ZAIDI ya wafanyabiashara 900 wanaodai majina yao kutokuwamo kwenye orodha ya kurejea Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, jana wamekusanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, kudai haki yao.
Walikusanyika kwenye viwanja hivyo kuhakiki majina yao kwenye orodha kama tangazo la Shirika la Masoko Kariakoo lilivyoelekeza juzi, huku wakieleza kutoridhishwa na utaratibu huo.
Katika eneo hilo, wafanyabiashara hao walipindua meza na viti na kuandamana kuelekea Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Lumumba, wakiimba “Tunataka haki yetu.”
Walidai kuwa walihamishwa katika soko hilo baada ya kuungua Julai mwaka 2021 na kupelekwa kwenye masoko mbalimbali kupisha ukarabati na ujenzi wa jengo jipya la ghorofa sita.
Ajali hiyo iliteketeza mali zote za wafanyabishara na serikali ilitenga Sh. bilioni 28 kwa ajili ya ukarabati.
Juzi, Shirika la Masoko Kariakoo lilitangaza kwenye tovuti yake kuwa timu maalum ya Ofisi ya Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam imekamilisha kazi na kutangaza majina ya watu wenye sifa ya kupewa vibanda vya biashara katika soko hilo.
Shirika hilo lilitoa tangazo la wito kwa wafanyabiashara kwa ajili ya kutangaziwa orodha ya majina 1,806 na wenye sifa na vigezo vya kurejeshwa kwa mujibu wa tangazo hilo ni wafanyabiashara 891.
Aidha, kabla ya kamati kufika kwenye kikao kwa ajili ya kusoma majina, wafanyabiashara hao walianza kuondoka na baadaye kwenda Ofisi ya CCM Lumumba.
Akizungumza na wafanyabiashara hao jana, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliwataka leo kufika kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuanzia saa mbili asubuhi ili kuhakikisha haki ya kila mmoja inapatikana.
“Cha msingi ni kuzingatia haki zetu. Kama kuna maombi kwa serikali na sisi tutawasilisha kwa Rais Samia na yeye ndiye atakayetuambia kinachoendelea. Mkuu wa Mkoa anawapa pole na kesho (leo) kuanzia saa mbili asubuhi mtaonana naye.
“Mmekimbilia eneo salama. Mmekimbilia Chama Cha Mapinduzi (CCM) nyumbani, ninawapigia makofi kwa kukimbilia nyumbani, niwahakikishie Rais Samia hapendezwi wala kufurahishwa na jambo lolote la Mtanzania kunyang’anywa au kupokwa haki yake ya msingi.
“Hiki kitendo chote kinachoonekana si cha kiungwana hakiendi serikalini hata kwa mtu mmoja mmoja, mara zote serikali ya wilaya na mkoa tumekuwa tukitatua changamoto,” alisema Mpogolo.
Aidha, alisema maisha ya soko ni mtoto, baba na mama na wanatambua kuwa kuna watu wenye uwezo mkubwa na mdogo na jukumu la serikali ni kuhakikisha wanakua kiuchumi na kulea familia zao.
“Mmesema mmeleta malalamiko yenu kwa mama (Rais) yaani mlezi, mmesema hamjaridhishwa na idadi mlikuwa kwenye uhakiki wa mwanzo baadhi hawaonekani.
“Ni haki kwa mtu kujua mwenzake ametolewaje. Kama viongozi wa serikali chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, tutakwenda kuzingatia haki zetu kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake. Mlipopata changamoto aliwakimbilia na kwa kutambua majukumu yenu kwa kutambua mliishiwa alitoa Sh. bilioni 28, mjengewe soko jipya na kukarabati la zamani,” alisema.
Juzi, Chalamila katika mkutano wa hadhara ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, alitangaza utaratibu mpya wa wafanyabiashara kuingia sokoni humo kuwa ni kulipa madeni kwanza.
Alisema masoko mengi hayafanyi vizuri kutokana na kuvamiwa na madalali na kwamba, wapo waliojenga kwenye vibanda katika maeneo ya serikali na kusababisha migomo ya kutokulipa na sasa mkoa umeweka mkakati mzuri wa kutibu tatizo hilo.
Chalamila alisema ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 96 na litakapokamilika wataingia wa zamani na wapya watakaohitaji na kipaumbele kitakuwa ni kulipa madeni.
Kwa mujibu wa tangazo kwenye tovuti ya shirika hilo iliyotolewa na Menejimenti, “Wafanyabiashara wanaodaiwa na shirika ambao wapo kwenye orodha hii wanajulishwa kuwa hawatarejeshwa sokoni hadi watakapolipa madeni ya kodi waliyolimbikiza kwa muda mrefu.
“Shirika linatoa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo Julai 10, 2024 hadi Agosti 9, 2024 kwa wadaiwa wote kukamilisha malipo ya madeni yao. Kwa wafanyabiashara wenye hoja au maoni kuhusu majina yao kutoonekana kwenye orodha ya uhakiki,
“Shirika linatoa muda wa siku tatu kuanzia Julai 11 hadi 13, 2024 kuwasilisha madai yao. Maofisa wa shirika watakuwapo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 9.00 alasiri kusikiliza na kutoa ufafanuzi kwa wafanyabiashara,” ilisema taarifa hiyo.
Tangazo hilo lilitaja majina ya wafanyabisahra 212 ambao waligawanywa katika makundi sita ikiwa ni watakaokaa eneo la soko kuu, vigoli, soko dogo ndani, soko dogo mzunguko, soko la wazi na shimoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED