Wizara ya Nishati yakabidhi gari la kubebea nguzo za umeme Mbinga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:46 PM Jul 20 2024
Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga akijaribu kuendesha gari la kubebea nguzo katika Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma alilokabidhi Leo.

Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga leo Julai 20, 2024 amekabidhi gari la kubebea nguzo katika Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Wakati akikabidhi gari hilo Kapinga amesema Serikali itaendelea kuboresha  maslahi, vitendea kazi na mazingira ya kazi kwa Wafanyakazi wa TANESCO ili kuwapa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

"Kulikuwa na changamoto ya kubeba nguzo kupeleka kwenye maeneo mnayofanyia kazi, Serikali inaamini magari haya yataleta tija na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi ikiwemo kutoa huduma kwa wakati kwa wateja." amesema Kapinga

Akizungumzia  changamoto ya kukatika kwa umeme wilayani Mbinga,  Kapinga amesema Serikali imeshaweka mikakati ya kujenga kituo kipya  cha umeme ambacho kitaboresha hali ya upatikaji umeme.

1

Ameongeza kuwa,  kituo hicho cha kupokea na kupoza umeme  kitajengwa katika mradi wa Gridi Imara Awamu ya Pili.

Amesema TANESCO inaendelea kuboresha miundombinu ya umeme wilayani humo  wakati ujenzi wa kituo cha kupokea na kusambaza umeme ukisubiriwa.

Katika hatua nyingine, Kapinga amewahakikishia wananchi kuwa, Wizara ya Nishati chini ya uongozi wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, itaendelea kuboresha  utoaji wa huduma na upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.
2

Awali, Meneja wa TANESCO  Wilaya ya Mbinga, Mhandisi Edward Kweka alisema kuwa walikuwa wakikutana na changamoto ya ubebaji nguzo kutokana na kutokuwepo kwa gari la kubebea nguzo hizo..

Mhandisi Kweka amesema gari hilo litawasaidia kutoa huduma kwa ufanisi na kuahidi kulitunza.

TANESCO Wilaya ya Mbinga inajumla ya wateja 37,925 na inapokea umeme wa gridi ya Taifa wa kilovoti 33 kutoka kituo cha kupoza umeme cha Songea.

3