi zisizo na tija kama kuuza doli, protekta za simu na 'foni' za masikioni.
Pikipiki za China zinatumiwa na kila mtu Afrika na vifaa vyote vinavyouzwa na wamachinga vijana kwa wazee wa Afrika vinatoka huko huko.
Wanalofanya ni kukaa juu ya bodaboda na kuzitumia kila mahali hata wakikimbia kwenye kukimbiza kubeti, hilo liibue tafakari.
Hivi bara hili linajua linachofanya kwa kuwaacha vijana wake waendelee kucheza kamari Januari hadi Desemba? Ni wakati wa kujirekebisha na ikibidi kuzipiga marufuku kwa sababu kuna faida kidogo kuliko hasara kubwa iliyo mbele yake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED