+63 BAADA YA UHURU: Tanzania iinuke kufikia miaka 100 ya uhuru iking’ara zaidi

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 08:31 AM Dec 10 2024
 Tanzania iinuke kufikia miaka  100 ya uhuru iking’ara  zaidi
Picha: Mtandao
Tanzania iinuke kufikia miaka 100 ya uhuru iking’ara zaidi

NI hongera kwa taifa kutimiza miaka 63 ya uhuru ikiwa imebakia miongo michache kuifikia jubilii ya miaka 100 ya uhuru wa Tanganyika, itakayosherehekewa Desemba 9, mwaka 2061.

Sherehe za uhuru jana hazikuadhimishwa kitaifa, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kusherehekea ngazi za mikoa.

Amefuta maadhimisho ya sherehe za miaka 63 ya uhuru kitaifa na kuelekeza zifanyike katika ngazi ya mikoa, kwa  kutoa huduma za kijamii, kupanda miti , usafi wa mazingira,  masoko, hospitalini, kambi za wazee na wenye mahitaji maalum.

Wakati Watanzania wanasherehekea kumpinga na kumshinda mkoloni, yapo mambo  ambayo raia wanayachukulia kawaida au poa, japo wanapaswa kuyabeba kama sababu kwa kila Mtanzania  kusherehekea miongo sita ya mafanikio ya kihistoria.

Ikumbukwe wakati mataifa mengine ya  Kiafrika  yalipopata uhuru yalijitumbukiza kwenye vita, machafuko na migogoro, Tanzania iliendelea kujiimarisha kiuchumi kadhalika kuwa nchi ya amani na kubaki kwenye misingi bila kuvurugana.
Zipo nchi baada ya uhuru ziliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini Tanzania iliendelea kuwa kimbilio la wanaoteseka, chemchemi na kisiwa cha  amani, utulivu  na maridhiano na hilo ni jambo la kujivunia zaidi.

Inawezekana Tanzania  imeendelea kuwa na utajiri mwingi  zaidi kuanzia madini, ardhi, mifugo na vivutia watalii katika ukanda huu wa  Afrika Mashariki. Haya yote ni mambo bora  na ya  kusherehekea kwa sauti kubwa na shangwe nyingi.

Lakini ikiwa miaka 63 iliyopita imekuwa ya kushikilia na kudumisha  amani na utulivu, kujenga uchumi, maridhiano na kuachana na mafarakano, miaka 37 ijayo  ili kufika miaka 100 lazima iwe ya kufikia maendeleo endelevu kwa kila sekta.

Ni  kwa kurejea zile taarifa kuwa nchi za Asia kama  Korea Kusini na China zilikuwa kwenye kiwango kimoja cha kiuchumi miaka ya 1960 lakini leo ziko mbali na ndizo injini za uchumi duniani.

Licha ya kwamba mataifa hayo yalikuwa pamoja na nchi za Afrika ikiwamo Tanzania 1960, miongo mitatu au  miaka 30 baadaye yaani kuanzia 1990 zilizizidi kwa kishindo nchi za Kiafrika.

Miaka 63 iliyopita ni uthibitisho kwamba watu wamesimama kulinda umoja na  utaifa wa Tanzania na Zanzibar.

Licha ya kuwa na makabila zaidi ya 130 taifa limebakia kuwa moja na hilo ni jambo la kujivunia lakini sasa likereketwe kufikia maendeleo na kuuaga umaskini. 

Japo Watanzania Bara na Zanzibar ni wengi hakuna wazo la kutengana na kila siku ni lazima kuimarisha na kudumisha umoja wa kitaifa na mshikamano. Watanzania wameelewa kuwa pamoja na changamoto, kupanda na kushuka  milima na mabonde ‘Tanzania is there to stay’ na kwamba lazima kuendelea kuiboresha na kuijenga zaidi kila uchao.

Sasa ni wakati wa kufikiria ni wapi Watanzania wanataka kwenda na wanafikaje? Cha msingi ni uongozi uendelee kuwa thabiti na wenye maono makubwa.

Watanzania wameimarika tangu uhuru licha ya kushindwa kufikia ilipo Korea Kusini au China sasa, lakini ili waweze kuruka masafa mengine wanahitaji uongozi bora zaidi na zaidi wenye maoni mapana yakuifikisha  miaka 100 ikiwa bora zaidi.

Wananchi na vongozi  lazima watambue kuwa bado ni nchi ya watu wengi maskini na wasio na elimu bora ambao pato la mtu mmoja mmoja  ni takriban Sh 3,000,000 (dola 1,200) kwa  mujibu wa Benki ya Dunia,  kwa mwaka.
 Lakini  huo ni wastani wa kitakwimu, wengi wanaishi chini ya dola moja (Shilingi 2,600), kwa kiwango hicho ya  shilingi  kwa siku.

Ili kufaulu miaka 37ijayo sera zinazopitishwa lazima ziakisi vipaumbele, hasa ukweli kwamba bado taifa halijaweza kuwezesha raia kupata chakula au milo mitatu, kutibu, kusomesha kutoa huduma muhimu kwa gharama rafiki.
Changamoto  kwa viongozi  na utawala wa awamu zote za sasa na zijazo iwe ni kuona uchungu kuwa watu  bado ni maskini, wanaoishi kwenye vibanda vya nyasi, makuti na matope au matembe.

Uongozi usikubali kuwapo na kiwango cha juu cha vifo vya watoto wachanga kwa kiasi cha watoto 43 kwa kila 1,000 wanaozaliwa hai.

Viongozi waone uchungu wakijipiga vifua na kujiambia kuwa ni aibu kuona wanawake wetu wanakufa kwenye uzazi yaani roho za wazazi 104  kati ya 100,000  zinapotea  kutokana na masuala ya uzazi.

Iwakere viongozi kuona kuwa wasichana  wanapewa mimba na kuozwa utotoni, watoto wanakatiliwa kwa kiwango kikubwa wakiingiliwa kinyume na maumbile na kujansiwa na hayoyote ni kutokana na umaskini kisha kulitokomeza tatizo hilo.

Si suala la siasa au ni nani anayeongoza. Ni wajibu wa viongozi  kuwapa watu  mambo muhimu wanayohitaji ili kuishi maisha ya furaha hasa kuwa na afya na bora, elimu, maji safi, makazi bora na bila kulia upungufu au ukosefu wa  chakula.

Tanzania inapoisogelea miaka 100 ya uhuru wa Tanganyika Watanzania wasionekane tena wakipokea bidhaa muhimu kama ‘taulo za kike’  kutoka kwa wahisani.

Haipendezi taifa likipokea misaada kama kujengewa vyoo shuleni , kuwekewa maji na wafadhili wa  mataifa wahisani badala ya serikali kuweka huduma hizo.

Ufike wakati kama taifa kujihusisha kikamilifu na rasilimali za taifa na kuzitunza. Kadhalika kutunza fedha za umma, kuacha ufisadi na ubadhirifu ili kuwa a watu wenye afya tele wanaosherehekea maiaka 100 ya uhuru na ushindi.