KUTOZINGATIA sheria kumetajwa kusababisha vifo vya watumishi wawili wa Idara ya Afya wilayani Chato, Geita waliofikwa na umauti kutokana na ajali ya barabarani juzi.
Watumishi hao walifariki duni baada ya gari aina ya Toyota Probox kugongana na mwendesha pikipiki aliyekuwa amebeba mtumishi mwenzake.
Kamanda wa polisi mkoani Geita, Safia Jongo, aliambia Nipashe kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:15 jioni katika kijiji cha Mlimani Rubambangwe, wilayani Geita kwenye makutano ya barabara kuu ya Muganza-Buzirayombo na ile ya Chato-Biharamulo.
"Watumishi hao walikuwa na pikipiki wakitokea kwenye njia ndogo kuingia kwenye barabara kubwa pasipo kuchukua tahadhari, wakati mwenye gari alikuwa kwenye barabara kuu akielekea Chato," alisema Jongo.
Kamanda Jongo alitoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka kutokea vifo visivyo vya lazima. Kila mmoja anapaswa kuelewa thamani ya maisha yake na watumiaji wengine wa barabara badala ya kusubiri kusimamiwa na askari wa Jeshi la Polisi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk. Madili Sakumi, akithibitisha kupokea miili ya watumishi hao wawili ambao ni Diana John muuguzi wa hospitali hiyo pamoja na Egidia Grevas (mtaalamu wa maabara wa Kituo cha Afya Bwina.
Baadhi ya marafiki wa marehemu hao walisema kuwa wawili hao walikumbwa na umauti huo wakati wakielekea nyumbani kwa Egidia kwa ajili ya kupata chakula kusherehekea sikukuu ya Eid Al-adha, wakitumia usafiri wao wa pikipiki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED