WATU watatu wamefariki dunia papo hapo huku mmoja akijeruhiwa kwa kukatika miguu yote katika ajali iliyohusisha malori mawili iliyotokea katika eneo la Manzese Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga barabara kuu iendayo Rwanda, Burundi, Uganda na Kongo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema tukio hilo lilitokea majira ya saa tano na nusu asubihi likihusisha malori mawili, moja likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Runzewe na lingine likitokea mkoani Kagera likielekea jijini Dar es Salaam.
Magomi amesema gari lililokuwa likitokea Dar es Salaam lenye namba za usajili T.854 DBY na tela namba T.180 DVH lilikuwa likiendeshwa na Rajab Tabu kuwa lilikwepa gari la mchanga bila kuchukua tahadhari hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na gari lenye namba T.195 EEY na tela namba T.811 SYU lililokuwa likitokea Bukoba na mzigo wa kahawa.
Amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kwa kuteketea na moto papo hapo kuwa ni pamoja na Rajab Tabu, Khalfani Mikidadi na na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Adam.
Amesema Omari Haji aliyekuwa katika gari lililokuwa linatokea Bukoba kwenda Dar es Salaamu akivunjika miguu yote miwili na yuko katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama akiendelea na matibabu.
"Watu hawa watatu wamekufa kwa kuteketea kwa moto uliosababishwa na ajali hii.Niwasisitize madereva wote wawapo barabarani kuchukua tahadhari safarini kwani wamekuwa chanzo cha kusababisha vifo visivyo vya lazima na kuacha wategemezi kwenye familia zao," amesisitiza Magomi.
Makaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, Hafidhi Omary amesema alipata taarifa za ajali hiyo kutoka kwa wananchi na kukimbia kwenye tukio kuzima moto uliokuwa unaendelea kuteketeza watu waliokuwa kwenye magari na kufanikiwa kuuzima.
Amesema katika ajali hiyo walifanikiwa kuokoa majeruhi wawili ambao wapo katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, wakiendelea na matibabu waliokuwa katika gari lililokuwa linatokea Dar es Salaam kuelekea Runzewe-Geita isipokuwa walikuwa kwenye gari lililokuwa linatokea Bukoba waliteketea wote kwa ajali ya moto.
Shuhuda wa ajali hiyo, Samweli John, amesema yeye anaishi jirani na ajali ilipotokea alisikia kishindo kikubwa cha magari yakigongana na kisha moto kuwaka katika gari lililokuwa likitokea Bukoba na kuchukua hatua ya kuutoa taarifa Jeshi la Polisi na Zimamoto waliofika mara moja kutoa msaada.
Amesema alisikia kelele za maumivu ya madereva waliokuwa wakiteketea na moto wakiomba msaada wakati huo, na walikuwa wamebanwa na vyuma vya bodi la gari na hawakuwa na uwezo wa kutoka na wote waliteketea akiwashuhudiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED