Serikali yaweka wazi hali ya damu salama

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:24 AM Jun 15 2024
 Siku ya Uchangiaji Damu Duniani.
Picha: Mtandao
Siku ya Uchangiaji Damu Duniani.

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema Zanzibar haina uhaba wa damu lakini pia haina damu ya kutosha ambayo imehifadhiwa katika benki ya damu kama ni damu ya akiba.

Akizungumza kuhusu maadhimisho ya Siku ya Uchangiaji Damu Duniani ambayo hufanyika Juni 14 kila mwaka, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wanaohitaji huduma hiyo, 

Alisema sababu kubwa zinazopelekea kuhitaji tiba ya damu ni kupoteza damu kwa wingi hasa wakati wa kujifungua, ajali au tiba ya upasuaji na pia upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka mitano wenye kuugua maradhi ya mifupa na watu wazima kutokana na sababu mbalimbali.

Mazrui alisema Mpango wa Taifa wa Damu Salama ambao unazingatia uchangiaji wa damu kwa hiari, ulianza mwaka 2005 Zanzibar chini ya Wizara ya Afya kwa ufadhili mkubwa wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupunguza Kasi za Maambukizi ya UKIMWI (PEPFAR).

“Nia ni kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI na pia kuziwezesha hospitali kuwa na akiba ya damu ya kutosha wakati wote kwa ajili ya matumizi na si kusubiri mpaka dharura itokee kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo damu zilikawia kuwafika wagonjwa wahitaji na kusababisha wengi wao kupoteza maisha,” alisema.

Waziri alisema kwa mwaka wa fedha 2023/24 mpango umejiwekea malengo ya kukusanya chupa za damu 20,000 na hadi kufikia Machi, mwaka huu, mpango ulikusanya chupa 16,155 sawa na asilimia 80.8 kwa Zanzibar.

Alisema maombi ya damu yaliyopokewa kutoka hospitali zinazotoa tiba ya damu ni 38,595 na kufanikiwa kusambaza 19,785 sawa na asilimia 51 ya maombi hayo.

Kila  mmoja, alisema  ni muhitaji wa damu, hivyo ni vyema kuweka akiba kabla ya kusubiri dharura kutokea na kuwataka wachangiaji damu kuendelea kuchangia ili kuhakikisha benki hiyo inakuwa na damu ya kutosha na kukidhi mahitaji .

Aidha, Waziri Mazrui alisema elimu ya lishe inahitajika kwa jamii kwa sababu kuna changamoto kubwa ya wananchi wa Zanzibar kuwa na lishe duni na bila lishe nzuri lengo la uchagiaji wa damu halitafikiwa.

Alisema mahitaji ya damu ni makubwa Zanzibar na katika miaka 20 ya kuanzishwa kwa benki ya damu na uchangiaji wa damu mwaka 2021/22 benki hiyo ilivunja rekodi kwa kukusanya damu nyingi na kuvuka malengo ambapo ilikusanya chupa 20,000 wakati lengo lilikuwa chupa 16,000.