Wimbi wanandoa kudai talaka laishtua BAKWATA

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:57 AM Apr 29 2024
Mchoro wa katuni unaoonesha wimbi la talaka kwa wanandoa.
Mchoraji: Abdul Kingo
Mchoro wa katuni unaoonesha wimbi la talaka kwa wanandoa.

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), linatarajia kutoa elimu ya ndoa ili kupunguza wimbi la migogoro na kuvunjika walilobaini kwenye utafiti walioufanya.

Naibu Kadhi Mkuu na Mjumbe wa Baraza la Mashehe (Ulamaa), Shehe Khamis Ngeruko aliyasema hayo jana kwenye mahafali ya saba ya kitaifa ya ‘Bakwata online Akademy (BOA)’ yaliyofanyika jijini hapa.

“Sisi kama Mahakama ya Kadhi tupo njiani sasa baada ya utafiti tumeufanya wa kugundua ndoa nyingi zinakufa katika jamii, ndoa nyingi zinakufa jamani, sisi tupo katika Mahakama ya Kadhi kila anayekuja anataka ndoa yake ivunjwe.”

“Tukamfuata Mufti imekuwaje? kama unavyoona mvua inavyonyesha nyingi na watu wanavuliwa kama samaki, ndio hivyo katika ndoa imekuwa ni balaa. Mufti akasema ingieni mtaani fanyeni utafiti, tukafanya utafiti kama Mahakama ya Kadhi tukagundua tatizo kubwa ni elimu, watu hawana elimu ya ndoa,” alisema.

Alisema wamejipanga mashehe wa mikoa kwenda mikoani kutoa elimu ya ndoa.

Alisema mwanamke na mwanaume wanapaswa kuonesha unyenyekevu nje ya kuta nne za chumba.

 Mufti wa Tanzania, Dk.Abubakar Bin Zubeir, aliwaasa wahitimu elimu waliyoipata waitumie ipasavyo kwa kuwa ujinga ni aibu.

Hivi karibuni, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima akizungumza kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia Mei 15, mwaka huu, alisema ndani ya miezi 10 ya Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 mashauri 14,600 yalipokelewa.

Alisema kati ya hayo migogoro ya ndoa ilikuwa 5,306 sawa na asilimia 36 na matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa yalikuwa 3,350 sawa na asilimia 23.

Alisema mashauri yaliyohusu masuala ya kifamilia na matunzo ya watoto ni 5,944 sawa na asilimia 41,

Kutokana na hali hiyo, aliagiza mikoa na halmashauri kuandaa mijadala katika jamii kwa kutumia wataalamu wa malezi chanya ya watoto, familia, kuhusisha viongozi wa dini ili kutafuta ufumbuzi tatizo la malezi duni ya watoto na mmomonyoko wa maadili.

Alisema mashauri hayo yalifikishwa kupitia mabaraza ya kata na jumuiya na kwa mashauri 3,411 yalifikishwa kwa maofisa ustawi wa jamii 1,642 yalipatiwa ufumbuzi na 443 yanaendelea kufanyiwa kazi.