DC mwenye dhamana abeba jukumu ‘mguu kwa mguu’ vitani kukabili mauziano feki yaliyokithiri

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:40 PM Jul 26 2024
Shamba.
Picha:Mtandao
Shamba.

BAGAMOYO ni wilaya iliyoko mkoa wa Pwani na makao makuu yake yalikuwa bandari muhimu ya biashara ya kimataifa katika Karne ya 19 na mwanzoni mwa Karne ya 20.

Mji huo, pia ulikuwa kituo cha biashara ya utumwa, jambo ambalo limeacha alama ya kudumu kwenye historia na utamaduni wa eneo hilo, hadi leo Bagamoyo ni kivutio maarufu cha watalii kinachojulikana kwa fukwe zake nzuri, maeneo ya kihistoria, na tamaduni hai.

Mengi yamefanyika katika wilaya hiyo, kuwafanya wananchi wake waendelee kukua kimaendeleo na kiuchumi ambao wengi wamejikita katika shughuli za biashara za rasilimali za bahari.

Wilaya ya Bagamoyo, hivi karibuni imekuwa ikitajwa si kwa utalii sana, bali kwa migogoro ya ardhi hususani katika kata ya Mapinga, jambo ambalo limechangiwa na wengi kuuziwa maeneo ambayo tayari yana hatimiliki.

Katika eneo hilo, wananchi walio wengi wanatoka mkoa jirani wa Dar es Salam na maeneo mengi wamekuwa wakilalamikia kuuziwa maeneo yenye hati miliki na baadhi yao kupata hasara ya kuvunjiwa nyumba zao kutokana na kujenga kwenye maeneo yanayomilikiwa kihalali.

Hali hiyo ilisababisha mawaziri tofauti kutoka Wizara ya Ardhi, wanapofanya ziara zao katika mkoa wa Pwani, ikaawalazimu kufika katika kata ya Mapinga kusikiliza wananchi wenye migogoro.

Pamoja na maeneo mengine ya mkoa wa Pwani kuwa na migogoro ya ardhi katika wilaya za Kibaha, Kisarawe, Mkuranga na Rufiji, bado, lakini Bagamoyo imekuwa ikitajwa kuongoza hususani eneo hilo la Mapinga na Makurunge.

Ni jambo ambalo Ofisi ya Kamishna wa Ardhi wizarani inashuhudia kesi nyingi za ardhi za mkoa huo, inatoka maeneo hayo.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Vagamoyo Halima Okash, akaaanzisha Kliniki ya Ardhi, ambayo ilianza kufanyika katika Halmashauri za Chalinze na Bagamoyo, kwa kusikiliza wananchi wenye migogoro akiwa na timu ya watendaji wa ardhi.

Hata hivyo, pamoja na kliniki hiyo, Okash akaona bado ipo sababu ya kuanza oparesheni malaum inayoanza kwenye maeneo yenye migogoro mingi ya ardhi, akiwa na timu ya watendaji wa Idara ya Ardhi, Mwanasheria akiambatana na watendaji kutoka ofisi ya ardhi ya kila Halmashauri.

Jambo analolifanya Okash, ni jipya kwa wakazi wa wilaya hiyo na linawezesha wananchi wengi wenye  migogoro kujitokeza kupatiwa ufumbuzi kutoka kwa watalaamu wa ardhi na mwanasheria kuhusiana na maeneo wanayomiliki.

Pamoja na kufanya kliniki hizo kwenye kila Halmashauri za Wilaya ya Bagamoyo, bado Okash anaona kuna malengo hajayafikia katika kutatua migogoro kwenye eneo lake na sasa analazimika kuanzisha Oparesheni Mapinga tokomeza migogoro ya ardhi ambayo aliianza June 24 hadi Julai 15.

Katika Oparesheni hiyo, ofisi ya Mkuu wa Wilaya  ikiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, watendaji kutoka Idara ya Ardhi ya Wilaya hiyo, wanasheria na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Pwani, wakaweka kambi Mapinga, kusikiliza migogoro hiyo. 

Ni oparesheni iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, kwa kushirikiana na watendaji kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Pwani, wataalamu wa sheria kutoka mahakamani na Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo. 

Okash anasema, wamelazimika kuanza katika kata hiyo na baadae wataenda Makurunge na Fujayisi, huku akieleza kwamba Oparesheni hiyo kuwa ni kwa ajili ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi katika Kata ya Mapinga. 

Okash anasema, wameona wawafuate wananchi kwenye maeneo yao yenye migogoro,Ili kuyatafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi na wanasheria.

 Anasema katika baadhi ya maeneo kata ya Mapinga kuna mashamba makubwa, nyumba nzuri lakini maeneo wanayoishi hawayamiliki kihalali tofauti na taratibu zinavyoelekeza.

 Kadhalika Mkuu huyo wa Wilaya anasema ili kukabiliana na migogoro hiyo pia wameanza kubainisha Makampuni yanayojihusisha na kupima na kuuza ardhi katika wilaya hiyo kutokana na baadhi ya Makampuni hayo kuhusishwa kuuza maeneo yenye hatimiliki.

 WADAU WAKUU

Kamishna Msaidizi wa ardhi Mkoa wa Dar es Salam na Pwani Shukrani Kyando anasema ameungana na Mkuu huyo wa Wilaya kusikiliza changamoto za masuala ya ardhi na kuyatafutia ufumbuzi.

Kamishna Kyando anasema, katika Oparesheni hiyo pia wametumia kutoa ushauri kwa kesi ambazo zipo mahakamani wananchi kuhakikisha wanatii amri Ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Pia, ametoa ushauri kwa wananchi kupima maeneo yao sambamba na kufuata taratibu za umiliki wa ardhi kuepusha migogoro ambayo inatokea kwa kutozingatia taratibu.

Rose Leon, ni mmoja wa wananchi waliojitokeza katika oparesheni hiyo ambaye anaiomba serikali kufungia kampuni zinazojihusisha na uuzaji ardhi kutokana na kulalamikiwa kuuza maeneo yenye hati miliki na kuchangia kuwepo kwa migogoro.

Mwinyi Masoud mkazi wa Mingoi, amempongeza Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuanzisha oparesheni hiyo ambayo imekuwa msaada kwa walio wengi kutatuliwa migogoro yao sambamba na kupewa ushauri wa kitaalamu kumaliza migogoro hiyo.

Kupita oparesheni hiyo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi na ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Pwani wananchi zaidi ya 3,018 walijitokeza kusikilizwa na zaidi ya migogoro 82 ilitatuliwa ikiwemo mikubwa ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 10.

Kupitia Mkuu wa Wilaya, migogoro ambayo ilihitaji suhuhu na maridhiano ambayo kwa kipindi kirefu ilisababisha wahusika kwenda mahakami mara kwa mara hatimaye nayo ilitatuliwa kwa makubaliano ya mmiliki wa eneo na wanaodaiwa kuvamia.

Kupitiaa oparesheni hiyo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imewabaini baadhi ya vinara wanaodaiwa kuhusika kuchochea migogoro ya ardhi katika kata ya Mapinga na maeneo mengine ya wilaya hiyo, wakiwamo viongozi wa serikali na kichama kuwa mashuhuda wa mauziano ardhi zaidi ya mara moja.

Pia, akasema baadhi wameshiriki moja kwa moja kwenye mauziano maeneo yenye migogoro ambao hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Baada ya Oparesheni Mapinga Tokomeza Migogoro, Okash anatoa rai kwa wananchi kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi na uuzaji wa ardhi kwa kuwashirikisha wataalamu wa idara ya ardhi wa wilaya hiyo kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

ALIYEKUWA WAZIRI 

Hivi karibuni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa, naye alifanya ziara katika mkoa wa Pwani na kufanya mkutano wilaya ya Bagamoyo ambayo kupitia kliniki ya ardhi maarufu kama ‘Samia Kliniki.

Alimppongeza Mkuu  wa Wilaya- Okash, kwa jitihada alizofanya kutatua migogoro ya ardhi kwa nia ya suluhu na anatumia  nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi wenye migogoro kuacha kwenda ofisini kwake na badala yake kutmia kliniki za ardhi kwenye maeneo yao kutafutiwa ufumbuzi wa migogoro yao.

Anasema, wananchi wengi wanaoenda ofisini ufumbuzi  wa changamoto zao unashindwa kupatikana kwakuwa watendaji pamoja na makamishna wa ardhi wa maeneo yao hawapo ofisini kwake ni lazima watarudishwa kwenye wilaya au mikoa waliyotokea kwa ajili ya utatuzi.

Akawaahidi  kuendelea kushirikiana na viongozi wa ardhi kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi hapa nchini huku akisema watendaji watakaobainika kuhusika kwenye migogoro hatua za kisheria zitachukuliwa.

Hata hivyo uhalisia unaonyesha kwamba migogoro katika ya ardhi katika mkoa wa Pwani inachangiwa na mashamba ambayo hapo awali yaliachwa bila kuendelezwa kwa muda mrefu na hivyo baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi kwa kuwauzia wananchi bila kufuata taratibu.