Watatu kortini wakidaiwa kusafirisha dawa za kulevya

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 05:52 PM Apr 23 2024
Watuhumiwa wa kesi ya Uhujumu Uchumi kwa kusafirisha Dawa za kulevya aina ya Methemphetamine Kilo 424.84 pamoja na Heroine Hydrochloride gram 158.24,  Rajabu Kisambwanda (kulia) Bakari Said ( katikati) na Hillary Rhite,  wakielekea katika Mahakamani.
PICHA: IMANI NATHANIEL
Watuhumiwa wa kesi ya Uhujumu Uchumi kwa kusafirisha Dawa za kulevya aina ya Methemphetamine Kilo 424.84 pamoja na Heroine Hydrochloride gram 158.24, Rajabu Kisambwanda (kulia) Bakari Said ( katikati) na Hillary Rhite, wakielekea katika Mahakamani.

WATU watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, mkoani Pwani, wakikabiliwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Methemphetamine kilo 424.84; pamoja na Heroine Hydrochloride gram 158.24.

Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Mkhoi 

Wakili wa Serikali, Agness Ndanzi, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Rajabu Kisambwanda (42) mkazi wa Kerege Matumbi, Bakari Said (39) mkazi wa Kunduchi Mtongani na Hillary Rhite (35) mkazi wa Kunduchi Sodike.

Aidha, imeelezwa kuwa washtakiwa hao watatu walikutwa wakisafirisha dawa hizo Aprili 10 mwaka huu, wilayani Bagamoyo, katika Mkoa wa Pwani.

Wakati huo huo mnano Aprili 10, 2024, katika eneo la Kunduchi, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa Bakari Said amedaiwa kukutwa akisafirisha dawa za kulevya aina Heroine Hydrochloride gram 158.24.

Hata hivyo washtakiwa wote hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi yao inahusu uhujumu uchumi na kwamba haina dhamana, hivyo waendelea kukaa mahabusu hadi Mei 7 mwaka huu.