2024 IMETESA WENGI; Trump apigwa shaba, Gen Z ikimtikisa Ruto

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:31 PM Jan 02 2025
Rais wa Kenya, William Ruto
Picha: Mtandao
Rais wa Kenya, William Ruto

ZIMEBAKIA siku 19 mbabe Donald Trump, arudi tena ndani ya ikulu ya Marekani ya White House, baada ya kuchaguliwa kwa kishindo.

Anarejea baada ya kumshinda mpinzani wake Makamu wa Rais wa sasa mwanamama Kamala Harris wa chama cha Democrat.  

Trump mwenye miaka 78 hatausahau mwaka jana kwa vile wakati wa kampeni wababe walitaka kumaliza maisha yake, kwa kumpiga risasi tena iliyolenga kichwani ikitua sikioni, mkasa ukitokea mwezi Julai.

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump
Akiwa kwenye kampeni ndania ya jimbo la Pennsylvania wakati akihutubia, milio ya risasi ilisikika kwenye mkutano wa hadhara.

Alinusuriwa kwenye jaribio hilo na maofisa usalama akiamini mhusika aliazimia kumuua, baada ya kurushiwa risasi sikioni. Katika chapisho lake kwenye mtandao wake wa Truth Social anasema.

“Risasi ilipenya sehemu ya juu ya sikio la kulia.”

Mtuhumiwa alipigwa risasi na kufa papo hapo katika eneo la tukio na maofisa wa secret service au wana usalama.

Wakati mwaka 2024 umemalizika, barani Afrika, wapo wanasiasa kadhaa waliotikiswa ndani ya mamalaka.

Ni jirani Kenya, Rais William Ruto, akikimbizwa mchakamchaka na maandamano ya miezi kadhaa, yaliyopewa jina maarufu Gen Z au Generation Zero, kwa maana kizazi cha mwishoni mwa karne 21, yakimtikisa.

Akichukua maamuzi kadhaa ikiwamo kubadilisha baadhi ya viongozi wanaomzunguka akianza na makamu wake Rigathi Gachagua.

Naibu Rais anatuhumiwa kumhujumu Rais Ruto, kufadhili na kuhamasisha GEN Z kuvuruga serikali.

Aidha, analichambua baraza lake la mawaziri na kuwatumbua baadhi huku akiingiza wapya. Gachagua mwenyewe akidai kuwa ametolewa kafara' chanzo kikianzia kwenye maandamano hayo.

Vijana wa Gen Z hoja yao ya kuingia mtaani na hata kidiriki kulivamia bunge, kujipiga picha za simu maarufu -selfie wakishikilia siwa, ni pamoja na madai kuwa maisha yamekuwa ghali chini ya uongozi wa Ruto.

Mara kadhaa Ruto anadai ndani ya maandamano hayo kuna uratibu wa kisiasa na hayana uhalisia wa akitoa lawama kwa viongozi tofauti waliokwisha staafu.

Kenya inashuhudia machafuko ya wiki tatu mfululizo waandamanaji wakivamia bunge Juni 25 baada ya muswada wa fedha uliopendekeza nyongeza ya kodi kupitishwa.

Muswada huo uliwakera ni baada ya kuwaongezea kodi Wakenya licha ya kodi ya nyumba ya asilimia 1.5 iliyowekwa awali na ile ya bima ya matibabu ya asilimia 2.7.

Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, zaidi ya watu 41 wameuawa katika maandamano hayo, ambayo yalibadilika na kuwa wito wa kumtaka rais kujiuzulu.

Uvamizi huo wa bunge ambao ni wa kwanza katika historia ya Kenya, unasababisha uharibifu mkubwa lakini ukiwashangaza wengi sio tu Afrika na  duniani 

GACHAGUA ARITHIWA

Baada ya vuta nikuvute Bunge la Taifa la Kenya likapitisha jina la mrithi wa naibu wa rais, Kithure Kindiki, na kumweka pembeni Gachagua kwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Alikuwa Waziri wa usalama wa taifa na alichukua nafasi hiyo baada ya bunge kupiga kura kumpa ridhaa. 

Katiba ya Kenya inaelekeza kuwa  baada ya jina la mrithi wa naibu kuwasilishwa na rais, bunge la taifa lina lazima kumridhia au kumkataa, kazi iliyofanyika Oktoba mwaka huu.

WALIA NA UTAJIRI

Utajiri wa ghafla wa baadhi ya viongozi umewastua baadhi ya Wakenya likiwamo Baraza la Wazee nchini humo.

Kwa ujumla liliwaunga mkono vijana na maandamano ya  Gen Z likimtaka Rais  Ruto, kukabiliana na ufisadi uliokithiri katika serikali yake.

Wazee hao wanaomba uwajibikaji katika serikali wakitaka kujua jinsi baadhi ya viongozi walivyo matajiri ghafla na kutangaza utajiri wao hadharani.

 “Tumeona watu waliokaa madarakani kwa muda usiozidi miaka miwili wakiwa na mamilioni ya fedha, wakitumia ndege kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine mbali na kutoa michango ya mamilioni ya hela kila wikendi katika harambee bila kujali vijana ambao hawana ajira,’’ ni moja ya madai yao.

MOTO KOREA

Mustakabali wa Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol, umebakia njia panda, baada ya usiku wa machafuko.

Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol
Ni hatua inayokuja baada ya kutangaza sheria ya kijeshi na kisha kuiondoa ghafla na kuitumbukiza nchi hiyo katika machafuko.

Yoon, ambaye alishinda urais kwa kura chache 2022, hakupendwa sana na Wakorea Kusini na amekuwa akikabiliwa na shinikizo tangu ashindwe uchaguzi wa bunge Aprili, mwaka huu.

Hatua hiyo aliyochukua inaonekana kuwa sawa na kura ya kutokuwa na imani naye.

 Pia amekumbwa na matatizo binafsi, akiomba msamaha katika hotuba yake kwa taifa kwa msururu wa mabishano yaliyomhusu  mkewe ambayo ni pamoja na madai ya kukubali mkoba wa kifahari zawadi kutoka kampuni ya vitu vya kifahari ya  Dior ya Ufaransa na udanganyifu wa uwekezaji wa hisa.

Bunge la Korea Kusini limepiga kura kumuondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol, kutokana na jaribio lake lililoshindwa la kutangaza sheria ya kijeshi iliyodumu kwa muda mfupi.Lilipiga kura Desemba 14, 2024, kumuondoa madarakani rais huyo.

Kati ya wabunge 300, 204 wamepiga kura ya kumuondoa rais madarakani kwa madai ya uasi, huku 85 wakipiga kura ya kupinga. Watatu hawakupiga kura, huku kura nane zikibatilishwa.

Chanzo: MITANDAO

HERI YA MWAKA MPYA 2025