Waandishi wafundwa miiko, maadili uchaguzi

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:44 AM Jun 15 2024
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Andrew Kisaka.
Picha: Mtandao
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Andrew Kisaka.

SERIKALI imewasisitiza waandishi wa habari kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa habari wakati wa mchakato wa uchaguzi na baada ya kumalizika kwa mchakato huo ili kuhakikisha nchi inabaki kwenye amani na utulivu.

Akizungumza kwenye mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Habari Maelezo, Patrick Kipangula, alisema waandishi na vyombo vya habari vina jukumu la pekee kuhakikisha nchi inabaki na amani, utulivu na mshikamano kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Alisema hilo litawezekana kama wagombea na vyama vya siasa vitapewa nafasi sawa ya kutangaziwa habari zake bila upendeleo.

Kipangula aliwataka waandishi kuzingatia ukweli, uadilifu, uaminifu, weledi na usahihi wa taarifa na kuepuka rushwa pamoja na kuheshimu faragha za watu.

“Tuepuke taarifa ambazo zinaweza kuvunja amani na usalama wa nchi. Tunatakiwa kuhakikisha Taifa letu linabakia tulivu na salama wakati wote wa mchakato na baada ya uchaguzi,” alisema.

Kadhalika, amewataka kuchukua tahadhari na kuthibitisha taarifa kabla ya kuitangaza au kuichapisha, kwa kuwa baadhi ya watu wanaweza kutumia akili mnemba kutengeneza picha zenye nia ovu dhidi ya vyama au baadhi ya wagombea.

Awali, Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Andrew Kisaka, alisema vyombo vya habari vinaaminika na jamii na hivyo vina nafasi ya kuunganisha nchi kwenye masuala yote ya kitaifa na maendeleo.

Alisema wakati huu wa zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura, waandishi na vyombo vya habari wanao uwezo wa kuwapa wananchi taarifa za faida za kujiandikisha na kupiga kura.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mtibora Selemani, alisema INEC itatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari na wadau wote wa tume wakati wa uboreshaji wa daftari na kwenye mchakato wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa INEC, maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura yanatarajiwa kuzinduliwa Julai Mosi, mwaka huu mkoani Kigoma.

Juzi, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, aliwataka wanahabari kutumia fani yao kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura.

“Tume inataajia ushirikiano mkubwa kutoka kwenu kwa kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,” alisema.